Msumbiji mradi wa Umoja wa Mataifa umewezesha maafisa wa ugani
kufundisha wakulima namna ya kulima mazao na kuandaa lishe bora na hivyo
kuepusha utapiamlo ambao ni tatizo kubwa kwa watoto hususan kwenye
jimbo la Cabo Delgado.
Katika
moja ya viunga vya jimbo la Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji
wakulima wanawake kwa wanaume pamoja na vijana wakiwa shambani
wanapatiwa mafunzo kutoka kwa afisa ugani wa kilimo.
Mafunzo haya ni sehemu ya mradi wa mfuko wa kimataifa wa maendeleo ya
kilimo, IFAD wa kuhakikisha wakazi wa eneo hili wanalima mazao yao kwa
bora zaidi na hatimaye waweze kuboresha lishe kwa watoto wao.
IFAD inasema asilimia 43 ya watoto nchini Msumbiji wana utapiamlo na
katika jimbo hili la Cado Delgado hali ni mbaya zaidi kwa kuwa kiwango
cha utapiamlo miongoni mwa watoto ni asilimia 53.
Baada ya mafunzo wanayopatiwa shambani juu ya ukulima bora, wakulima
wakiwa kwenye vikundi wanafundishwa jinsi ya kuandaa chakula bora.
Lucia Lauteno ni mmoja wa wakulima takrbani 5,000 walionufaika na mafunzo hayo ambaye anasema. “nimejifunza
maana ya lishe, nimejifunza mambo mengi, mosi ni kuandaa uji ambapo
naongezea mayai na mafuta. Watu kwenye jamii yetu wamefurahishwa na kile
tunachofanya. Tunapofanya maonyesho yetu ya mapishi baada ya kujifunza
wanakuja kuonja na wanakipenda sana. Kabla ya huu mradi hatukufahamu
iwapo kuchanganya vyakula kunaweza kusababisha afya njema . Sasa tuko
vizuri na watoto wana nguvu na majirani wanatuuliza watoto tunawalisha
nini. “
IFAD inasema kuwa mkulima kama Lucia baada ya kupata utaalamu huo
naye anapatia watu wengine katika jamii yake ili kuhakikisha
wanaondokana na utapiamlo miongoni mwa watoto mkoani Cabo Delgado.
Taarifa hii nikwamjibu wa idhaa ya kiswahili radio ya umoja wa mataifa UN RDAIO.