Zaidi ya shilingi laki saba ambazo Ni michango ya wananchi wa Mjimwema Mkoani Njombe, zimekabidhiwa kwa Maria Mtitu mama mwenye watoto wawili wenye Ulemavu wa akili.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo Mratibu wa kampeni ya TUNAISHI NAO inayoendeshwa na kituo cha radio mkoani humo Fikirini Ngairo, amewapongeza wananchi kwa kushiriki kikamilifu kuchangia fedha hizo zitakazo msaidia Bi. Maria kuhudumia na kununulia mahitaji ya watoto hao.
“Wananchi wa Mtaa wa Mjimwema wamechangia shilingi laki tatu na elfu 21 na mia mbili na kufanya jumla ya shilingi laki saba na elfu ishilini na moja na mia mbili ambazo zimekabidhiwa kwa mama huyo mwenye watoto wenye ulemavu wa mtindio wa ubongo” amesema.
Baadhi ya viongozi wa serikali wa mtaa wa Mjimwema akiwemo Afisa Mtendaji Elia Chilatu amesema watawaunganisha watoto hao na Afisa elimu kata ya Mjimwema ili kuwapeleka kwenye shule zinazolea watoto wenye mahitaji maalumu ili wasomeshwe.
“Afisa Elimu wa kata ameniambia nipeleke majina lakini wao watawatafutia shule hawa watoto watakapofanikisha utaratibu wao” amesema.
Pia Mama wa watoto hao wawili ambao wanaumri wa miaka 7 na 10 Maria Mtitu, ameshukuru kwa msaada huo uliotolewa na wananchi na kwamba itamsaidia kutatua changamoto zilizokuwa zikimkabili.
Na; Marco Kilangwa- Njombe