Mamilioni ya watoto wanaishi katika nchi ambazo takwimu kuhusu watoto hazipo
au ni shida kupatikana na hivyo kuweka mustakhbali wao mashakani, imesema
ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF.
Ikipatiwa jina la maendeleo ya watoto katika zama za malengo ya maendeleo
endelevu, SDGs, ripoti inaonyesha kwamba watoto milioni 650 wanaishi kwenye maeneo
ambayo theluthi mbili za malengo hayo itakuwa ndoto kutekelezwa bila hatua mpya
za kuchagiza.
Maeneo yaliyongaziwa ni afya, kujifunza, ulinzi dhidi ya ukatili na ghasia,
mazingira salama na fursa sawa.
Mkurugenzi wa takwimu UNICEF, Laurence Chandy amesema ni lazima dunia
itangaze upya azma yake ya kufanikisha SDGs kwa kutangaza upya ahadi ya vigezo
vya kupima.
Iwapo hili halitazingatiwa, kati ya sasa na mwaka 2030 watoto watakuwa
hatarini zaidi ambapo milioni 31 wanaweza kudumaa kutokana na ukosefu wa lishe
bora.
Bwana Chandy amesema ingawa serikali zina wajibu wa kuandaa takwimu na
vigezo vya kupima mafanikio ya SDGs, bado jamii ya kimataifa ina wajibu wa
kushirikiana nazo ili kuhakikisha vigezo vinafikiwa.