Kituo cha wasaidizi wa Kisheria Mkoa wa Morogoro (MPLC) wameadhimisha siku ya mtoto wa Afrika kwa kukitembelea kituo cha kulea watoto Yatima Mgolole mkoani humo kwa lengo la kuunga mkono na kuwapa faraja watoto hao kwa kuwapatia msaada wa vitu mbalimbali vikiwepo unga, sukari na sabuni.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo Afisa Mawasiliano na Mahusiano wa Kituo cha wasaidizi wa kisheria Manispaa ya Morogoro Peter Kimath amesema kuwa kulingana na siku hiyo iliyopitishwa na umoja wa Mataifa ili kuwakumbuka watoto waliouwawa wakipigania haki zao za msingi mwaka 1976 huko nchini Afrika Kusini.
“tunatambua mchango unafanywa na walezi wa kituo hiki lakini tunatakiwa kuwaweka karibu watoto hata wale waliopo mtaani, kwani wazazi tunamtihani mkubwa wa kuhakikisha watoto wanaishi katika mazingira salama, wanapata haki zao za msingi na kuwajengea uwezo wa kujijitea ili waweze kupinga ukatili wa kijinsia” amesema Peter Kimath.
Mkuu wa Kituo cha Kulea watoto yatima cha Mgolole Sister Evarista Bunga kilichopo Bigwa, Manispaa ya Morogoro amekishukuru Kituo hicho cha wasaidizi wa Kisheria (MPLC) kwa kuwapatia msaada huo huku akibainisha kuwepo kwa changamoto kwa baadhi ya bidhaa zinavyohitajika kupanda bei hasa Maziwa ya unga kipindi hiki cha COVID 19 ambayo huhitajika zaidi kwa watoto waliochini ya mwaka mmoja.
“tunawashukuru wadau ambao wanaendelea kutusaidia , msichoke tunawakaribisha wengine kituo kwa sasa kinawatoto 48 tunaendelea kuwalea katika maadili na utendaji wa kazi ili kusudi waweze kuendelea na kujua katika hatua za kibinadamu yapo mambo ya kimwili na kiroho” amebainisha Sister Evarista Bunga.
Bi. Isabela Katungutu ni miongoni mwa Wasaidizi wa kisheria Mkoani Morogoro walioguswa kuwatembelea watoto hao, ambapo amewataka wazazi na walezi kuendelea kutembelea kituo cha watoto yatima Mgolole ili kuwafariji watoto hao ambao walitakiwa kupata malezi ya wazazi wao kama wengine, kutokana na matatizo mbalimbali na wengine kupoteza wazazi imepelekea watoto hao kulelewa kwa pamoja katika kituo hicho.
Juni 16 kila Mwaka Tanzania na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika wanaadhimisha siku ya mtoto wa Afrika ambapo ilitokana na mauaji ya watoto wapatao 2,000 yaliyofanywa na Utawala wa makaburu wakati wa maandamano ya kudai haki ya kupata Elimu bila kubaguliwa katika kitongoji cha Soweto nchini Afrika Kusini Juni 16, 1976.
NA, SHUA NDEREKA
Morogoro