Lishe ya wanawake wakati wa ujauzito na kunyonyesha ni muhimu kwa afya ya mama na mtoto aliye tumboni na hata afya ya mtoto mchanga baada ya kuzaliwa.
Wanawake wanashauriwa kula chakula mchanganyiko na cha kutosha kutoka katika makundi yote ya chakula wakati wa ujauzito na kunyonyesha ili kupunguza athari za kuzaa mtoto mwenye uzito pungufu na matatizo mengine.
Na wanawake wanaonyonyesha ni muhimu waongeze ulaji wa vyakula vyenye nishati lishe na utomwili kwa wingi zaidi kuliko kiwango kinachoshauriwa kwa wajawazito.
Hayo yameainishwa na bi, Salome Magembe afisa lishe mkoa wa Morogoro katika semina ilio wakutanisha waandishi wa habari mkoni humo kuhusu kuandika na kuripoti habari zitakazo elimisha jamii kuhusu umuhimu wa unyonyeshaji mtoto maziwa ya mama na lishe kwa mama mjamzito na baada ya kujifungua.
kwa nini kuongeza nishati lishe wakati wa ujauzito?
Aidha mahitaji ya nishati lishe na virutubishi vingine wakati wa ujauzito huongezeka kwa ajili ya kukidhi ongezeko la mahitaji ya mwili wa mama kama vile kuongezeka uzito, kuupa nguvu mwili wakati wa ujauzito na kuweka hifadhi ya nishati lishe ya kutosha itakayotumika wakati wa kunyonyesha.
Ukuaji wa mtoto aliye tumboni, kondo la nyuma la uzazi na tishu za mfuko wa uzazi, mabadiliko ya utendaji kazi wa moyo na mfumo wa hewa kwa mama
Kuweka uwiano sahihi wa uzito wa mama na kuupa nguvu mwili wakati wote wa ujauzito
MAHITAJI YA NISHATI LISHE KWA WAJAWAZITO.
Hata hivyo bi, Magembe akazungumzia mahitaji ya nishati lishe na virutubishi vingine mama mwenye ujauzito.
Wanahitaji kula chakula kingi katika kila mlo au kula milo midogo midogo mara kwa mara;
Kula asusa kati ya mlo na mlo;
Kula matunda na mboga mboga kwa wingi katika kila mlo;
Kunywa maji ya kutosha kila siku (glasi 8 au lita 1.5); na
Kuepuka kunywa chai au kahawa pamoja na mlo kwani huzuia ufyonzwaji wa madini ya chuma na huweza kusababisha upungufu wa damu. Ni vyema kunywa chai au kahawa saa moja kabla au baada ya kula.
Katika hatua nyingine bi,Magembe akazungumzia faida na athari za ongezeko la uzito wakati wa ujauzito.
Kuongezeka uzito wakati wa ujauzito ni muhimu sana kwani ni kiashiria cha lishe nzuri. Mama anatakiwa kuongezeka wastani wa kilo 12 kwa kipindi chote cha ujauzito.
Sehemu ya akiba ya mafuta yatatumika kwa ajili ya unyonyeshaji katika miezi michache ya mwanzo
Ni muhimu kuzingatia kwamba wanawake walio na uzito uliozidi au viribatumbo kabla ya kupata ujauzito hawatakiwi kuongezeka uzito kiwango sawa na wanawake waliokuwa na uzito wa kawaida kabla ya kupata ujauzito.
Athari za uzito uliozidi wakati wa ujauzito
Endapo mama atakuwa na uzito uliozidi au kiribatumbo kabla ya ujauzito, au ameongezeka uzito zaidi ya kiwango kinachoshauriwa wakati wa ujauzito anaweza kupata madhara kama vile:
Kisukari cha ujauzito (kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu wakati wa ujauzito)
Viashiria vya kifafa cha mimba, hali inayoambatana na shinikizo la juu la damu na kupoteza protini kwenye mkojo.
Matatizo wakati wa kujifungua mfano mtoto kushindwa kutoka kwa njia ya kawaida.
Matumizi ya vitamini na madini ya nyongeza
Shirika la Afya Duniani linapendekeza matumizi ya vitamini na madini ya nyongeza hasa madini chuma na asidi ya foliki ili kuzuia upungufu wa wekundu wa damu kwa wanawake wajawazito na wanao nyonyesha, kuzuia kujifungua watoto wenye uzito pungufu, njiti pamoja na kujifungua watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi.
Nyongeza ya vitamini na madini kwa mjamzito