Katika mwendelezo wa habari zetu tulizo kwisha zichapisha kupitia tovuti hii kuhusu masuala ya afya ya mama na mtoto hususani Unyonyeshaji maziwa ya mama na lishe kwa mtoto, leo tumekuletea dondoo nyingine kuhusu lishe bora kwa siku 1000 tangu kuzaliwa kwa mtoto,ambapo Afisa Lishe Manispaa ya Morogoro bi,Ester Kawishe anatanabaisha hatua zote muhimu ambazo mzazi/mlezi anapaswa kuzifuata katika kumuhudumia mtoto.
Mtoto anayekuwa na lishe duni katika umri huo ana uwezekano mkubwa wa kudumaa kimwili na kiakili, kuugua mara kwa mara, na hata kufa.
Madhara ya kilishe yanayojitokeza yasiporekebishwa katika kipindi hiki cha siku 1,000 za mwanzo za maisha ya mtoto huleta athari zisizoweza kurekebishwa tena katika ukuaji na maendeleo yake.
Wizara ya Afya imeainisha vipindi vitatu muhimu vya ulishaji katika maisha ya mtoto. Vipindi hivyo ni:
Miezi 0 – 6
Miezi 6 – 24
Miezi 24 – 59
Aidha bi, Kawishe akazungumzia Ulishaji wa watoto wadogo na wachanga kwa saa ya kwanza hadi miezi 24.
Saa ya kwanza.
Mtoto anyonyeshwe maziwa ya mama ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa.
Miezi 6: Mtoto anyonyeshwe maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo.
Miezi 6-24
Mtoto aanzishiwe vyakula vya nyongeza atakapotimiza umri wa miezi sita na aendelea kunyonyeshwa maziwa ya mama mpaka atakapofikisha miaka miwili au zaidi.
Maana ya maneno yanayotumika katika ulishaji wa watoto wachanga na wadogo.
Unyonyeshaji maziwa ya mama pekee
Tendo la kumpa mtoto maziwa ya mama kwa njia ya kunyonya kutoka kwenye titi, au kupewa maziwa ya mama yaliyokamuliwa kwa kutumia kikombe, bila kumpa vinywaji au vyakula vingine ikiwemo maji, isipokuwa dawa na chanjo kwa ushauri wa mtaalamu wa afya.
Ulishaji watoto vyakula vya nyongeza
Mchakato wa kuanza kumpa mtoto vyakula vya nyongeza atakapofikisha umri wa miezi 6 kwa kuwa maziwa ya mama pekee hayatoshelezi mahitaji yake ya kilishe. Mtoto apewe vinywaji na vyakula vingine huku akiendelea kunyonyeshwa.
Hata hivyo bi, Kawishe aka fafanua Taratibu za Unyonyeshaji.
Maziwa ya mama ni chakula cha kipekee – hakiwezi kuigwa.
Kina uwiano sahihi wa virutubishi, kimetengenezwa kwa usahihi kutumiwa na mtoto wa binadamu na hubadilika kulingana na mabadiliko ya mahitaji ya mtoto kulingana na umri.
Ingawa kunyonyesha ni tendo la kiasili, mama anahitaji kujifunza mbinu na kanuni za kunyonyesha vizuri.
Mwili wa mama ugusane na mwili wa mtoto ngozi kwa ngozi mara tu baada ya kujifungua.
Mtoto anyonyeshwe ndani ya saa moja baada ya kujifungua.
Kunyonyesha maziwa ya mama pekee kuanzia mtoto anapozaliwa hadi anapotimiza umri wa miezi 6.
Kunyonyesha mtoto mara kwa mara wakati wote usiku na mchana
Kuyonyesha mtoto kila wakati kadiri anavyohitaji.
Mtoto anyonye na kumaliza maziwa yote kwenye titi moja na aachie mwenyewe kabla ya kumhamishia kwenye titi lingine.
Mpakate na kumweka mtoto vizuri kwenye titi.
Faida za Unyonyeshaji.
Kupungua kwa uwezekano wa kupata tatizo la manjano
Kuboresha ukuaji na hali ya lishe ya mtoto
Kupungua kwa vifo vrisha kingamwili ya mtoto
kupungua kwa maambukizi
Kupungua kwa magonjwa ya ngozi
kupungua kwa magonjwa ya mfumo wa njia ya chakula
Kupungua kwa magonjwa ya kuharisha
Kupungua kwa magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa
Kuboresha mahusiano baina ya mama na mtoto
Kupungua kwa uwezekano wa magonjwa sugu (kisukari, magonjwa ya moyo, pumu na baadhi ya saratani)
Kupunguza uwezekano wa kuwa na uzito uliozidi au kiribatumbo
Kuboresha ukuaji wa kiakili na misuli.
