Ni wastani wa kilomita moja hivi, kutoka ilipo shule kongwe ya msingi inayotumia lugha ya kiingereza kufundishia (English Medium Primary School) katika Manispaa ya Morogoro hadi kufika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, yaani Ikulu ndogo ya nchi. Shule hii ipo pembezoni kabisa mwa mto Morogoro unaotiririsha maji yake kutoka katika miamba ya milima ya Uluguru. Hapa ndipo penye historia kubwa kuhusu Elimu ya awali na msingi Mkoani Morogoro.
Leo tutaiangazia shule ya msingi iliyopo katika kata ya Mji Mkuu ijulikanayo kwa jina la Nguzo English Medium Pre and Primary School. Hii ni shule ya kutwa yenye wanafunzi wa kike na wa kiume, ambayo kwa upande wa kaskazini imepakana na uwanja mzuri wa mchezo wa gofu, na ukitupa macho yako pembeni kidogo mwa uwanja utajikuta unatazama na Morogoro Hotel. wengi wanaweza wasiifahamu shule hii lakini ni miongoni mwa shule kongwe kabisa ya binafsi kuwahi kufunguliwa katika Manispaa ya Morogoro.
Ndani ya Makala hii mna mjumuiko wa maelezo kutoka kwa watu watatu ambao ni Mwalimu mkuu, Mwalimu mkuu mtaafu ambaye amekuwepo shuleni takriban miaka 40 na Daktari aliyesoma katika shule hii kuanzia darasa la awali hadi darasa la saba.
Tahiya Mohamed ni mwalimu mwenye uzoefu wa miaka arobaini (40) katika shule ya Nguzo, yeye anaanza kutueleza historia fupi ya shule hii. Kwanza anafafanua majina ya shule hii iliitwaje kabla ya jina la sasa “Expertriate and Overseas Educational Association” hili ndilo jina la kwanza kabisa la shule hii ilipoanzishwa na uongozi wa kikoloni wakati huo.
LENGO LA KUANZISHWA SHULE HII
Wakati huo katika mkoa wa Morogoro hapakuwa na shule ya binafisi ambayo ilikuwa ikitoa elimu yenye vigezo vya mtaala wa kimataifa, ambapo wakoloni walilazimika kuwarejesha watoto wao nchini kwao ili waweze kupata elimu, jambo ambalo liliwatenga mbali na familia zao.
Kutokana na sababu hizi muhimu kwao, waliamua kujenga shule kwa lengo la kutoa huduma ya kuwafundisha watoto wa viongozi wa kikoloni waliokuwa wakiishi eneo hili la Manispaa ya Morogoro, kwa hivyo shule hii wakati huo ilitumia mtaala wa kimataifa.
“Baada ya viongozi hao wa kikoloni kuondoka na familia zao kurejea nchini kwao, shule hii ilianza kumilikiwa na tajiri mmoja mwenye asili ya kiashia aliyekuwa akiishi eneo hili la Manispaa ya Morogoro aliyejulikana kwa jina la Taj Mohamed.
Ilipoanza kumilikiwa na Taj Mohamed ndipo jina la shule lilipobadilishwa na kuitwa Nguzo English Medium Primary School. Waliosoma katika shule hii enzi hizo wengi wao walikuwa ni watoto kutoka familia zenye asili za kiarabu na kihindi. Pia walisoma watoto wa viongozi wa Serikari ngazi ya juu na wafanya biashara wakubwa. Mwaka 1973 shule ilisajiliwa rasmi na kuruhusiwa kutumia mtaala wa Tanzania badala ya mtaala wa kimataifa kama ilivyokuwa awali”.
KITAALUMA
Shule hii ina walimu wenye umahiri na uzoefu wa kufundisha watoto katika rika zote kuanzia darasa la awali hadi darasa la saba. Shule ya Nguzo inayo maktaba yenye vitabu vinavyoendana na umri, nyakati na vyenye kumjengea mtoto kupata umahiri wa kujua kusoma, kuandika na kuhesabu. Tangu shule hii iruhusiwe kutumia mtaala wa Tanzania hakuna mwanafunzi aliyewahi kufeli mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi.
NAFASI YA SHULE KITAALUMA KATIKA NGAZI YA WILAYA NA MKOA:
Aboud Masoud ambaye ni mwalimu mkuu wa shule hii anasema “Shule ya Nguzo imeendelea kufanya vizuri katika matokeo tangu ilipoanza kufanya mitihani ya taifa darasa la saba hadi sasa. Shule hii ina historia ya kutunukiwa vyeti vya ubora shule kitaaluma kutoka Wizara ya Elimu na Utamaduni pamoja na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI kwa nyakati tofauti baada ya kushika nafasi ya kwanza, ya pili na ya nne katika matokeo ya darasa la saba”.
Katika matokeo ya darasa la saba ya mwaka 2021 shule ya Nguzo imekuwa katika nafasi ya 16 kati ya shule 77 ngazi ya Wilaya na nafasi ya 22 kati ya shule 640 katika ngazi ya Mkoa.
Wanafunzi waliohitimu darasa la saba mwaka huu 2022 ni 101.
