Na Hamad Rashid
Shirika lisilo la kiserikali la Uwezo Tanzania limeratibu kikao na mashirika mengine wanachama wa Mtandao wa Elimu wa kikanda Afrika Mashariki (RELI), kilichofanyika Mkoani Morogoro, kwa ajili ya kujadili na kutengeneza mikakati ya kuwashirikisha wazazi na walezi kuwafundisha watoto stadi za maisha na maadili.
Kupita Mradi wa ALiVE katika awamu yake ya pili (Mradi unaoshughulika na masuala ya stadi za maisha na maadili kwa vijana Afrika ya Mashariki), wanachama hao zaidi ya 20 wa Mtandao wa RELI kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani, katika kikao cha siku mbili watajadili na kuandaa mpango mkakati wa utoaji Elimu kwa wazazi kupitia mashirikisho ya walimu na wazazi, juu ya stadi za maisha na maadili, alisema Gaudence Kapinga Mratibu wa RELI Tanzania.
Kapinga aliongeza kuwa, “Tunatakiwa tufahamu kwamba stadi za Maisha zinaanzia nyumbani na nyumbani ndio kuna wazazi, walezi, ndugu, wanafamilia na Jamii nzima, kisha kuna Shule, tuko hapa na wanachama wa RELI ambao wanafanya kazi katika ngazi ya Jamii kupitia miradi yao mbalimbali, kwa hivyo tunajadili kwa namna gani tutafikia Jamii yetu, wazazi na Shule ili kuhakikisha watoto wapata stadi za Maisha ambazo zitawasaidia kuweza kukabiliana na changamoto za kimaisha wawapo shuleni na katika Jamii”
Meneja wa kitengo cha mawasiliano kutoka Shirika la Uwezo Tanzania, Greyson Mgoi ni miongoni mwa wawezeshaji wa kikao hicho cha kutengeneza mikakati ya kuwashirikisha wazazi katika uelimishaji wa stadi za maisha na maadili.
Kulingana na Afisa miradi mwandamizi katika Mradi wa ALiVE kutoka Shirika la Milele Zanzibar Foundation, Samson John Sitta utafiti uliofanyika Tanzania bara na visiwani Mwaka 2021 kupitia Mradi wa ALiVE katika awamu yake ya kwanza, ulibaini viwango vya chini vya mahili za stadi za maisha na maadili kwa vijana wa Tanzania, ambapo Mradi wa ALiVE katika awamu yake ya pili miongoni mwa maeneo inayojikita nayo ni kuwawezesha wazazi na walezi kuzielewa stadi za maisha na maadili kisha kuzifundisha kwa watoto.
Samson Sitta aliongeza kuwa “Mpango huo unaowahusisha wazazi, ni utekelezaji wa eneo la tatu la Mradi wa ALiVE awamu ya pili, la ukusanyaji wa maarifa tunayojifunza katika mchakato mzima, kuona ni kipi kinafanikiwa katika ufundishaji na utengenezaji wa stadi za maisha na maadili kwa vijana ili kuweza kusaidia wadau mbalimbali wanaoshughulika na masuala ya stadi za Maisha na maadili”.
Lightness Godwin msimamizi wa miradi kutoka Shirika la GLAMI akihojiwa na Tanzania Kids Time ilipotaka kufahamu GLAMI inafanikishaje masuala ya stadi za maisha na maadili kwa wasichana wanufaika wake alisema,“Sisi kama GLAMI tumekuwa tukishirikiana na wazazi kwenye eneo la kuwasaidia wanafunzi hasa mabinti kupata stadi za Maisha na baada ya kikao chetu hiki cha leo kitatuwezesha kupata mikakati bora na yenye matokeo mazuri katika kuwashirikisha wazazi juu ya namna ya kufanikisha zoezi letu la kuwasaidia mabinti walioko katika programu zetu kuwa na stadi za Maisha na maadili”.
Akizungumzia manufaa ya kijana kuwa na maarifa ya stadi za maisha na maadili, Mhadhili kutoka Chuo kikuu cha Dar Es Salaam Daktari, Daniel Marandu ambaye ni Mratibu wa mafunzo ya ALiVE alisema, “Ukiangalia kwa sasa kuna wimbi la vijana wengi wanaomaliza vyuo vikuu lakini wanakutana na changamoto ya ukosefu wa Ajira, kwa hivyo moja ya faida ya stadi za maisha ni kwamba, kijana mwenye stadi ya Maisha ya utatuzi wa matatizo, hata kama akimaliza Chuo na akakosa Ajira, ile stadi inamsaidia yeye kufikiria nje ya Boksi”