Na, John Kabambala: Sekta ya
Afya ni muhimu katika ustawi wa watu, uimarishaji wa nguvu kazi na ukuzaji wa
maendeleo ya taifa. Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuboresha
utoaji wa huduma za afya ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vituo vipya vya afya,
ukarabati wa vituo vilivyopo, utoaji wa vifaa tiba na upatikanaji wa dawa
muhimu.
Katika
tathmini kuhusu mwenendo wa utoaji huduma za afya katika Mamlaka za Serikali za
Mitaa; ilibainika kuwa, pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali katika
kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya, sekta ya afya bado inakabiliwa
na changamoto mbalimbali zikiwemo upungufu wa wataalamu, ufinyu wa bajeti,
mazingira duni ya kazi, upungufu wa miundombinu na uhaba wa dawa na vifaa tiba.
Makala hii
inaangazia juu ya changamoto zinazoonekana katika sekta ya afya, na inabainisha
maeneo muhimu ambayo yanahitaji kusimamiwa kwa umakini na kupendekeza hatua
zinazopaswa kuchukuliwa na Serikali na wadau wengine ili kutatua changamoto zilizobainika.
HATUA ZA KUPUNGUZA VIWANGO VYA VIFO
VYA WAJAWAZITO NA WATOTO WACHANGA.
Kwa
mujibu wa Mwongozo wa mapitio ya vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto
wachanga uliotolewa Oktoba 2019 unaeleza kuwa Kifo cha Mama mjamzito ni kifo
cha mwanamke kinachotokea wakati akiwa mjamzito au ndani ya siku 42 baada ya
mimba kutoka, bila kujali miezi ya ujauzito na eneo la ujauzito kutokana na
sababu zinazohusiana au kuchochewa na ujauzito au usimamizi wake, lakini sio
kwa sababu za ajali au sababu zisizozuilika. Vifo vya watoto wachanga ni kifo
cha mtoto mchanga ndani ya siku 28 za kwanza tangu kuzaliwa.
Aya ya 4.4 ya
Mpango wa Taifa wa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto
wachanga wa Mwaka 2021 ‘one plan III’ uliotolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii imeonyesha shabaha ya vifo vya wajawazito kupunguzwa kutoka 250 hadi 100
kwa vizazi hai 100,000. Hata hivyo viwango hivyo vinatofautiana na shabaha ya
vifo 180 kwa vizazi hai 100,000 iliyoelezwa katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo
wa Miaka Mitano wa 2021/22-2025/26.
Kulingana
na takwimu zilizochapishwa kwenye tovuti ya Shirika la Afya Duniani (WHO), hadi
kufikia mwaka 2020, Tanzania ilikuwa na makadirio ya vifo vya wajawazito 238
kati vizazi hai 100,000.
Mpango wa
Taifa wa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga wa Mwaka
2021 ‘one plan III’ unaeleza shabaha ya kupunguza vifo vya watoto wachanga
kutoka 20 kwa vizazi hai 1,000 hadi vifo
15 kwa vizazi 1,000 ifikapo 2025.
Hata hivyo,
viwango hivyo vinatofautiana na viwango tarajiwa katika Mpango wa Taifa wa
Maendeleo wa Miaka Mitano wa 2021/22-2025/26 ambao unaonyesha kuwa Tanzania
imepanga kupunguza vifo vya watoto wachanga kutoka vifo 36 hadi 30 katika
vizazi 1000 ifikapo mwaka 2025/26.
Katika
mwaka 2021/22, ripoti ya mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali ya mwaka 2021/22 ilibainisha
kwamba, kulikuwa na ongezeko la viwango vya vifo vya wajawazito zaidi ya lengo
la vifo 100 kwa kila vizazi hai 100,000 katika Mamlaka 20 za Serikali za Mitaa.
VIWANGO VYA
VIFO HUKADIRIWAJE?
Viwango vya
vifo vya wajawazito katika vizazi hai 100,000 hukadiriwa kwa idadi halisi ya
vifo vya wajawazito vilivyotokea katika vizazi hai halisi kwenye Halmashauri husika. Viwango hivyo vinapatikana
kwa kuchukua idadi ya vifo halisi kugawanywa na vizazi hai halisi na kuzidishwa
na vizazi hai 100,000.
