Katika juhudi za kuendelea kuunga Mkono lengo la namba Nne la umoja wa mataifa la kuboresha Elimu bora, nchini Tanzania baadhi ya vijana wameeleza kukosa maarifa ya Stadi za maisha ambayo wangeweza kufundishwa katika mtaala wa Elimu iwasaidie kujitambua na kupanua fikra zao, maarifa na kuwa wabunifu hata baada ya kuhitimu masomo.
Chini ya shirika la Milele Zanzibar Foundation na Uwezo Tanzania, tathmini ya upimaji stadi za maisha kwa vijana wa umri wa miaka 13 hadi 17 inaendelea kufanyika Tanzania Bara katika awamu ya pili huku ambapo upande wa Jiji la Dar es salaam vijana wameendelea kufanyiwa tathmini katika Halmashauri za Wilaya ya Ilala na Kinondoni.
Kwa mujibu Ripoti ya mustakabali wa kazi iliyotolewa na Foramu ya kiuchumi ya Dunia Oktoba 2020 inaonesha ukosefu wa stadi za maisha unazidi kuwa mkubwa katika Ajira, na hadi kufikia Mwaka 2025 45% ya waajiri watahitaji waajiriwa wenye maadili ya stadi za maisha badala ya kuwajengea uwezo na mafunzi wakishaajiriwa hii ni kutokana na mfumo wa Elimu jinsi unavyowaandaa wahitimu kuwa tegemezi.
Elizabeth Lazaro ni msichana anayesoma kidato cha Nne Shule ya Sekondari BUYUNI Kata ya PUGU katika Jiji la ILALA, baada ya kufanyiwa utafiti akiulizwa maswali alisema ni dhahili kuna umuhimu wa Serikali kuongeza Somo la Stadi za Maisha katika mtaala wa Elimu ili kukisaidia kizazi chao kuwa na maarifa zaidi ya Elimu ya kawaida yatakayo wasaidia kujitegemea na kuwa msaada kwa Jamii.
“Katika maswali haya niliyoulizwa nimejifunza mengi, nimejifunza jinsi ya kumtetea mtu, nashukuru kwa uelewa huu unatusaidia, kwa sababu katika Jamii vijana wanachukuliwa kama ni watu wasio faa, kama wanatabia mbaya, ikiingia mashuleni itasaidia sana kwa sisi vijana kujitambua’’ alisema Elizabeth
Athumani Kihagila kutoka Kata ya PUGU Jiji la ILALA ni mmoja wa watafiti wanaododosa vijana, alisema uzoefu alioupata kote alikopita kuhoji, vijana wengi walikosa maarifa ya ziada katika kujibu maswali huku akigusia suala la wanafunzi kushindwa kutumia vifaa vya kidigitali katika ujifunzaji.
Athumani alisema ‘’kwa tathmini niliyoifanya kwa vijana, kwanza wengi kusoma kwa kutumia vifaa vya kidijitali wengi uwezo wao uko chini wachache sana wanaweza, kama Serikali ingeweza kuweka somo la stadi za maisha kama yalivyo masomo mengine Shuleni, ingesaidia sana kwani ni jambo ambalo linahitajika sana’’
Mratibu wa mradi wa ALiVE Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, TUNU SANGA alisema watatumia matokeo ya tathmini ya stadi za maisha kwa vijana kushirikiana na Serikali kuboresha mitaala ili kuwasaidia vijana kulitumikia vyema Taifa lao.
‘’Zoezi hili litatuwezesha kuweza kushirikiana na Serikali kuja na mbinu mbadala za kuweza kuboresha namna gani vijana wa kitanzania wanaweza kupata Elimu ya stadi za maisha ili tuondokane na dhana za kusema vijana hawajitambui’’ alisema Tunu sana
Ripoti ya hali ya maadili ya stadi za maisha kwa vijana Tanzania na Afrika mashariki inatarajiwa kutoka Mwezi wa Tisa 2022, ambayo inalenga kuleta ushawishi wa mabadiliko ya Sera na mitaala ya Elimu kujumuisha Somo la stadi za maisha shuleni.
Na. Hamad Rashid.