Lishe inavyotibu utapiamlo kwa watoto
Ni saa kumi kasoro dakika kadhaa hivi, jua linaanza kuelekea magharibi. Nipo katika Kijiji cha Kiswanya baada ya kusafiri takriban kwa saa 6 kufika kijijini hapa.
Ni safari ya ubali wa kilometa 185 kusini mashariki mwa mji wa Morogoro. Kwa kawaida safari hii hutumia si zaidi ya saa nne, lakini kutokana na matemgenezo ya barabara kunzia eneo la Mikumi kuelekea Ifakara, nalazimika kurumia saa 2 zaidi.
Nafika nyumbani kwa mkazi wa Kijiji hiki, Neema Mustafa ambaye ambaye kwa zaidi ya miaka 20 amekuwa akiishi na ulemavu uliotokana na kupooza.
Lengo siyo kumwona Neema, bali kupata taarifa za mtoto Omary mwenye umri wa miaka miwili, akilelewa na mama huyu mwenye ulemavu.
Nilifika nyumbani kwa Neema katika Kijiji cha Kiswanya kilichopo Kata ya Mang’ula, wilayani Kilombero katika mkoa wa Morogoro, nikiwa nimeambatana na Mariam Mwita.
Huyu ni mtaalamu wa lishe wa Shirika la Save the Children akifanya kazi katika Wilaya ya Kilombero. Tulikutana eneo la Mang’ula kadri tulivyokuwa tumeahidiana, yeye akitokea mjini Ifakara nami nikitokea Morogoro mjini.
Wakati tukiwasili tulikutana na macho ya majirani kadhaa ambayo yaliashiria shaka au shauku ya kilichotufikisha nyumbani kwa Neema. Nje ya nyumba alikuwapo mtoto akicheza na dada.
Baadaye nilibaini kuwa yule mtoto ndiye Omary mwenyewe, na yule binti ni msaidizi wa Neema au dada wa Omary kwa maana ya malezi ya kila siku. Nilikaribishwa pamoja na Mariam ambaye kwake haikuwa mara ya kwanza kufika mahali hapa.
Binti yule aliingia katika moja ya vyumba viwili vilivyoko katika eneo hii na kutoka na stuli mbili ambazo tulizitumia kuketi. Kisha binti yule aliingia katika chumba kingine, na baada ya muda tulikarbishwa ndani.
Tulinyanyua stuli zetu na kuingia nazo ndani. Tulimkuta mwanamama akiwa amelala kitandani. Huyu ni Neema Mustafa (41) aliyepooza kwa miaka 20 sasa. Huyu ndiye wa Omary kwa sasa.Abtoria ya aina yake. Alizaliwa July,2018 katika kijiji cha Msolwa wilayani Kilombero Mkoa wa Morogoro.
Kwa mujibu wa mlezi wake, Neema Mustafa, makuzi ya Omary yalianza kukumbwa na changamoto mara tu baada ya kuzaliwa kwake.
Neema anasema mama yake na Omary alipatwa na ugonjwa wa kupooza mwili, hivyo ilihindwa kabisa kumnyonyesha.
Tangu mama yake alipopooza, Omary hakuwahi kupata malezi ya mama, badala yake alikabidhiwa kwa mama yake mkubwa kwa ajili ya uangalizi na malezi.
Hata hivyo alipofikisha umri wa miezi minne, Omary alikabidhiwa kwa baba yake aitwaye Abubakar, hivyo kuondoka mikononi mwa mama yake mkubwa.
Habari zinasema, mama mkubwa aliamua kumkabidhi Omary kwa baba yake baada ya kutokea kutokuelewana baina ya wawili hao (mama mkubwa na baba wa mtoto).
Kwakuwa Omary alikuwa bado mdogo, baba yake (Abubakar) baada ya kumchukua kutoka kwa mama yake mkubwa, alilazimika kutafuta mlezi mwingine ili amsaidie kumlelea kufanya kazi hiyo kwa malipo ya fedha.
Neema anasema huo ulikuwa mwanzo wa Omary kudhoofika kiafya kutokana na lishe duni. Kadri siku zilivyokwenda mtoto alianza kuwa na uzito pungufu.
