dunia ikiadhimisha siku ya mtoto duniani, Millie Bobby Brown
ametangazwa kuwa balozi mwema mpya wa Shirika la kuhudumia watoto
UNICEF. Mtoto huyu wa umri wa miaka 14 anakuwa mtu mdogo zaidi kuwa na
wadhifa huo wa balozi mwema wa UNICEF.
uteuzi huo Millie amesema, “Kuwa balozi mwema wa UNICEF ni ndoto ambayo
imetimia, ni heshima kubwa kuungana na orodha ya watu ambao wameiunga
mkono UNICEF kwa miaka mingi. Ninatazamia kukutana na watoto wengi na
vijana wadogo nitakavyoweza, kusikiliza habari zao na kuongea kwa niaba
yao” .
Katika majukumu yake haya ya balozi mwema wa UNICEF, nyota huyu wa
mfululizo wa maigizo ya filamu ya Stranger Things atatumia nafasi yake
kusaidia kukuza ufahamu kuhusu haki za watoto na masuala yenye athari
kwa vijana kama ukosefu wa elimu, maeneo salama ya kucheza na kujifunza,
matokeo ya vurugu, kuonewa na umaskini. Millie amekuwa akiunga mkono
kazi za UNICEF tangu mwaka 2016. Anaungana na orodha ya mabalozi wema
wengine akiwemo: Muzoon Almellehan, David Beckham, Orlando Bloom, Jackie
Chan, Priyanka Chopra, Danny Glover, Ricky Martin, Lionel Messi, Liam
Neeson, Shakira na Lilly Singh.
Akizungungumzia uteuzi huo wa Millie, Mkurugenzi mkuu wa UNICEF
Henrietta Fore anasema, “Ninayo furaha kumkaribisha Milllie katika
familia ya UNICEF, hususani katika siku hii ya mtoto duniani-siku ambayo
inahusu kumpa mtoto na vijana wadogo sauti. Ninajua kuwa Millie
atatumia shauku na kujitolea kwake kulinda haki za watoto na vijana
walio katika mazingira hatarishi popote”.
Siku ya mtoto duniani huadhimishwa kila tarehe 20 ya mwezi novemba
ili kukuza uelewa na kusongesha haki za msingi za mtoto ambazo ni
kuishi, kuendelezwa, kushirikishwa na kulindwa. Miongoni mwa shughuli
zinazofanyika katika siki hii ni pmaoja na kuchangia fedha kwa ajili ya
watoto ambao hawapati fursa ya shule, hawalindwi na wasio na makazi.
Katika siku ya leo, UNICEF inawataka watu wote wanaoiunga mkono
kupaza sauti zao katika kuwaunga mkono watoto wenye uhitaji. Watu wote
wanapaswa kuibadili dunia na kuifanya ya buluu kwa kufanya au kuvaa kitu
cha rangi ya buluu iwe shuleni, mitaani, kwenye mitandao ya kijamii,
vyumba vya mikutano na katika viwanja vya michezo.
https://www.youtube.com/watch?v=xLBykXFjGR8
Siyo wanadamu tu, siku hii itaonekana hata katika majengo maarufu
ulimwenguni. Mathalani Sydney Opera nchini Australia, Kituo cha michezo
cha kitaifa mjini Beijing China, Petra Jordan, Mnara wa Galata na
madaraja kule Uturuki hata jengo la kihistoria katika jiji la New York
nchini Marekani yote yatakuwa katika rangi ya buluu.
Watoto ‘watatwaa madaraka ya juu ya uongozi’.
Mmoja wa watoto nchi Ireland kwa muda hii leo ‘atachukua madaraka ya
uwaziri mkuu’ wa nchi hiyo. Katika nchi nyingine kama kule Montenegro,
Peru, Tonga, Suriname na Zambia, watoto watachukua majukumu ya kibunge.
Tanzania Nigeria na kwingine watoto wamo katika vyombo vya habari
wakiripoti masuala yanayowagusa wakati kule Brussels vijana wakilitwaa
bunge la Ulaya na wakiwaeleza viongozi kuhusu Ulaya wanayoitaka, kule
Afrika magharibi na kati vijana watakuwa wakifanya hivyo pia kwa
viongozi wao. Leo ni siku kubwa kwa watoto kote duniani. Kwa maelezo zaidi tembelea news.un.org/sw