Na, Hamad Rashid.
Wadau wa masuala ya Elimu na malezi na makuzi ya vijana nchini
wamepokea kwa mshtuko matokeo ya upimaji mahili za Stadi za maisha na maadili
kwa vijana, baada ya Ripoti iliyotolewa na Taasisi ya Milele Zanzibar
Foundation kubaini vijana waliohojiwa wengi wao, viwango vyao vya kujitambua,
utatuzi wa matatizo, ushirikiano na Heshima viko chini katika pande zote za
Bara na Visiwani.
Katika muktadha huo Ripoti hiyo ya Mradi wa ALIVE katika kipengele cha
Utatuzi wa Matatizo Tanzania Bara, imebaini Karibu 6 katika 10 ya vijana
hawawezi kutambua uwepo kwa tatizo kutoka kwa mtazamo mmoja na hivyo
wanashindwa kutambua suluhisho linalowezekana kutatua tatizo hilo.
Aidha katika upande wa Tanzania Zanzibar kipengele cha “Kujitambua’’
Ripoti imebaini kijana mmoja kati ya watano ndiye mwenye ufahamu wa kujitambua
(kutoka katika Kiwango cha 3 cha upimaji), ilhali wengi wanaweza kudhibiti
athari zinazotokana na hisia, lakini hawajui njia nyingi ambapo wengine
wanaweza kutambua.
MAPOKEO YA RIPOTI KATIKA MAKUNDI MBALIMBALI
Neema Mchau ni Mzazi kutoka Jijini Dar es salaam, alisema alipatwa na
mshtuko baada ya kuona hali mbaya ya matokeo ya vijana wa umri wa miaka 13-17, kuwa
na viwango vya chini katika suala la Stadi za Maisha na Maadili.
“Kimsingi kama Mzazi nimepokea kwa mshtuko, kwa sababu Ripoti ile
imeonekana ina mapungufu mengi kwa watoto wetu, kama mzazi na mdau wa Elimu
imenishtua sasa nimejiangalia nikasema, lakini hili ni tatizo lililopo kwenye
Jamii yetu na sisi kama wazazi lazima tujitathmini kwamba tumekosea wapi, wale
ni watoto bado wako chini yetu na tunahitaji kuwaongoza, niwakumbushe wazazi
wenzangu tusiwalee watoto kama Ndege tukawaacha wakazubaa maana wazazi tumekua
bize sana kutafuta maisha” Alisema Neema Mchau.
Naye Mwalimu kutoka Skuli ya Mikunguni iliyopo Unguja Asha
Mussa Ally alizungumzia matokeo ya Ripoti ya ALIVE na kueleza mbinu zinazoweza
kutumiwa na walimu kuwafundisha wanafunzi Stadi za Maisha na Maadili Shuleni. “Ripoti
ya ALiVE haikua nzuri kwa sababu Stadi za Maisha kwa wanafunzi ambao
tumewafanyia utafiti zilikua chini kabisa, na kuna vipengele vingi ambavyo
vinasababisha hali hiyo kwa upande wa walimu, wazazi na Jamii, kwa hivyo sisi
walimu tunachotakiwa ni kuboresha mbinu za ufundishaji darasani na tuweze
kuwahusisha zaidi wanafunzi kuliko sisi walimu, mbinu ambazo zitafanya
wanafunzi waweze kushirikiana kwa pamoja, kwa sababu kitu kinachoonekana kwa
sasa wanafunzi wenyewe kwa wenyewe wanaogopana, kwa mfano ukimsimamisha mmoja
kujibu swali mwingine anacheka, kwa sababu hawana uelewa kama kusoma ni kwa
pamoja na hata mtu hajui wanatakiwa washirikane”
Katika upande mwingine, Mwanafunzi wa Kidato cha pili Muznati
Salim Hamad kutoka katika Skuli ya Sekondari Mikunguni iliyopo Unguja alieleza
namna Jamii na Sekta ya Elimu zinavyopaswa kuwajibika kuwafundishwa vijana
Stadi za Maisha.“Kwa Stadi za maisha na maadili kushuka kwa wanafunzi au vijana katika
mitaa kwa mtazamo wangu mimi, katika ulimwengu mzima hii inakua kutokana na
Jamii inavyowaweka vijana wao, kama Jamii imekaa hivi na vijana na wale vijana
wataenda hivyo hivyo, kama Jamii itakua haishughulikii Stadi za Maisha maana
yake vijana watakua hawana Stadi za Maisha, kama vile kujithamini kwa hivyo,
naishauri Jamii ya kwamba masuala haya yawe yanafundishwa sehemu zote za Jamii
kwa wazazi na masheha na katika Skuli zetu” Alisema Muznati Salim Hamad. Mwanafunzi
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Guluka
kwalala Kata ya Gongo la Mboto Augustino Simba alisema, Stadi za maisha ni
muhimu vijana wakaanza kufundishwa shuleni kama ilivyo masomo mengine ili
kukabiliana na suala la mmomonyoko wa maadili kwa vijana.
