Pater Juma Maru na Cecilia Ofowa ni wanandoa kwa miaka 38, raia hawa
wa Sudan Kusini hivi sasa ni wakimbizi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
DRC, ingawa wanaonana , lakini hawawezi kuishi pamoja kama mke na mume
kulikoni?
Wanandoa hao Peter na Cecilia kama walivyo maelfu ya raia wengine wa Sudan
Kusini walilazimika kufungasha virago vita vya wenyewe kwa wenyewe
vilipochachamaa na kukimbilia DRC kusaka hifadhi.
Licha ya kuhepa kutenganishwa na kifo wakati wa vita nchini mwao, lakini sasa
wamelazimika kutengana na kuishi tofauti kwa mara ya kwanza kabisa, kisa? uhaba
wa malazi kwenye kambi za wakimbizi DRC.
“Mke wangu nakadiria
anaishi kilometa mbili kutoka mahali ninapoishi, inanichukua muda kwenda,
lakini namtembelea ingawa sio kila mara, namkumbuka sana, tumekuwa pamoja
karibu maisha yetu yote sasa, tunazeeka pamoja.”
Naye Bi Cecilia Ofowa akiwa kwenye kambi ya wakimbizi inayohifadhi wanawake
na watoto tu DRC, hakuficha hisia zake
“Inaumiza sana, sasa hivi sie ni wazee, nataka
aje hapa ili tuishi pamoja na wajukuu zetu na hata watoto wetu hadi pale Mungu
atakaponitenganisha naye.”
Peter amekuwa akiishi kwenye kibanda kidogo cha nyasi kwa miezi minane na
hali si shwari hata kidogo
“Upepo uvumapo unanifikia,
wakati mvua ikinyesha inaingia ndani, Ni hali mbaya, ni mazingira magumu.
Nahisi kwa kiasi kikubwa kutokuwa na matumaini kabisa”
Peter anatumia siku nyingi kujikumbusha ya kale akiwa na hamasa kubwa ya kutaka
kurejea nyumbani kwakwe na kwa mkewe, lakini kama walivyonena wahenga , ya kale
si dhahabu tena. Taarifa hii ni kwa mjibu wa UN Radio.