Maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji kitaifa yamefanyika katika Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, ambapo Mh.Ummy ametoa wito kwa jamii kuwa saidia majukumu wakina Mama iliwanyonyeshe kwa wakati unao takiwa watoto na kupunguza utapiamlo.
Aidha kwa upande wa takwimu za hali ya ulishaji watoto nchini Tanzania zinaonesha kuwa takribani asilimia 97 ya watoto wenye umri chini ya miaka miwili wananyonyeshwa maziwa ya mama.
“Idadi ya watoto wanaoanzishiwa kunyonyeshwa maziwa ya mama kwa wakati sahihi katika kipindi kisichozidi saa moja baada ya kuzaliwa ni asilimia 53 na idadi ya watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya mama pekee bila kupewa maji, vinywaji na vyakula vingine katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo baada ya kuzaliwa ni asilimia 58,”
amesema Waziri Ummy.
Hata hivyo idadi ya watoto wanaoanzishiwa vyakula vya nyongeza kwa wakati sahihi katika umri wa miezi 6 hadi 8 ni asilimia 87 na idadi ya watoto wenye umri wa miezi 6 – 23 wanaolishwa chakula kinachokidhi vigezo vya ubora kilishe ni asilimia 35.
“Vigezo hivyo ni idadi sahihi ya milo anayopewa mtoto kwa siku kulingana na umri wake, na mlo uwe na mchanganyiko wa vyakula kutoka kwenye makundi yasiyopungua manne ya vyakula,” amesisitiza.
Mh.Ummy amesema Maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji Duniani kwa mwaka 2020 yamebebwa na kauli mbiu inayosema “Tuwawezeshe wanawake kunyonyesha watoto kwa afya bora na ulinzi wa mazingira”.
Kwa upande wa kauli mbiu amefafanua na kusema,inalenga kutukumbusha mchango wa unyonyeshaji katika utunzaji wa mazingira ya dunia na ikolojia yake sanjari na kulinda afya ya binamu,Inahimiza jamii kuboresha kasi ya unyonyeshaji sanjari na kupunguza kiwango cha matumizi ya maziwa na vyakula mbadala vya watoto wachanga na wadogo.
“Hata hivyo tukumbuke kuwa matumizi ya maziwa na vyakula mbadala vya watoto wachanga na wadogo yanakwenda sanjari na matumizi ya vifungashio mbalimbali vikiwemo vya plastiki, nishati ikiwemo kuni na mkaa, maji, chupa za kulishia watoto na ongezeko la hewa ya ukaa inayoathiri mazingira ya dunia,” amesema Waziri Ummy.