ULISHAJI usio sahihi unaochangiwa na mama kuelemewa na majukumu mengi ya kazi na hivyo kukosa muda wa kutosha wa kumtunza mtoto ni sababu kubwa ya utapiamlo kwa watoto
Hayo yamesema leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji ambayo kitaifa yamefanyika wilaya ya Muheza mkoa wa Tanga.
“Ni dhahiri kuwa mchango wa mwanamke katika familia, ajira na uzalishaji kwa ujumla ni mkubwa hivyo ni muhimu kuwatia moyo na kuwasaidia wanawake ili waweze kufanya majukumu ya uzalishaji na utunzaji familia kwa ukamilifu”.
Waziri Ummy amesema kuwa jamii ina wajibu wa kuwawezesha wazazi, hususani wanawake waweze kunyonyesha watoto wao maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo baada ya kujifungua.
Aidha, amesema watoto wanapotimiza miezi sita waanzishiwe vyakula vya nyongeza vyenye ubora kilishe huku wakiendelea kunyonyeshwa hadi watakapotimiza umri wa miaka miwili.