Mkuu wa Mkoa wa Morogoro LOATA OLE SANARE amewapongeza askari waliomuokoa mtoto na baba yake kwenye maporomoko ya maji maeneo ya Nguzo camp Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza katika tukio la kuwapongeza na kuwapatia zawadi askari hao, lililofanyika Januari 06, 2020 katika kiwanja cha FFU, SANARE alisema kuwa, vijana wamefanya kazi nzuri ya uokoaji, na wamejenga heshima kubwa katika Jeshi Polisi nchini.
“niwapongeze vijana wangu wale, na kuwatia moyo.. mlijitolea kwa nguvu zenu zote na kuhakikisha mnamuokoa yule mtu aliyedhamilia kufanya nia mbaya yake binafsi pamoja na mtoto” alisema Sanare.
Aidha aliwashukuru wananchi wa mkoa huo kwa kutoa taarifa hiyo, ambayo ilipelekea askari kuwahi katika tukio ili kutoa msaada wa uokoaji kwa raia, huku akiwasisitiza kuendelea kutoa taarifa pindi wanapoona viashiria vyovyote vile ambavyo wataona si vya kawaida katika maeneo yao.
Askari waliopatiwa zawadi ni PF.19925 A/INSP Sylivester Nganga, G.6409 D/C Josephat Tindwa, G.8808 D/C Mapalala Magembe, H.5798 D/CEdwin Clement, J.1517 D/C na Onesmo Kahemela.
Desemba 19, 2019 katika maporomoko ya maji ya Nguzo Camp, zilianza kusambaa video kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii, zikimuonesha mtu mmoja akiwa na mtoto mwenye umri wa miaka saba katika maporomoko hayo huku akiwa ameshika panga, msumeno na kuongea lugha isiyoeleweka.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro WILLBROAD MUTAFUGWA iliyotolewa Desemba 23, 2019 alisema askari walikwenda kwa haraka, katika eneo hilo baada ya kupata taarifa, pasipo maandalizi yoyote.
“…katika uokoaji huo simu, saa za askari hao ziliharibika na nyingine kwenda na maji kutokana na kwamba hawakuwa na maandalizi lakini walifanikiwa kuwaokoa baba na mtoto wake wote wakiwa salama”. Alisema Kamanda Mutafungwa.
Pia Kamanda MUTAFUNGWA alisema wanamshikilia baba huyo aliyefahamika kwa jina la BENSON BENARD (31) Mkazi wa Kihonda Manispaa ya Morogoro ili kumpeleka katika uchunguzi wa Afya ya Akili katika hospitali ya Rufaa ya Morogoro.
Hata hivyo kufuatia tukio hilo, Desemba 24, 2019 Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, WILLBROAD MUTAFUNGWA aliandaa gwaride rasmi na zawadi ili kuwapongeza askari hao kwa kazi ya kujitoa mhanga katika uokoaji wa watu hao.
Na; Shua Ndereka Morogoro.