Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limepitisha azimio linalotoa
muongozo wa namna ya kulinda haki, usalama na ustawi wa watoto walioko
ndani ya mzunguko wa mizozo, pamoja na kuimarisha juhudi za kujenga
amani endelevu.
Akihutubia kikao hicho kabla ya kura iliyopitisha azimio hilo,
mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya
watoto kwenye vita vya silaha Virginia Gamba amesema azimio limekuja
wakati muafaka kutokana na ongezeko la visa vya utekwaji nyara,
uandikishwaji na utumikishwaji wa watoto wa kiume na wa Kike.
Ametolea mfano Somalia ambako watoto 1,600 walitekwa nyara baada ya jamii zao na shule kuvamiwa.
Aidha amesema ongezeko la ukatili kumesababisha kuongezeka kwa idadi
ya watoto wanaouawa ikiwemo huko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo, DRC, Iraq na Mynmar, huku kundi la Boko Haram likiendelea
kushambulia maeneo ya jamii na kijeshi kwa kutumia watoto kutekeleza
mashambulizi ya kujitoa mhanga huko Afrika Magharibi.
Halikadhalika ametoa mtazamo wake katika suala hilo na kusema..
Virginia Gamba
“Nimeshtushwa na idadi kubwa ya visa vya ukatili dhidi ya
watoto mwaka uliopita 2017 huku visa 21,000 vikiripotiwa na Umoja wa
Mataifa ikiashiria kuongezeka kwa idadi ikilinganishwa na mwaka jana. Bi
Gamba amesema ukatili huo umesababisha mateso kwa watoto, familia zao
na jamii kwa ujumla.”