“Takriban watoto na vijana 110,000 wa umri wa miaka 0-19 walikufa kutokana na sababu zinazohusiana na Ukimwi mwaka 2021” Kwa mujibu wa taarifa ya UNICEF inayotoa taswira mpya ya kimataifa kuhusu watoto, VVU na Ukimwi. Wakati huo huo, shirika hilo limesema wengine 310,000 walipata maambukizi mapya na kufanya jumla ya vijana wanaoishi na VVU kufikia milioni 2.7 ulimwenguni kote”.
TATIZO LA VVU KUTOKA KWA MAMA KWENDA KWA MTOTO
Kwa mujibu wa taarifa za shirika la umoja wa mataifa linalohusika na kupambana na kuratibu shughuli za kudhibiti VVU (UNAIDS), limeonyesha kwamba mpaka mwisho wa mwaka 2020, asilimia 84% ya watu wanaoishi na VVU walikuwa wanajua hali zao za maambukizi, kati yao 96% walikuwa wameanzishiwa na wanatumia dawa, na kati ya hao wanaotumia dawa 95% virusi vilikuwa vimefubazwa.
Pamoja na hatua hii kubwa, kundi la Watoto liko nyuma kufikia haya malengo ikiwa ni asilimia 62% ya Watoto wanaoishi na VVU wamejulikana, 96% wameanzishiwa dawa na 87% virusi vimefubazwa. Hii inaonesha kwamba kunahitajika juhudi za kitofauti kuharakisha upatikanaji wa dawa, Watoto wengine ambao bado hawajajulikana na kuwaanzishia matibabu na huduma ili waweze kukua kulingana na umri wao.
CHANZO CHA TATIZO HILI
Dr. Theopista Jacob yeye ni makamu wa Rais wa chama cha madaktari bigwa wa watoto Tanzania (PAT), amesema haya nilipo hojiana nae, “Mwaka 2021, zaidi ya maambukizo mapya 75,000 elfu ya watoto yalitokea kwa sababu wajawazito hawakugunduliwa mapema kuwa wameambukizwa na kuanza matibabu kwa wakati. Mtoto anapozaliwa na VVU kinga yake ya mwili inadhoofu angali tayari kinga yake haiko imara kulingana na umri wake na kupelekea kupata magonjwa nyemelezi mapema Zaidi ukilinganisha na mtu mzima.
Kama mama mjamzito akigundulika mapema kuwa anaishi na VVU na akaanza kuzingatia matibabu kama alivyoelekezwa na wataalamu wa afya, virusi kwenye mwili wa mama vitafubaa na kupunguza uwezekano wa kumwambukiza mtoto wakati wa ujauzito, kujifungua na hata wakati wa kunyonyesha”.
MADHARA YAKE NI YAPI?
Dr. Theopista anasema madhara ya mtoto kuambukizwa VVU na kutoanzishiwa matibabu mapema, kwa kawaida mtoto anapozaliwa huwa na kinga kidogo dhidi ya magonjwa mbalimbali ndio maana wanapatiwa chanjo ili kuimarisha kinga ya mwili kadiri wanavyokuwa.
Mtoto akipata magonjwa nyemelezi yanaathiri afya yake kwa ujumla kwakuwa VVU vinashambulia sehemu zote za mwili, Mfano mtoto anaweza kupata utapiamlo na kudumaa mwili na hata kuathiri ukuaji na maendeleo yake ya awali, mfano kushindwa kukaza shingo, kutambaa, kutembea, kuongea n ahata uelewa wake wa mambo. Ukimlinganisha na mtoto mwingine wa umri wake asiyekuwa na VVU anaonekana ni mdogo kwa umbo lake lakini anakuwa na sura ya kikubwa.
Taarifa mpya ya UNICEF inaonesha maambukizi mapya ya VVU miongoni mwa watoto wadogo wa umri wa miaka 0-14 yalipungua duniani kote kwa asilimia 52 kati ya mwaka 2010 hadi 2021, na maambukizi mapya kati ya vijana barubaru wa umri wa miaka 15-19 pia yalipungua kwa asilimia 40.