Faida kwa mama
Kupunguza upotevu wa damu baada ya kujifungua
Kupunguza sononi (depression) baada ya kujifungua
Kupunguza uwezekano wa kupata ujauzito mapema katika miezi sita ya mwanzo endapo mama atanyonyesha maziwa ya mama pekee
Kupunguza uwezekano wa kupata baadhi ya saratani kama:
Saratani ya via vya uzazi mfano Shingo ya uzazi
Saratani ya matiti
Mama kurudia hali yake ya kawaida mapema kimaumbile na kupunguza uzito uliotokana na ujauzito.
MADHARA YA ULISHAJI MBADALA KWA WATOTO.
Athari kwa mtoto ni:
Ukuaji duni na utapiamlo
Kuongezeka kwa vifo
Kuongezeka kwa magonjwa mbalimbali:
Maambukizi kwenye masikio
Magonjwa ya ngozi
Magonjwa ya mfumo wa njia ya chakula
Kuhara
magonjwa ya njia ya mfumo wa hewa
Kuathiri mahusiano ya mama na mtoto
Uwezekano mkubwa wa magonjwa sugu (kisukari, magonjwa ya moyo na baadhi ya saratani)
Kuongezeka kwa uwezekano wa kuwa na uzito uliozidi na kiribatumbo
Kupata alama za chini (IQ) kwenye mitihani ya majaribio ya ufahamu kiakili.
Athari za kutonyonyesha mtoto.
Athari kwa mama
Sonona au msongo wa mawazo baada ya kujifungua
Uwezekano wa kupata ujauzito mwingine mapema
kuongezeka kwa uwezekano wa kupata baadhi ya saratani kama:
Saratani ya via vya uzazi
Saratani ya matiti
Kuchelewa kupunguza uzito uliotokana na ujauzito na hivyo kushindwa kurudia hali yake ya kawaida mapema baada ya kujifungua.
Kukabiliana na Imani Potofu na Changamoto za Unyonyeshaji.
Baadhi ya imani potofu na changamoto za unyonyeshaji ni pamoja na:
Maziwa ya mama hayatoshi katika siku tatu za mwanzo baada ya kujifungua, na hata kidogo yanayotoka hayafai kumpa mtoto, inafaa kumpa mtoto asali, maji yenye sukari, au maziwa mbadala katika kipindi hiki.”
ii. “Wingi wa maziwa ya mama unategemea chakula na tabia za ulaji za mama, pia vyakula vingi huathiri afya ya mtoto. Kama mama anakula vyakula vya moto mtoto atapata tatizo la kuhara na kama mama atakula vyakula vya baridi, mtoto atapata tatizo la kukohoa.”
iii. “Wakati anaponyonyeshwa, mtoto anahitaji maji ya nyongeza hususani hali ya hewa inapokuwa ya joto.”
iv. “Kama mama ana matiti madogo, atatengeneza kiasi kidogo cha maziwa.”
v. “Kama mama amejifungua kwa njia ya upasuaji hatakiwi kumnyonyesha mtoto.”
vi. “Mtoto anayeharisha asinyonyeshwe maziwa ya mama.”
“Mtoto mwenye umri wa miezi 3 anaweza kuachishwa kunyonya na kuanzishiwa vyakula mbadala ili mama yake arudi kazini.”
ULISHAJI WATOTO VYAKULA VYA NYONGEZA.
Katika hatua nyingine afisa lishe akasema nibora kufuata taratibu zinazo shauriwa na wataalamu wa afya na Shirika la Afya Duniani linavyopendekeza:
“kuwaanzishia watoto vyakula vya nyongeza katika umri muafaka wa miezi 6 huku akiendelea kunyonyeshwa maziwa ya mama mpaka atakapofikisha umri wa miaka miwili au zaidi.”
Inapendekezwa kumwanzishia mtoto vyakula vya nyongeza anapotimiza umri wa miezi 6 kwa sababu :
Mahitaji yake ya nishati lishe na virutubishi yameongezeka na maziwa ya mama pekee hayawezi kutosheleza mahitaji hayo.
Kuanzisha ulishaji wa vyakula vya nyongeza kabla ya umri wa miezi 6 kunaweza kusababisha kuongezeka kwa uwezekano wa mtoto kupata maambukizi hususani kuhara.
Kiumri wanakuwa tayari na uwezo wa kula vyakula vingine.
Itaendelea ……….