wanaotoa uangalizi kwa kundi la wasichana na wavulana balehe wenye ulemavu
wamebainisha kwamba kundi hili muhimu katika jamii limekuwa likisahaulika
linapokuja suala la kuwafikia vijana balehe ili kuwapatia elimu ya afya ya
uzazi.
Kwa
mujibu wa wataalamu wa afya ya jamii, afya ya uzazi kwa vijana wa rika la
balehe ni muhimu mno kwani ni katika kipindi hiki ndipo vijana hukabiliwa na
changamoto mbalimbali, ikiwemo mimba za utotoni, magonjwa, na utoaji mimba usio
salama, ambapo bila elimu muhimu kutolewa zinaweza kuhatarisha maisha na ustawi
wa mhusika.
Linda Ngido ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mehayo Centre for Disabled
Young People, kituo kinachojihusisha na kuwapatia ujuzi na fursa vijana wenye
ulemavu ambaye ameiambia Tanzania
Kids Time kwenye mahojiano maalum kwamba hajawahi kuona wataalamu wa
afya ya uzazi kutoka serikalini au kwenye asasi za kiraia kufika kituoni hapo
kwa ajili ya kutoa elimu ya afya ya uzazi.
“Kuna
wakati ambao wasichana wanafikia umri wa kupata hedhi, ukimuelekeza binti mwenye
ulemavu kuhusu kutumia vifaa vya kujistiri hawataki,” anaeleza Ngido ambaye ni
mwalimu kitaaluma. “Wakati mwingine wanavitupa.”
Ngido
haelewi ni kwa nini wadau hawajikiti kwenye kuwapatia vijana wa rika la balehe
wenye ulemavu elimu ya afya ya uzazi wakati watu hawa pia ni binadamu kama
walivyo watu wengine ambao hukua na kuanzisha familia zao.
“Watoto
wenye ulemavu nilioanza kuwa nao kwenye kituo hiki, wavulana na wasichana, sasa
hivi ni watu wazima, wameoana wenyewe na wana watoto wanasoma,” anaeleza Ngido
ambaye alilazimika kuacha kazi yake ya ualimu kufanya kazi yake ya sasa. “Kwa
hiyo, siyo kwamba hawa watu wenye hali hii hawawezi kuwa na familia. Hapana,
wanaweza.”
Tanzania
Kids Time ilitembelea kituo cha Erick Memorial Foundation for
Education and Rehabilitation for the Disabled (EMFERD) kilichopo mkoani hapa
kinachojihusisha na kutoa huduma kwa watu wenye ulemavu.
Vijana wengi walio katika rika la balehe ambao ni walemavu
waliopo kituoni hapa walikiri kwa Tanzania
Kids Time kwamba hawajawahi kufikiwa na kupatiwa elimu ya afya ya
uzazi, hali ambayo wanasema inawasononesha.
“Hii huduma tunaihitaji kwa sababu watu wenye ulemavu nao wana
haki zote za msingi [kama vile ya] kuoa au kuolewa,” Benedict Mwenyasi, kijana
mwenye ulemavu wa viungo kutoka EMFERD, aliiambia Tanzania Kids Time, “[Wadau] sisi wanatusahau
[kutupatia elimu hii].”
Wadau
wanakubaliana kwamba ipo haja ya Serikali na wadau wengine wa afya ya uzazi
nchini Tanzania kuweka mikakati na kuchukua juhudi za pamoja za kuhakikisha
kwamba kundi hili nalo linafikiwa kwenye utoaji wa elimu ya uzazi nchini.
Moja
kati ya wadau hawa ni Obed Mtagulwa, mwanzilishi mwenza na Mkurugenzi Mtendaji
wa Care Youth Foundation, shirika linalojihusisha na kutoa elimu ya uzazi kwa
vijana rika balehe.
“Hizo
sehemu wanazokaa watu wenye mahitaji maalum huwa tunaenda kwa ajili ya kutoa
huduma ya misaada pekee yake, bado hatujafika kupeleka elimu ya uzazi,” anakiri
Mtagulwa. “Kuna haja kubwa sana ya kuwapa elimu [watu hawa].”
Naye
daktari bingwa wa afya ya uzazi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Morogoro Dk
Deodata Ruganuza ameonya kwamba endapo wadau hawataweka kipaumbele kwenye
kuwapatia watu wenye ulemavu elimu ya afya ya uzazi haki za msingi za watu hao
zitakuwa zipo hatarini kukiukwa.
“Tusipoweka kipaumbele katika hili kundi, [vijana walemavu walio
katika rika balehe] watakuwa wanakosa kitu cha muhimu sana kwao na kwa familia
zao watakazoanzisha,” Dk Ruganuza aliiambia Tanzania Kids Time kwenye mahojiano maalum
yaliyofanyika ofisini kwake.
Na, John
Kabambala.