MAZINGIRA NA AFYA ZA WATOTO SHULENI
“Mwalimu Aboud Masoud anasema mazingira ya shule ni mazuri tukianzia majengo ya madarasa, viwanja vya michezo na miti yenye kivuli iliyozunguka eneo lote la shule. Aidha ukizingatia kuwa shule yetu ipo mjini jirani na Manispaa pamoja na ofisi za mkuu wa Mkoa huduma zetu ni tofauti kabisa na shule nyingine. Usimamizi na ulinzi ni wa kutosha, hakuna mtoto anayeruhusiwa kutoka nje au mtu kuingia ndani pasipo ruhusa ya mlinzi getini.
Hapa shuleni tuna mwalimu wa afya ambaye anasimamia masuala ya afya za watoto, ambapo watoto wanapopata changamoto ya kiafya hupatiwa huduma ya kwanza kabla ya kupelekwa hospitali kwa uchunguzi na matibabu Zaidi”.
KIWANGO CHA ADA KWA MWAKA MZIMA
Aidha Mwalimu Aboud Masoud anasema shule hii ilipoanza kumilikiwa na ndugu Taj Mohamed aliamua kutowatoza ada kubwa watoto watakaosoma hapa, bali watozwe ada inayolenga kuwapa wananchi huduma na sio kufanya biashara kama zilivyo shule nyingine zisizo za serikali. Ambapo kwa miezi sita mzazi humlipia mtoto wake Shilingi 270,000/= na kwa mwaka mzima hulipa Shilingi 540,000/=.
WATU MAARUFU WALIOSOMA SHULE HII
Bi, Tahiya Mohamed anasema “najivunia kazi yangu ya ualimu, ninaifurahia sana hasa unapoona wanafunzi uliowafundisha kuanzia darasa la awali hadi darasa la saba wakiendelea ngazi za juu za elimu pasi na kurudi nyuma kimasomo. Wengi niliowafundisha walisomea udaktari, kwa mfano miongoni mwao ni Dkt.Taibali ambaye ni mwanzilishi wa Hospital ya Hakimi, Dkt. Mukhi na Dkt. Abizer. Mbali na hao wapo wahadhiri wa vyuo vikuu mbalimbali nchini, makatibu wakuu na wengine wengi waliowahi kusoma katika shule hii”.
Nilifanikiwa kumtafuta na kumuhoji Dkt. Taibali Abderasul. Kwanza nilimuuliza ni jambo gani utaendelea kulikumbuka katika maisha yako kutoka shule ya Nguzo Primary School wakati huo? “Tulifundishwa misingi thabiti katika maisha ya kujitegemea pasipo kumtegemea mwingine kwamba yupo atanisaidia, tulipewa mbinu za bata na kuku wa kienyeji za kujitafutia baada ya kupewa masomo yetu ya mwanzo kuanzia darasa la awali na msingi na huo ndio mwanzo bora wa mafanikio ya maisha ya mtu kielimu” Alisema Daktari Taibali.
Dkt.Taibali ni mwanzilishi wa hospitali ya hakimi iliyopo katika kata ya Kilakala Manispaa ya Morogoro ambayo ni miongoni kati ya hospitali zinazotoa huduma bora zaidi,. Yeye alimaliza darasa la saba mnamo mwaka 1994, na kufanikiwa kuchaguliwa kuendelea na masomo ya Sekondari katika shule nyingine.
Ni mtaalamu na mbobezi katika magonjwa ya moyo, anasema msingi alioupata wakati huo katika shule ya Nguzo English Medium Pre and Primary School, kuanzia darasa la awali hadi darasa la saba ulikuwa imara na ndio uliochangia yeye kufika hapo alipo sasa ambapo kazi yake kubwa ni kuisaidia jamii katika kushauri na kutibu magonjwa mbali mbali ya moyo.
ZIARA ZA MAFUNZO (STUDY TOUR)
Mbali na kupumzisha akili, njia moja wapo ni ya kujifunza kwa kuona na kusikia, “tunapo mfundisha mtoto umuhimu na faida za kutunza kumbukumbu za kale ni lazima tumpeleke kwenye majumba ya makumbusho akaone kwa macho yake mwenyewe.
Tunapomfundisha mtoto faida za kutunza mazingira, misitu na wanyama ni lazima tumpeleke kwenye hifadhi za misitu na wanyama akajionee mwenyewe, kwa kufanya hivyo anakuwa na uwezo wa kufanya vizuri zaidi katika masomo yake”
Mwl. Masoud alipambanua juu ya umuhimu za ziara shuleni.
Wasiliana na Mwalimu Mkuu wa shule hii Ndugu Aboud Masoud kwa namba hii 0789 034 904.
JICHO LA MWANDISHI WA MAKALA HII
Mojawapo ya vigezo muhimu zaidi kwa mzazi au mlezi anavyo paswa kuzingatia wakati wa kufanya uchaguzi wa shule atakayompeleka mwanawe kusoma ni pamoja na kufahamu Mazingira, Afya na Usalama wa mtoto awapo shule hapo.
Nguzo English Medium Pre and Primary School, inafaa kwa sifa hizi muhumu, ipo katika eneo tulivu na lenye ulinzi wa kutosha katika pande zote za shule, eneo hili asikari hufanya doria kila baada ya muda mfupi, kutokana na umuhimu wa ofisi zilizopo na viongozi wakuu wa Serikali wanaoishi katika eneo hili.
Mazingira anayoishi mtoto wakati awapo katika shule hii, hayawezi kumfanya apate magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu, hii ni kwa sababu shule inatunzwa katika hali ya usafi wakati wote.
Na, John Kabambala.