Athari za mabadiliko ya tabia nchi yanayotokana na kuharibika kwa ozoni leya yamepelekea miale ya jua kupenya moja kwa moja kwenye ardhi na yameendelea kuonekana katika mikoa mbalimbali nchini Tanzania, miongoni mwa athari zinazo zaniwa kuchangiwa na mabadiliko hayo ni ongezeko la mama wajawazito kujifungua kabla ya wakati.
TATIZO NI NINI?
Mapema mwezi October Mwaka huu nchini Tanzania mashirika yasio ya kiserikali yamezindua mpango wa kufanya utafiti wa pamoja kuhusu athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi kwa watoto, mpango huo ukisimamiwa na taasisi ya Doris Mollel Foundation kwa msaada wa ubalozi wa uingereza nchini Tanzania.
Doris Mollel ni mkurugenzi wa Shirika la Doris Mollel Foundation, anasema “utafiti umefanyika unaonesha kwa kiansi kikubwa sana wakina mama wengi wanaokaa kwenye mazingira yenye hali ya hewa ambayo sionzuri, inawapelekea kujifungua kabla ya wakati hasa wanaokaa maeneo ya viwanda”.
Kwa mujibu Shirika la afya duniani (WHO) Mwaka 2020 pekee, zaidi ya watoto 336,000 walizaliwa kabla ya wakati nchini Tanzania, na zaidi ya watoto 11,500 kati yao walifariki dunia, moja kati ya sababu zinazotajwa kuchangia Mama mjamzito kujifungua kabla ya wakati yaani mtoto ambae hajafikia wakati wake kamili wa kuzaliwa (mtoto njiti) ni ongezeko la joto.
CHANZO CHA TATIZO HILI NI NINI?
Utafiti unaonesha kwamba kwa miongo kadhaa uchafuzi wa hewa, hasa chembechembe ndogo zinazoweza kuning’inia hewani, zinaweza kuingizwa ndani ya mapafu ya binadamu hasa kwa mama mjamzito kwani huitaji hewa Zaidi, zinaweza kuongeza hatari ya mtoto kuzaliwa kabla ya wakati.
Ripoti ya Hali ya hewa ya Dunia ya mwaka 2020 iligundua kuwa uchafuzi wa hewa husababisha 20% ya vifo vya watoto wachanga duniani kote takriban vifo 500,000 vya watoto wachanga mwaka wa 2019, vilihusiana zaidi na matatizo ya kuzaliwa kabla ya wakati na uzito pungufu.
Nae Dr. Sylvia Ruambo yeye anatoka katika shirika la Support for Future Foundation ambalo nimiongoni kati ya mashirika yatakayo shiriki katika mpango huo wa utafiti, anasema lengo hasa la kujumuika na kufanya utafiti huo kwa pamoja nikuendelea kuisaidia jamii na hasa pale tatizo linapo julikana nirahisi kulitatua kwa pamoja kushirikiana na serikali.
Kwa mujibu wa ripoti ya hali ya hewa barani afrika ilio chapishwa na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) mapema mwezi September mwaka huu, ukrasa wa 15 unaonesha jinsi joto lilivyo ongezeka na kusababisha barafu ya mlima Kilimanjaro nchini Tanzania, hadi sasa kushuka kutoka kwenye kiwango chake cha zamani cha urefu wa kilomita 11.40 kilicho kuwepo tangu mwaka 1912 hadi kufikia kilomita 1.76 mwaka 2011, hasara ilio patikana ni takriban 85% ya barafu imepotea katika kipindi cha miaka 100 iliyopita.
Hali hii imesababishwa na mabadiliko ya hali mbaya ya hewa kamavile shughuli za kibinadamu, upotevu wa viumbe hai, uchafuzi wa mazingira kwa kueneza kemikali, uharibifu wa tabaka la ozone, ukataji miti, hivyo kupelekea ongezeko la joto kali na kusababisha athari kwa mama mjamzito kulazimishwa kujifungu kabla ya wakati kutokana na uvutaji wa hewa chafu iliojaa chembechembe za kemikali na hewa nzito.
Muakilishi wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa nchini Tanzania bi, Clara Makenya anabainisha uhusiano uliopo katika ya mabadiliko ya hali ya hewa na watoto, anasema “sisi kama umoja wa mataifa tunaona uhusiano wa karibu sana kati ya mabadiliko ya tabianchi na athari zake kwa watoto, tuanafahamu kwamba kunaathari kwa wanadamu wote kwa ujumla.
Lakini ikifika kwa watoto na akina mama zinaweza kuwa kubwa Zaidi, takwimu zinaonesha kwamba kati ya watoto wanne 4 mmoja anaweza kua anafariki kutokana na changamoto zinazo tokana na mabadiliko ya tabianchi, mfano, mvua zinapo nyesha kupitiliza, magonjwa, mafuriko nk”.
HALI ILIVYO KWA MAMA WAJAWAZITO NCHINI TANZANIA.
Kiwango cha kuzaliwa kabla ya wakati kinaongezeka duniani kote kwa sasa, kulingana na Shirika la Afya Duniani -WHO, mtoto 1 kati ya 10 huzaliwa kabla ya wakati, na viwango vyao vya kuishi ni chini ya 40%. Nchini Tanzania pekee, vifo vya watoto wachanga sasa vinachangia hadi 40% ya vifo vyote vya watoto chini ya miaka mitano kila siku.
