Tarehe 20 Novemba 2019
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inataarifu Umma kuwa leo tarehe 20 Novemba Tanzania inaungana na nchi nyingine Duniani kuadhimisha siku ya Kimataifa ya Haki za Mtoto pamoja na kusherehekea miaka 30 ya utekelezaji wa Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto. Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Mtoto ulipitishwa rasmi na nchi wanachama wa umoja huo mnamo tarehe 20 Novemba, 1989 sambamba na uanzishwaji wa Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto (Child Rights Convention) ambapo hadi sasa nchi 190 wanachama wa Umoja wa Mataifa zimetia saini na kuridhia mkataba huu.
Tanzania kama ilivyo Nchi nyingine Wanachama ilitia saini mkataba huu tarehe 1 Juni, 1990 na kuuridhia tarehe 10 Juni, 1991 ambapo siku hii imetengwa mahususi kuikumbusha Dunia kuwa, watoto wana haki ambazo hazistahili kupuuzwa. Hata hivyo kuna idadi kubwa ya watoto Duniani wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo ukiukwaji mkubwa wa haki za Mtoto na ukatili wa aina mbalimbali kama vipigo, kubakwa, mimba na ndoa za utotoni, ukeketaji, ulawiti, vitisho, umasikini unaowanyima mahitaji ya msingi, utumikishwaji, kuhusishwa na vita vinavyopelekea ulemavu na hata kupoteza maisha. Hivyo, lengo la kuadhimisha siku hii ni kuelimishana na kuikumbusha jamii nzima ya watanzania hasa wazazi na walezi wajibu wao katika kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi.
Maadhimisho ya mwaka huu 2019 Wizara kwa kushirikiana na wadau imeandaa kongamano la wadau ambalo limejielekeza zaidi katika kutafakari upatikanaji wa haki za Mtoto, ambazo zimeainishwa vizuri na Sera yetu ya Mtoto ya 2008; haki hizo ni Haki ya Kuishi, Haki ya kuendelezwa, Haki ya kulindwa, Haki ya kushiriki na kushirikishwa na Haki ya kutobaguliwa. Serikali ya Tanzania imetekeleza kwa vitendo katika kusimamia Haki zote tano za msingi ambapo katika kusimama haki ya Mtoto ya kuishi, Serikali imeboresha huduma za afya ya mama na mtoto katika hospitali, vituo vya afya na zahanati zetu nchini. Kwa mfano; Serikali imefanikiwa kupunguza vifo vya watoto wachanga chini ya mwaka mmoja kutoka vifo 99 mwaka 2011 hadi vifo 43 mwaka 2016 kwa watoto 1,000 na katika kipindi kama hicho, vifo vya watoto chini ya miaka 5 vimepungua kutoka vifo 147 hadi vifo 67. Mafanikio haya yanatokana na maboresho yaliyofanyika katika utekelezaji wa Sera ya Afya ya mwaka 2000.
Aidha, kuhusu haki ya kuendelezwa kielimu, Serikali imehakikisha watoto wote nchini wanapata elimu bila malipo kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha nne. Hatua hii imeongeza idadi kubwa ya watoto wanaojiunga na shule. Mwaka 2017, idadi ya watoto walioandikishwa kwenye shule za awali imeongezeka hadi kufikia watoto 1,517,670 ukilinganisha na watoto 1,069,823 walioandikishwa mwaka 2015. Kadhalika, idadi ya watoto walioandikishwa kwenye shule za msingi kwa mwaka 2017 imeongezeka kufikia watoto 2,078,379 ukilinganisha na watoto 1,568,378 walioandikishwa mwaka 2015.
Katika kuimarisha usimamizi na utoaji wa haki na ulinzi wa Mtoto, Serikali imezindua Mpango kazi wa Taifa wa miaka 5 (2017/18-2021/2022) wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na Watoto ambapo kupitia Mpango huo Kamati za Ulinzi wa wanawake na watoto ambao ndio wasimamizi wakuu wa usalama wa Wanawake na Watoto zimeanzishwa katika ngazi mbalimbali. Kamati hizi zinajukumu la kuratibu vitendo vya ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto kuanzia ngazi ya Taifa, Mikoa hadi Mamlaka za Serikali za Mitaa. Serikali imeanzisha Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto katika mikoa 26 na Halmashauri 89 kwa lengo la kudhibiti ukatili dhidi ya wanawake na Watoto; bado tunahitaji kufikia Halmashauri zote 185 na kujenga uwezo wa Kamati hizi ili kuweza kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Katika haki inayosisitiza ushiriki na kushirikishwa kwa Mtoto; Serikali kwa kushirikiana na wadau imeendelea kuhimiza Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuongeza bajeti ya kuwezesha mabaraza ya watoto. Mabaraza haya hutoa fursa kwa watoto kujadili masuala mbalimbali yanayohusu haki na ustawi wao na pia kuishauri Serikali kuhusu masuala hayo. Mpaka kufikia mwezi Machi, 2019 mabaraza ya watoto 19 katika ngazi ya mikoa, mabaraza 121 katika ngazi ya Halmashauri za Manispaa/Wilaya/Miji, mabaraza 733 katika ngazi ya Kata na mabaraza 795 katika ngazi ya kijiji/Mtaa yalianzishwa. Mabaraza haya yameleta mchango mkubwa katika kuwajengea watoto uwezo wa kujieleza na kujiamini ambayo ni nyenzo muhimu katika kujilinda na vitendo vya ukatili.
Serikali kupitia Jeshi la Polisi imeanzisha dawati la Jinsia na Watoto katika vituo 420 nchini kwa lengo la kuwezesha matukio ya ukatili wa kijinsia na watoto hufikishwa vituo vya polisi na hatua za kisheria huchukuliwa dhidi ya wakosaji.
Aidha, Serikali kwa kushirikiana na shirika la C-SEMA tumeanzisha huduma ya bure ya kutoa taarifa za ukatili dhidi ya mtoto kupitia huduma ya simu ya bure kwa Watoto yenye Na. 116. Taarifa hizo hupokelewa na kufanyiwa kazi bila kumuathiri mtoa taarifa. Napenda kuwajulisha wananchi wote hususan wanawake na watoto kwamba tuzitumie huduma hizo zilizoanzishwa kwa ajili yenu ili kutoa taarifa za aina yoyote ya ukatili. Huduma hizi zimesaidia sana upatikanaji wa haki kwa wahanga wa ukatili.
Wito wa Serikali katika kipindi hiki cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Haki za Mtoto na miaka 30 ya utekekelezaji wa Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto ni kuhakikisha kuwa wazazi, walezi, jamii na wadau mbalimbali tunazingatia wajibu wa utoaji wa huduma za ustawi na Haki za Msingi za Mtoto katika ngazi ya familia, taasisi, na jamii kwa ujumla ili kuwa na Taifa lenye nguvukazi imara.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto