Kufikia mwaka 2023, programu ya pamoja ya UNFPA na UNICEF
kutokomeza ndoa za utotoni itawakuwa imewafikia zaidi ya mabinti
milioni 14 katika nchi 12 barani Afrika, Mashariki ya kati na Asia
Kusini. Programu hiyo ambayo kwa mara ya kwanza ilizinduliwa mnamo mwaka
2016, pia inahusisha familia, waelimishaji, watoa huduma, serikali,
viongozi wa dini na kimila kama sehemu ya juhudi za ulimwengu kutokomeza
ndoa za utotoni ifikapo mwaka 2030.
Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore amesema, “tangu
kuzinduliwa, mpango wa dunia umeokoa mamilioni ya wasichana dhidi ya
ndoa zisizohitajika. Pia tunatakiwa tusisahau wasichana milioni 12 ambao
bado wanaolewa kila mwaka na kusababisha madhara ambayo hayawezi
kurekebishika kwa mstakabali wa maisha yao, afya na ustawi wao. Miaka
minne ijayo ya mpango huu inatoa fursa mpya kuendeleza kasi yetu
tulipofikia na kutokomeza milele matendo haya ya kusikitisha.”
Awamu ya pili ya programu iliyozinduliwa katika msingi na mazingira
ya kampeni ya Kizazi cha Usawa na pia wakati wa kuadhimisha miaka 25 ya
Mkataba wa Beijing na Jukwaa la Hatua itaendelea kuangazia mikakati
inayotambulika, ikiwemo kuongeza nafasi ya wasichana kupata elimu na
huduma za kiafya, kuendeleza ujuzi, kuwaelimisha wazazi na jamii kuhusu
hatari za ndoa za utotoni na pia kukuzausawa wa kijinsia, kujenga
ushirikiano kwa kutoa msaada wa kiuchumi kwa familia na kuimarisha na
kutekeleza sheria ambazo zinaeleza kuwa miaka 18 ndio umri wa chini wa
ndoa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA Natalia Kanem amesema, “ikiwa
mabinti watakuwa wanaendelea kuolewa wakiwa bado wadogo, hatuwezi
kufikia usawa wa kijinsia ambao vijana wadogo wanauhitaji. Wasichana
wanatakiwa kuwa na nguvu ya kufanya machaguo yao wenyewe, yaani ni
wakati gani nan ani wa kuoana naye, kuhusu kuendelea na elimu, na kuhusu
iwapo wapate watoto na lini.Mpango huu umepanga kuwawezesha wasichana
kutekeleza haki zao, kutimiza uwezo wao na kuleta mabadiliko katika
jamii zao.”
Tangu programu hiyo ilipozinduliwa mwaka 2019, zaidi ya wasichana
wadogo 7.7 na wana jamii milioni 4.2 wamefikiwa na taarifa, ujuzi na
huduma. Programu hii pia imezisaidia serikali kuendeleza na kutekeleza
mikakati ya kitaifa ya kutokomeza ndoa za utotoni.
Duniani kote, inakadiriwa kuwa wasichana na wanawake milioni 650
walioko hai hii leo, waliolewa wakiwa watoto, ambapo takribani nusu yao
wanaishi katika nchi ambazo hivi sasa zinasaidiwa na mpango huo wa Umoja
wa Mataifa kutokomeza ndoa za utotoni.
Kwamaelezo zaidi tembelea news.un.org/sw