Mkazi wa Mtaa wa Kikuyu, barabara ya Kinywambwe, Kata ya Hazina, mkoani Dodoma, Amos Manyika, ambeye ni mlemavu wa ukoma na uoni hafifu, ameomba msaada wa malezi kwa mtoto wake ambaye anadaiwa kufanyiwa vitendo vya ukatili na mke wake, Jenipher John.
Amesema amelazimika kutengana na mke wake akidai amekuwa akiendekeza tabia ya ulevi na kutokuwa muaminifu kwenye ndoa yao.
Akizungumza na Tkt Radio kwa mahojiano maalum Mkoani humo Ndg. Amos amesema mke wake amekuwa akimpiga mtoto wake mwenye umri wa miaka mitano (jina linahifadhiwa) kwa kumpiga na kumgongesha ukutani mara kwa mara.
“Nimekuwa nikiishi katika mazingira magumu ya ulemavu kwa kuomba msaada kwa wapita njia hali ambayo imesababisha kushindwa kufuatilia alipo mtoto wangu. Kilio changu kwa serikali ni mwanangu asaidiwe kupata haki zake za msingi, yakiwemo Malezi,Huduma za Afya,Chakula na Elimu muda utakapo fika wa kuandikishwa shuleni” ameeleza.
Hata hivyo Ameongeza kuwa maranyingi amekuwa akizungumza na mke wake kubadili mwenendo mbaya bila mafanikio, hadi kufikia uamzi wa kumuacha,“Sitaki kuoa tena kwanza nimeshajichokea na moyo umekufa, bora nihangaike na maisha yangu, Nawaasa wanawake wengine waachache hizo tabia wawe waaminifu kwenye ndoa zao na kulea watoto,” amebainisha.
Kadhalika, aliiomba serikali na wasamaria wema, kumsaidia baiskeli ya kutembelea na mtaji wa biashara ili aweze kufanya shughuli ya kumpatia kipato kumudu maisha yake.
“Maisha ya kuomba sipendezwi nayo natamani nipate msaada kutoka kwa jamii maana kwa sasa sina msaada nategemea kuomba, chochote nachopata nakula na sina mtu wa kunihudumia,” amesema.
Kwa upande wake, msamaria mwema Eliya Lungwa, amesema ametoa msaada kwa kupiga simu kwa kamanda wa polisi wilaya ya Dodoma Mjini, baada ya kushuhudia mama wa mtoto huyo akimpiga mwanae kwa kugongesha ukutani.
“Usiku wa Desemba 11 mwaka 2019 wakati nikirudi nyumbani, nilishuhudia mwanamke huyo anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 40 akiwa anampiga mtoto wake mwenye umri wa miaka mitano kwa kumgongesha ukutani kwa madai ya ugumu wa maisha.
“Alimsababishia maumivu makali ndipo nilipochukua hatua ya kutoa taarifa kituo cha polisi pamoja na diwani kwa hatua zaidi za kisheria,” amesimulia.
Aliongeza kuwa kipigo hicho kilipelekea mtoto huyo kulazwa katika Hosptali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, kwa siku tatu.
Amewataka wazazi kuwatunza watoto wao katika mazingira yoyote badala ya kuwafanyia ukatili ambao huwenda ukawasababishia kilema cha maisha huku akiisisitiza jamii kutofumbia macho wanaofanya vitendo hivyo.
Diwani Kata ya Hazina, Samweli Mziba, amekemea vitendo vya baadhi ya wazazi kuendekekeza ulevi tabia ambayo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa migogoro ya kifamilia.
Mziba amekiri kuwepo kwa wazazi ambao wamekuwa hawatimizi majuku yao akibainisha kuwa wamekuwa wakitoa ushauri na kuwachukulia hatua za kisheria.
Ameongeza kuwa ofisi yake imekuwa ikishirikiana na ofisi ya Maendeleo ya Jamii kuhakikisha hali ya ustawi wa jamii hasa kwa watoto ina kuwa vizuri kwa kutembelea maeneo ya shule na kusikiliza kero za watoto kisha kuzitatua.
Naye, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Theresia Mdendemi, anayesimamia Dawati la Jinsia na Watoto Dodoma, aliihimiza jamii kuendelea kushirikiana na polisi kwa kutoa taarifa za uwepo matukio ya ukatili kwa watoto, wanawake, walemavu na makundi mengine.
Nakuongeza kuwa dawati la jinsia kwa kushirikiana na viongozi wa serikali za mitaa wamekuwa wakitoa elimu kwa jamii katika maeneo mbalimbali ikiwemo shuleni, kupitia mikutano ya kata na vyombo vya habari.
“Niwatoe hofu watu wote wenye taarifa za ukatili kuwa ni wajibu wa jeshi la polisi kumhifadhi mtoa taarifa hivyo kwa aliye na taarifa hizo anaweza kuwasiliana na dawati la jinsia,” amesema.
Kwa upande wake Sarah Eliyo, mkazi wa Ipagala amebainisha kuhusu vitendo vya ukatili kwa watoto vimekuwa vikifanywa na watu wa ndani ya familia,Na,Nassoro Kikwembe, mkazi wa Njedengwa, Kata ya Makulu aliwahimiza wazazi kutoshirikisha watoto katika ugomvi wao jambo ambalo hupelekea watoto kukimbia familia zao hatimaye kuishia mitaani na kujiingiza kwenye makundi ya uhalifu.
Na Devotha Songorwa – Dodoma.