Mfano H/Mji
Geita mwaka 2021, kiwango ni (27/12,931*100,000=209) Licha ya kwamba viwango
vya vifo vya wajawazito katika Mamlaka 13 za Serikali za Mitaa kuwa chini ya
vifo 100 kati ya vizazi hai 100,000, kwa miaka miwili takwimu zilizopatikana
zinaonyesha kuwa idadi ya vifo vya wajawazito ilikuwa inaongezeka na kuashiria
kuwa katika miaka ijayo viwango hivyo vitakuwa juu ya shabaha inayokusudiwa.
Hata hivyo ripoti hiyo inabainisha katika mwaka 2021/22
niligundua viwango vya vifo vya watoto wachanga katika Mamlaka 2 za Serikali za
Mitaa vilikuwa ni vifo 135 na vifo 49 kwa watoto 1000 waliozaliwa ambavyo
viwango vikubwa zaidi kuliko lengo la vifo 30 kwa watoto 1000 wanaozaliwa kama
ilivyoelezwa katika Mpango wa ‘One Plan III’.
Vifo vya
watoto wachanga 6335 katika Mamlaka 20 za Serikali za Mitaa kwa miaka miwili;
hata hivyo, kiwango cha vifo kwa watoto 1000 wanaozaliwa hakikuweza kupatikana
baada ya kukosekana taarifa za idadi ya watoto waliozaliwa. Idadi ya vifo
vilivyotokea ni kubwa inayolazimu kuchukuliwa hatua ili kuondoa vifo vya watoto
wachanga na kufikia shabaha ya vifo 30 kwa watoto 1000 wanaozaliwa.
SABABU ZINAZO
SABABISHA VIFO VYA UZAZI:
Sababu kuu
za vifo vya uzazi ni kuvuja damu wakati wa kujifungua ambayo husababisha zaidi
ya robo moja ya vifo, matatizo ya shinikizo la damu wakati wa ujauzito,
upungufu wa damu wakati wa ujauzito, kifafa cha mimba na magonjwa yanayohusiana
na ujauzito.
Sababu
nyingine ni kuchelewa kwa wajawazito katika vituo vya afya ili kupata huduma ya
matibabu kwa wakati wa uchungu, watoa huduma za afya ya msingi na wakunga
kutokuwa na ujuzi wa kutosha wakati wa kutoa huduma za kujifungua na uhaba wa
dawa na vifaa tiba katika vituo vya afya katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.
INASABABISHA VIFO VYA WATOTO WACHANGA:
Kwa mujibu
wa Mpango wa Taifa wa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto
wachanga wa 2021 ‘one plan III’ kukosa hewa kwa watoto wanaozaliwa ni chanzo
kikuu cha vifo vya watoto wachanga, ikifuatiwa na kuzaliwa kabla ya wakati na
maambuzi ya bakteria.
Vifo hivi
vinaweza kuzuilika kwa kuboresha; upatikanaji wa watoa huduma wenye ujuzi,
ubora wa huduma kwa wajawazito kabla na baada ya kujifungua na matunzo ya
watoto wachanga wanaozaliwa na wanaoumwa. Aidha hatua thabiti zenye ubunifu na
ubora zinahitajika kuchukuliwa ili kuzuia viwango vya vifo vya wajawazito na
watoto wachanga kufikia shabaha inayolengwa ifikapo mwaka 2025/26.
MKAGUZI MKUU WA
HESABU ZA SERIKALI AMEPENDEKEZA KUWA:
“Menejimenti za Mamlaka za Serikali
za Mitaa zihakikishe kuwa huduma bora za afya zinatolewa katika vituo vya afya,
kuwapatia wahudumu wa afya ya msingi maarifa na ujuzi wa kutosha ili kupunguza
vifo vya wajawazito na watoto wachanga.
Kuongeza ufahamu juu ya umuhimu wa wajawazito kuhudhuria kliniki mapema
na kujifungua katika vituo vya afya. Pia, ninashauri Menejimenti za Mamlaka za
Serikali za Mitaa kuhakikisha kuwa fedha zinazohusu shughuli za kupunguza vifo
vya wajawazito na watoto zinatolewa kama ilivyopangwa ili kuondoa/kupunguza
vifo vya uzazi na watoto wachanga kama ilivyolengwa”.