Augustino Simba alisema “Elimu kama hii ya Stadi za Maisha
isilengwe kwa hawa wa mitaani, iende hadi kwenye Shule za Msingi na Sekondari,
kwa sababu kule ndio kwenye jumuiko kubwa la vijana, na matukio mengi yanatokea
katika maeneo yale hasa wakati wa mwanafunzi kutoa au kwenda Shule, mimi naomba
kwenye Mtaala wa Elimu Somo kama hili liwepo Shuleni na kuwe na walimu maalumu
wa kufundisha kama wanavyofundisha masomo mengine, naamini vijana wengi
watabadilika kujitambua kwao”
Aidha, akizungumza katika Mahojiano wakati wa uzinduzi wa
Ripoti ya ALiVE Halmashauri ya Wilaya ya Ilala, muwakilishi wa Afisa Elimu
Sekondari Jiji la Dar es salaam Festo Mlimila alipokea vyema suala la Somo la
Stadi za Maisha na Maadili kufundishwa katika Shule nchini.
“Nafikiri ni Mradi mzuri kujadili Stadi za Maisha hasa ukizingatia hali
ya sasa iliyopo kutokana na mmomonyoka wa maadili kama mnavyosikia kuna masuala
mazima ya ukatili wa kijinsia katika Jamii ambao wengine wanakua ni wanafunzi,
kama utafiti ulivyofanyika kupima vijana wa umri wa miaka 13-17, Idara ya Elimu
ya Msingi na Sekondari kwa ujumla, hili jambo tumelipokea vizuri kupitia Taasisi
ya Milele Zanzibar Foundation na itatusaidia kuwezesha watoto wetu kuwa na
maadili mema na waweze kujifunza vyema wanapokua mashuleni” Alisema
Festo Mlimila
KINACHOFUATA
BAADA YA MATOKEO YA MRADI WA ALIVE
Mipango ya Taasisi ya Milele Zanzibar Foundation (MZF) sasa
ni kusonga mbele katika kuzalisha wataalamu watakaoweza kufundisha Stadi za
Maisha kutoka Afrika, alisema Msimamizi wa Miradi kutoka MZF Khadija Shariff
alipohojiwa na Tanzania Kids Time Ofisi kwake Mbweni Unguja.
Khadija Shariff alisema
“Sasahivi Duniani kuna mwamko mkubwa
kuhusu Stadi za Maisha na maadili, hizi ni mahili ambazo zinajulikana Duniani
zinahitajika kwa ajili ya kuleta maendeleo makubwa, kwa hivyo wenzetu huko
Ulaya na Mabara mengine wameshaanza kuwa na wataalamu wakutosha, jamba ambalo inabidi
tuwalete wao hapa kuja kutusaidia sisi”
Khadija Shariff-Msimamizi wa Miradi-MZF.
Khadija aliongeza kuwaLakini “Sisi kwa sasa tumejikita katika
kujenga wataalamu safari hii, ili tuweze Kujitegemea wenyewe tuweze kuzalisha
zile mbinu za upimaji ambazo zitakua zinaendana na mazingira yetu na tutafanya
hivyo kupitia kitu kinaitwa, ALiVE Accademy itakua chuo ambacho kwa sasa
kitaanza kutoa mafunzo yake kupitia njia ya Mtandao”