Ongezeko la kasi ya matukio ya wanawake kuingia makubaliano ya
kubebeana mimba linatishia haki za mtoto, ameonya hii leo mtaalamu maalum wa
Umoja wa Mataifa kuhusu biashara na unyanyasaji wa watoto, Maud de Boer-Buquicchio.
Akiwasilisha ripoti yake mbele ya Baraza la haki za binadamu la Umoja wa
Mataifa huko Geneva, Uswisi hii leo, Bi. Boer-Buquicchio amesema tishio hilo
linazingatia ukweli kwamba kimataifa hakuna haki ya kuwa na mtoto na hivyo
mbebaji na mbebewaji wanaweza kuingia katika mvutano.
Amesema katika mazingira hayo watoto wanaozaliwa kupitia mfumo wa ubebeanaji
mimba haki zao zinakumbwa na kizungumkuti hasa kwenye nchi ambako ubebeanaji
mimba hufanyika kibiashara.
Mtaalamu huyo ameema iwapo mwanamke mbeba mimba analipwa ujira kwa kazi hiyo
au mtu aliyeratibu mpango huo, hiyo ni biashara ya mtoto kwa mujibu wa sheria
za haki za binadamu za kimataifa.
Kwa mantiki hiyo ametaka kuwekwa kwa mifumo ya kusimamia biashara hiyo ya
ubebeanaji mimba kwa kuwa wahusika wataendelea kuhama kutoka eneo moja hadi
jingi ili kukidhi matakwa yao huku haki za mtoto zikiendelea kusiginwa.