Hasira inazidi kuongezeka nchini Somalia wakati bunge likipanga kuujadili muswada wa sheria ambayo itaruhusu ndoa za watoto mara baada ya kubalehe, na kuruhusu ndoa za lazima ilimradi familia itoe ridhaa yake.
Muswada huo unatajwa kuwa mabadiliko makubwa katika jitihada za mashirika ya kiraia za kuwasilisha pendekezo la sheria ya kuwalinda zaidi wanawake katika moja ya mataifa ya kihafidhina zaidi duniani.
Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu vurugu za kingono katika maeneo ya migogoro, Pramila Patten, amesema muswada huo mpya wa makosa yanayohusiana na ngono, “utakuwa ni pigo katika mapambano dhidi ya ukatili wa kingono nchini Somalia na duniani kote” na unapaswa kuondolewa haraka”.
Kulingana na tathmini ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2014-2015, zaidi ya asilimia 45 ya wasichana nchini Somalia tayari wameolewa katika umri mdogo wa chini ya miaka 18.
Somalia ilikubaliana na Umoja wa Mataifa mwaka 2013 kuboresha sheria zake zinazohusiana na vurugu za kingono, na baada ya miaka mitano ya juhudi, muswada wa makosa ya kingono uliidhinishwa na baraza la mawaziri na kutumwa bungeni.
Chanzo cha habari ni Idhaa ya Kiswahili ya DW.