Wanandoa Mkoani Njombe wametakiwa kuimarisha ndoa zao kwa kuepuka tabia ya kutengana na kupeana taraka pindi wanapokuwa na migogoro ili kupunguza tatizo la ongezeko la watoto wa mitaani na wanaoishi katika mazingira magumu.
Kauli hiyo imetolewa na waumini wa kanisa la Tanzania Assembles of God TAG Wa mtaa wa Melinze wakati wakizungumza na Tanzania Kids Time/ UN Radio kuhusiana na athali za kutengana kwa wanandoa katika jamii.
Aidha Waumini Hao akiwemo Yosia Chongolo na Mwandila Msigwa wamesema serikali inatakiwa kuweka mikakati ya kupunguza uwepo wa watoto wa mitaani na watoto walioko kwenye mazingira magumu ambao wamesababishwa na wazazi wao kutengana.
Aidha wameeleza kuwa, watoto wengi wanashindwa kupewa malezi yenye maadili mema na kuishia kutangatanga mitaani baada ya kulelewa na mzazi Mmoja ambaye anashindwa kutimiza mahitaji muhimu kwa watoto.
Mchungaji wa kanisa la Tanzania Assembles Of God (TAG) Cefania Teve amesema, wamelazimika kufunga Siku sita na kufanya maombi ili kutokomeza Ugonjwa wa CORONA Duniani pamoja na kuziombea ndoa mbalimbali zisivunjike ili watoto waweze kupatiwa haki zao za msingi.
Kwa Upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Njombe Bi. Luth Msafiri ambaye alihusika katika hitimisho la kongamano la maombi kanisani hapo amesema, serikali imetambua kuwa kuwepo kwa watoto wa mitaani kunachangiwa na kuvunjika kwa ndoa na kutaka wanandoa Waliotengana kupatana ili kulea watoto wao.
Hata hivyo Afisa ustawi wa halmashauri ya mji wa Njombe Bi. Veronica Muyango amesema, licha ya kuwepo kwa watoto wa mitaani bado kuna ukatili dhidi ya watoto hao wa kulawitiwa na kulawitiana wao kwa wao na kutaka wazazi kukemea vikali tabia hiyo.
NJOMBE Na-Michael Ngilangwa