Chumba cha Darasa la Kidato cha kwanza B” Sumaye Sekondari Manispaa ya Morogoro.
Wanafunzi wa Shule za Sekondari Mkoa wa Morogoro nchini
Tanzania wameeleza kunufaika na Mkopo wa riba nafuu Trilioni 1.3 ambao Tanzania
iliupata mwaka 2021 kutoka Shirika la Fedha Dunia – IMF kwa kuelekeza sehemu ya Fedha katika uboreshaji wa mpango
wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Uviko 19, ikijenga
vyumba vya madarasa 12,000 vilivyogharimu shilingi Bilioni 240 kwa lengo la
kupunguza msongamano shuleni sambamba na kujikinga na ugonjwa wa Uviko 19.
Katika kuonesha Taswira halisi Mwandishi wa Habari Hamad
Rashid, amefanya ziara ya kutembelea Mradi uliokamilika wa vyumba vya madarasa
ya Uviko 19 katika Shule za Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Manispaa
ambayo imejenga jumla ya vyumba vya madarasa 86 na kuandaa Makala ifuatayo.
Ziara yangu imeanzia Shule ya Sekondari Sumaye iliyopo
Kata ya Bigwa nakutana na Wille Victor Mwanafunzi wa kidato cha kwanza, alisema
anafurahi kusomea katika madarasa ya Uviko19 na manufaa anayoyapata ni makubwa.
“haya madarasa ya Uviko19
yameninufaisha cha kwanza katika upande wa Viti na madirisha, mwanzo ilikua
wanafunzi wanakaa zaidi ya 50 ndani ya Darasa moja lakini saivi tunakaa ka
nafasi na madirisha yanapitia hewa safi, hata kusoma Mwanafunzi inakua rahisi
kumuelewa Mwalimu” alisema Wille Victor.
Ofisini kwa Makamu mkuu wa Shule ya Sekondari Sumaye,
Mwalimu Msokelo Baruti nilifika na alieleza namna walivyonufaika na Mradi huu
wa madarasa ya Uviko 19.
Baruti alisema “hapa
shuleni tumenufaika kwa kujengewa Vyumba viwili vya madarasa, viti na meza zake
Mia moja Mwaka jana tulitoa wanafunzi wa Kidato cha Nne 164, Mwaka huu
tumepokea zaidi ya wanafunzi 200 unaweza kuna jinsi tulivyokuwa na uhitaji”
Ziara yangu ikahamia Shule ya Sekondari Lupanga Kata
ya Kilakala ndani ya Darasa la kidato cha kwanza baada ya kukaribishwa na Wimbo
wa Shule nilimhoji mwanafunzi mnufaika wa Kidato cha kwanza, Grace Marema ambapo
pamoja na mambo mengine alisema, madarasa ya Uviko yamepunguza utoro Shuleni.
“Kwenye adha ya utoro
imesaidia wanafunzi wengi kutotoroka kwa sababu mnapokua mmeachiana nafasi ni
rahisi Mwalimu kujia namba ya wanafunzi nani yupo na nani hayo kwa hivyo inakua
ni ngumu mwanafunzi kutoroka, kuliko mwanzo ambapo kulikua na msongamano wa
wanafunzi darasani” alisema Grace
Neema ya kujengewa madarasa ya Uviko 19 imekuja wakati
sahihi Mkuu wa Shule ya Sekondari Lupanga Mwalimu Flora Ndunguru alisema.
“Kiukweli tumepokea kwa
furaha kubwa Lupanga Sekondari tumejengewa madarasa Sita na kila darasa lina
viti na meza 50 jumla ya katika maradasa yote ni viti na meza zake 300, hii ni
kutokana na wingi wa wanafunzi tulionao, tulikua tumepangiwa wanafunzi
wanatakiwa kuripoti Kidato cha Kwanza Mwaka 2022, 277 na walioripoti ni
wanafunzi 230” alisema Mwalimu Flora.
Baada ya Flora Ndunguru ikafika wakati wa viongozi wa
Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Gabriel Paul ni Afisa Elimu Sekondari.
“Katika Halmashauri ya
Manispaa ya Morogoro tulipokea jumla ya Fedha 1, 720,000,000, tumejenga jumla
ya vyumba vya madarasa 86 katika Shule 21 zilizonufaika ambapo ndani yake
tumejenga Shule mpya Nne za Sekondari ambazo ni Mazimbu, Mkundi, Tungi na Shule
ya Sekondari Mbuyuni Modern” alisema Gabriel Paul.
Ujenzi wa madarasa ya Uviko 19 umezingatia viwango
vyote vya Serikali, alisema kaimu Mhandisi wa Majengo Halmashauri ya Manispaa
Morogoro, Injinia Juma Gwisu.
Gwisu alisema “tulikua na
Fomu maalumu ya kuhakikisha kwamba kila hatua ya ujenzi tunakagua na kabla ya
kuanza ujenzi fundi anajaza na msimamizi anajaza, hivyo hivyo na katika vifaa
tulikua hatuwezi kupeleza Tofali eneo la Ujenzi (site) tukishajirishisha ndio
tunaruhusu ujenzi kuendelea, hii imeleta manufaa mazuri hadi kufakisha vyumba
vyote vya madarasa kujengwa kwa kiwango bora”
Ally Machela ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa
ya Morogoro ameeleza jinsi madarasa ya Uviko19 yalivyoleta chachu katika Elimu.
Machela alisema “Kwanza
tumeweza kuwapeleka Shule wanafunzi wa Kidato cha kwanza kwa wakati kama agizo
la Serikali lilivyoelekeza, na tumefikia zaidi ya Asilimia 90 ya wanafunzi wote
wa kidato cha kwanza wamesharipoti Shule”
Machela pia alizungumzia afua za kujikinga na Homa ya
mapafu Uviko 19 kwa wanafunzi kwa kusema Jamii sasa imebadilika, watu wengi
wanafuata maelekezo ya Serikali ya namna ya kujikinga na Uviko19 na Shuleni
kuna miundombinu mizuri inayomuwezesha mwanafunzi kujikingakama kuwepo kwa
visima vya Maji vilivyochimbwa na wadau mbalimbali wa Elimu.
Na Hamad Rashid – Morogoro.