Hali ya kibinadamu nchini Syria imefikia pabaya, mlo ni dhiki, malazi tabu
na watoto wanaendelea kulipa gharama kubwa ya vita yameonya leo mashirika ya
umoja wa Mataifa.
Kwa mujibu wa mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa
(OCHA) nchini Syria Panos Moumtzis, wamezidiwa uwezo katika kukabiliana na
changamoto za kibinadamu na hali ni mbaya kwani wamejikuna na mkono umefika
mwisho.
“Tuna kidogo cha kushibisha
sasa tu , maghala ni matupu , tunafanya kazi usiku na mchana kwa kila upande,
tumekuwa na timu zinazofanya kazi, zinapokea saa tita alfajiri idadi kubwa ya
watu, na daima tunajaribu kupata mahali pa kuwahifadhi kwenye jumuiya za
wenyeji, kwenye majengo yaliyo tupu, kwenye makambi, tunatumia kila sehemu
inayowezekana ya Idlib ili kuweza kuwapokea, kuwahifadhi na kushughulikia
mahitaji yao.”
Nalo shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa
UNICEF limesema, watoto nchini humo wameendelea kulipa gharama kubwa ya vita
kila uchao. Mkurugenzi wa kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini wa
shirika hilo Geert Cappeleaere’ amesema wamepokea taarifa kuwa watoto 13
wameuawa siku chache zilizopita katika mashambulio yanayodaiwa kulenga vijiji
na katika shambulio la Kijiji cha Zardana Kaskazini Magharibi mwa Idlib maisha
ya watoto 9 yamekatiliwa Jumapili .
Amesisitiza kuwa huu ni ukiukaji mkubwa wa haki za watoto ambao wengi
wamesambaratishwa na vita na hawana mahali pengine pa kwenda isipokuwa kupata
hifadhi kwenye makambi ya wakimbizi na mashuleni. Hali hii amesema
inadhihirisha kwamba vita dhidi ya watoto Syria havina dalili yoyote ya
kumalizika.Taarifa hii nikwanjibu wa UN Radio.