Ombi hilo limetolewa kwenye mkutano wa siku mbili mjini Berlin, Ujerumani unaohudhuriwa na mashirika ya kimataifa, serikali na asasi za kiraia ukiwa na lengo la kusaka michango zaidi ya kibinadamu kwa ajili ya wathirika wa mzozo katika bonde la Ziwa Chad.
Kwenye mkutano huo unaokunja jamvi leo, UNICEF imeonya kuwa mzozo unaoendelea, ukilazimisha watu kukimbia makwao na kuhatarisha shule kushambuliwa unatishia fursa ya elimu kwa watoto zaidi ya milioni 3.5, hasa wakati huu ambapo takribani shule 1,000 zimefungwa kaskazini Mashariki mwa Nigeria, Chad, Cameroon na Niger.
Manuel Fontaine, Mkurugenzi wa mipango ya dharura ya UNICEF amesema wakati wa mizozo, elimu yaweza kusaidia maisha kuendelea na kuwa mwokozi wa maisha kando na kutoa fursa za elimu ya maisha kwa watoto.
Ameongeza kwamba elimu huwapatia ujuzi unaofaa kuwasaidia kujenga mustakbali wao na familia zao kinachochangia kwa ujenzi wa amani na uwepo wa jamii endelevu.
Fontaini amesema licha ya umihimu wa elimu, ufadhili wa kibinadamu katika sekta hiyo mara nyingi huwa finyu wakati wa dharura.
Naye Marie-Pierre Poirier, Mkurugenzi wa kanda ya Afrika Magharibi na Kati wa UNICEF, amezitolea wito nchi kutia saini mkataba wa Shule Salama na kuweka mikakati ya kuhakikisha usalama wa watoto shuleni hata wakiwa mzozoni.
Ingawa hali ya usalama imeimarika katika Bonde la Ziwa Chad, watu zaidi ya milioni 10 wakiwemo watoto milioni 6 bado wanahitaji misaada ya kibinadamu huku wengine milioni 2.4 waliolazimika kukimbia makwao.Taarifa hii nikwamjibu wa radio washrika Umoja wa Mataifa UN RADIO jijini New York Marekani.