Daktari wa Watoto kutoka hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dr. Robert Moshiro amesema mama kujifungua kabla ya wakati kuna sababu nyingi miongoni kati ya hizo, ni magojwa ya kuambukiza, kuwa na watoto Zaidi ya mmoja au Zaidi ya watoto wawili tumboni, mbali na hayo kuna uhusiano mkubwa kati ya ongezeko la joto na mama mjamzito kujifungua kabla ya wakati.
RIPOTI MPYA DHIDI YA ONGEZEKO LA JOTO DUNIANI.
Kwa mujibu wa Ripoti mpya iliyozinduliwa jijini New York Marekani mwezi huu na shirika la UNICEF , na kuchapishwa pia kwenye tovuti ya Un news Kiswahili imeonesha kuwa watoto milioni 559 kwa sasa wanakabiliwa na joto Kali.
Hali hiyo inategemewa kuwa mbaya zaidi ambapo mpaka kufikia mwaka 2050 watoto wote duniani ambao wanakadiriwa kuwa bilioni 2.02 watakuwa wameathiriwa, na mawimbi tofauti ya joto kali bila kujali wapo kusini au kaskazini mwa dunia na vile vile bila kujali ongezeko la joto litakuwa katika kiwango cha wastani wa nyuzi joto 1.7 katika kipimo cha Selsiyasi au kiwango cha juu cha nyuzi joto 2.4 katika kipimo cha Selsiyasi.
Ripoti hiyo iitwayo Mwaka wa baridi zaidi katika maisha yao yote: kuwalinda watoto kutokana na athari zinazoongezeka za misimu ya joto imeangazia athari ambazo tayari zimedhihirika kwa watoto na kuonesha kuwa hata katika maeneo ambayo kuna viwango vidogo vya joto katika kipindi cha miongo mitatu athari za jua haziwezi kuepukika.
Ripoti hiyo iliyotolewa na UNICEF ni ushirikiano baina yake na shirika jingine liitwalo The Data for Children Collaborative ambapo akizungumza kuhusu ripoti hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell amesema wakati joto linazidi kuongezeka kuna athari pia ya ongezeko la zebaki. “Tayari, mtoto 1 kati ya 3 anaishi katika nchi ambazo zinakabiliwa na hali ya joto kali na karibu mtoto 1 kati ya 4 wanakabiliwa na misimu mikubwa ya joto, na hali itazidi kuwa mbaya zaidi.”
SULUHISHO LA TATIZO HILI NILIPI? UNICEF INASHAURI.
Serikali kuwalinda watoto dhidi ya uharibifu wa hali ya hewa kwa kufanya marekebisho kwenye huduma za kijamii. Kila nchi lazima ibadilishe huduma muhimu za kijamii ambazo ni maji, usafi wa mazingira na usafi (WASH), afya, elimu, lishe, ulinzi wa kijamii na ulinzi wa mtoto – ili kulinda watoto na vijana. UNICEF imesema katika mkutano wa COP27 utakao fanyika wiki chache zijazo, watoto na haki zao lazima zipewe kipaumbele katika maamuzi ya kukabiliana na hali hiyo.
Serikali lazima ziandae namna ya watoto kuishi katika ulimwengu unaobadilika-badilika. Kila nchi lazima iwape watoto na vijana elimu ya mabadiliko ya tabianchi, elimu ya kupunguza hatari ya majanga, mafunzo ya ujuzi wa kijani na fursa za kushiriki kikamilifu na kushawishi uundaji wa sera za mabadiliko ya tabianchi. COP27 lazima ione nchi zikiimarisha mwelekeo wa elimu ya tabianchi ya watoto na kutekeleza ahadi za awali za kujenga uwezo wa vijana.
Serikali lazima ziweke kipaumbele kwa watoto na vijana katika utoaji wa fedha na rasilimali za mabadiliko ya tabianchi. Nchi zilizoendelea lazima zitekeleze ahadi zao walizoweka kwenye COP26 ya kuwa watafadhili wa dola bilioni 40 kwa mwaka ifikapo 2025 kwa kiwango cha chini, ikiwa ni hatua ya kuelekea kwenye kutoa angalau dola bilioni 300 kwa mwaka kwa ajili ya kukabiliana mabadiliko ya tabianchi ifikapo mwaka 2030.
Serikali lazima zijitahidi kuzuia janga la hali ya hewa kwa kupunguza kwa kiasi kikubwa utoaji wa gesi chafuzi na kuweka lengo la viwango vya Celsiasi 1.5 hai. Uchafuzi unatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 14 katika kipindi cha muongo huu, hali inayoiweka dunia katika njia ya janga lajoto duniani. Serikali zote lazima ziangalie upya mipango na sera zao za mabadiliko ya tabianchi za kitaifa ili kuongeza matamanio na hatua zaidi za kukabiliana na janga hili. Ni lazima nchi ziwe tayari kupunguza utoaji wa hewa chafuzi kwa angalau asilimia 45 ifikapo mwaka 2030 ili kuweka joto lisizidi nyuzi joto 1.5.
Na, John Kabambala.