Anasema inaaaminika kuwa hali hiyo ilitokana na mlezi wake mpya kutozingatia vyakula wanavyopaswa kumlisha kulingana na umri wake. Hatimaye Omary alipata utapiamlo uliosababisha kudumaa katika ukuaji wake.
Takwimu katika ofisi ya lishe ya Mkoa wa Morogoro inayoongozwa na Salome Maghembe zinaonyesha kuwa udumavu mkoani humo ni asilimia 26.4, ukondefu asilimia 3.7 na watoto wenye uzito pungufu ni asilimia 12.1.
TKT/UNRadio ilimtafuta Abubakar ambaye ni baba mzazi wa mtoto Omary ili kuzungumzia maisha na hali ya afya ya mwanaye, lakini hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa undani
Licha ya ulemavu alionao, Neema baada ya kusikia taarifa kuhusu mtoto Omary, aliamua kuchukua jukumu la kumlea ili kurejesha afya yake kutoka katika utapiamlo uliompata kwa sababau ya changamoto za maisha ya wazazi wake.
“Siku moja Abubakar (baba yake Omary) alipigiwa simu kutoka kituo cha afya wakitaka kufahamu maendeleo ya mtoto. Wakati huo Omary alikua na mwaka mmoja na uzito wake ukiwa kilo sita(6) tu. Hiyo ndiyo siku niliyoamua kumchukua kukaa naye nyumbani kwangu.
“Baada ya kumchukua Omary nikawa natafuta ushauri kutoka kwa watu mbali mbali kuhusu afya yake. Wakati nasikiliza redio siku moja, nikasikia mtaalamu wa lishe anayeitwa Mariam Mwita anafundisha umuhimu wa lishe kwa watoto wadogo.
“Alivyotaja namba za simu, nikazichukua na baada ya kipindi nikampigia nikamueleza kuhusu mtoto Omary, akanielekeza aina ya vyakula ninavyopaswa kumuanzishia,”anasema Neema.
Anaongeza kuwa baada ya miezi mitatu, Mariam alikwenda nyumbani hapo kumuona mtoto nah apo akabaini kuwa ni mfanyakazi katika shirika la Save the Children. Shirika hilo linatekeleza mradi wa Lishe Endelevu.
“Tunavyo zungumza leo mtoto amepona na kwa sasa ana umri wa miaka miwili na miezi minne,” anasimulia Neema.
Naye Mariam ambaye ni msimamizi wa mradi wa Lishe Endelevu mkoa wa Morogoro anasema lengo la mradi wake ni kupunguza udumavu, ukondefu na uzito pungufu kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.
“…hivyo Omary yupo kwenye kundi la watoto wa umri huo, tulimuelekeza mlezi wake aina ya vyakula kulingana na umri na hali yake ilipokuwa amefikia kwenye hatua nyekundu kwenye kadi yake ya kliniki. Mradi huo unaotekelezwa nashirika la Save the Children kwa ufadhili wa USAID.
Mariam anasema Omary ambaye sasa ana miaka miwili na miezi minne, amepona na kwa kushirikiana na Emilia Raphael ambaye ni Afisa Ustawi wa Jamii wa Ifakara wamemtafutia kituo cha kulelea watoto kiitwacho Ebeneza. Amekabidhiwa kituoni hapo Septemba 18, 2020.
Walichukua hatua hiyo kutoka na ukweli kwamba wazazi wake bado hawana msimamo wa makazi yanayoweza kuendelea kusimamia afya ya yake, hususan Mama yake ambaye mpaka sasa anaendelea na matibabu akihudumiwa na dada yake.
Kadhalika hali ya kiafya ya mlezi wake (Neema) ambaye amepooza siyo ya uhakika, kwani wakati mwingine hubadilika.
Afisa Lishe katika Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, Bodygad Buhari akizungumza kwa simu kuhusu mtoto Omary alisema: “Ni kweli taalifa ya mtoto Omary aliyekuwa na udumavu, ninaifahamu japo sikuwahi kufika nyumbani kwa mlezi wake ili kujua maendeleo yake”.
Mwisho….
Na. Mwandishi John Kabambala Morogoro.