Dr. Theopista Jacob ! Mama asipotumia dawa kwa wakati madhara yapi yatajitokeza kwa mtoto aliopo tumboni? Kama mama hatatumia dawa ya kufubaza VVU kwa wakati uwezekano wa kumwambukiza mtoto wakati wa ujauzito ni asilimia 5 hadi 10, wakati wa kujifungua ni asilimia 10-15 na wakati wa kunyonyesha ni asilimia 5 hadi 20. Lakini kama mama atatumia dawa basi hatari ya kuambukiza mtoto inashuka hadi chini ya asilimia 2.
Watoto wa umri wa chini ya miaka mitano wamekuwa kwenye hatari kubwa Zaidi ya kufa kwa kuwa hawagunduliki mapema ama kugundulika wakiwa wameshaugua sana na wazazi kutokuchukua hatua mapema kuwaleta kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
HALI YA MATIBABU IKOJE?
Pengo lilikuwa kubwa zaidi kati ya watoto na wajawazito wanaoishi na VVU ambalo ni asilimia 81%. Inashangaza kwamba, asilimia ya watoto wenye umri wa kati ya miaka 0-4 wanaoishi na VVU na wasiotumia dawa imekuwa ikiongezeka katika kipindi cha miaka saba iliyopita, na kupanda hadi asilimia 72 mwaka 2021, kama ilivyokuwa mwaka 2012, Shirika la UNICEF limesema.
Dr. Theopista Jacob anasema dawa zinapatikana bure kwenye vituo vya kutolea huduma na kila mjamzito akifika kliniki anaruhusiwa kuulizia huduma ya upimaji ili aweze kujua afya yake mapema anapo hisi kwamba ni mjamzito.
“Mimi kama daktari bingwa wa Watoto ninasikitika sana ninapoona mtoto amekuja kulazwa hospitali na maginjwa nyemelezi wakati njia ya kuzuia ilikuwepo na ipo mpaka sasa. Kuna vifo vingi vya Watoto wanaoishi na VVU inayofikia hadi asilimia 7 ya Watoto wanaotumia dawa. Tanzania tuna takribani Watoto 62,000 wenye umri wa miaka 0 hadi 14 waliogundulika na kuanzishiwa dawa za kufubaza VVU.
Changamoto kubwa kwa Watoto wanawategemea watu wazima wawatunze na kuwalea, na wakiwa wanaishi na VVU basi walezi walipaswa wawape dawa kama inavyostahili. Sasa wazazi wengi hawapi Watoto dawa kwa usahihi, mara nyingine unakuta dawa alizopewa hakuzihifadhi kwenye kopo lake zinapoteza ubora na kutokufanya kazi yake.
Wazazi na walezi wengine hawawaambii Watoto wana shida gani kwa hiyo Watoto wanapokosa majibu sahihi wanaacha au kukataa kuendelea na dawa, Haya yote yanachangia sana kuzorota kwa huduma endelevu.
Ninaungana na mashirika ya kimataifa Pamoja na malengo mkakati ya kitaifa ya kukabiliana na kutokomeza kabisa maambukizi mapya kwa Watoto kutoka kwa mama, pia kutoa huduma stahiki na mwendelezo kwa wale ambao walikwisha kuambukizwa ili waweze kuishi Maisha bora yasiyokuwa na magonjwa ya mara kwa mara. Kauli mbiu yetu ni “mtoto Kwanza” kwa hiyo kipaumbele chetu kiwe ni kuhakikisha mtoto anakuwa salama kwa ajili ya maendeleo ya taifa la sasa na lijalo” Amesema Dr. Theopista Jacob.
SULUHISHO LAKE NI LIPI?
Ni wito wetu madaktari na watoa huduma wa afya kwa wazazi na jamii nzima kulichukulia uzito suala zima la kumlinda mtoto asipate VVU kwa kuwa inawezekana kabisa.
Serikali kupitia maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani ya mwaka Desemba 01, 2022, yaliyofanyika Mkoani Lindi kitaifa imesema itaimarisha huduma za upimaji wa VVU na matumizi ya ARV ili kutokomeza vifo vitokanavyo na UKIMWI hususan kwa Wanaume, Vijana, Watoto na makundi maalumu.
Kuweka mikakati ya kutokomeza ubaguzi na unyanyapaa kwa WAVIU, Elimu ya kutosha itolewe kwa watoa huduma za afya, maofisini na katika jamii ili kupambana na hali ya ubaguzi na unyanyapaa.
Na, John Kabambala.