Hiyo ni kauli ya Adama Dieng mjumbe
maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uzuiaji wa mauaji ya kimbari, kufuatia ziara
yake huko Bangladesh kunahohifadhiwa maelfu ya waislamu wa kabila la Rohingya
kutoka Myanmar,akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa kuhusu ziara hiyo na
mauaji ya warohingya huko kaskazini mwa Myanmar Bwana Dieng amesema…
“Natumaini kwamba kile
nilichokiona Cox Bazar na kile nilichoripoti kwa jumuiya ya kimataifa kwa
ujumla kitawafanya watu wawaamini warohingya. Kwa sababu nilishuhudia
janga la kibinadamu ambalo halijawahi kutokea. Ninachosema ni kwamba watu hawa
wa kabila ya Rohingya wanapitia mateso kwa muda mrefu zaidi ambapo
wamekuwa wakilazimika kukimbia mauaji katika vijiji vyao na kutembea safari
ndefu huku wakivuka mpaka kuelekea Bangladesh, ambako walipokelewa kwa ukarimu
.”
Bwana Dieng amesema vyombo vya Umoja wa Mataifa vyenye dhamana ya
kukabiliana na changamoto za kiusalama duniani kama Baraza la Usalama, Ofisi ya
haki za binadamu na mahakama ya kimataifa kuhusu mauaji ya kimbari
vinapaswa kuzingatia majukumu yao ili kuokoa janga la kibinadamu linalowakumba
warohingya huko Myanmar.
“Kutoridhika kwangu bila shaka, ni kuona kwamba Baraza la
Usalama, chombo ambacho kina jukumu la msingi la kuhakikisha amani na
usalama duniani, hakipo tayari kuzuia uhalifu unaoendela . Tumeona kile
kilichotokea Syria. Leo tuna karibu watu nusu milioni ambao wameuawa huko
Syria. Tuna karibu watu milioni 7 ambao wapo ukimbizini. Kwa nini tunaendelea
kuruhusu hii hali izidi kutokea? Kwa nini tunapaswa kuruhusu matumizi ya silaha
za kemikali? Nikiongeza pia mgogoro mwingine, kama ule wa Sudan Kusini.”