Wananchi katika kitongoji cha LUGANJO MTONI kata ya USENYE wilaya ya KALIUA mkoani TABORA wameiomba serikali kuisajili shule waliyojenga kwa nguvu zao ili watoto waweze kusoma karibu.
Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara baadhi ya wananchi wamesema kutokana na watoto wao kutembea umbali mrefu kwenda shule ya msingi SHELLA waliamua kujitoa kwa hali na mali ili kukamilisha miundombinu ya shule kwenye kitongoji hicho.
Akizungumza na wananchi kwenye mkutano huo wa hadhara Mkuu wa wilaya ya KALIUA, ABELI BUSALAMA amesema atafatilia ili shule hiyo ipate usajili na watoto waanze kusoma karibu kuondokana na adha ya kutembea ubmbali mrefu.
Kwa mujibu wa afisa mtendaji wa kijiji cha SHELLA, LEMUNJE YAIRO amesema tayari kuna vyumba sita vya madarasa, ofisi mbili za waalimu na matundu manne ya vyoo huku matundu mengine manne yakiwa katika hatua za ujenzi.
Amesema katika ujenzi huo halmashauri imechangia mabati, huku mfuko wa jimbo ukiunga mkono kwa kutoa milioni tano na michango kutoka kwa wananchi.
Na Simon Jumanne Wilaya Ya Kaliua Tabora.