Katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya uelimishaji kuhusu usonji, ambayo
kila mwaka huwa Aprili pili, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio
Guterres amesisitiza kusimamia haki ya watu wenye usonji na kupazia sauti
ubaguzi dhidi yao.
Kupitia ujumbe wake mahsusi kwa siku hii siku Guterres amesema, kauli mbiu
mwaka huu inatanabaisha umuhimu wa kuwawezesha wanawake na wasichana wenye
usonji, kwani wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo vikwazo vya kupata
fursa ya elimu na ajira sawia na watu wengine, wananyimwa haki zao za afya ya
uzazi na haki ya kufanya maamuzi yao, lakini pia kutoshirikishwa katika
utungaji wa sera za masuala yanayowahusu.
Guterres ameongeza kuwa kazi ya kupigania usawa na uwezeshaji wa wanawake
lazima iwafikiwe wanawake na wasicha wote duniani ,na juhudi za kufikia malengo
ya maendeleo endelevu lazima zizingatie ahadi ya ajenda ya mwaka 2030 ya treni
hiyo kutomwacha yeyote nyuma.
Katibu Mkuu ametoa wito kwa kila mmoja katika siku hii kuongeza juhudi za
kuchagiza ushiriki kikamilifu wa watu wenye usonji na kuhakikisha wanapata
msaada wa lazima unaohitajika ili waweze kufurahia haki na uhuru wao wa msingi.Taarifa hii nikwa mjibu wa radio ya umoja wa mataifa.