Warsha iliyowakutanisha Wahariri na wawakilishi wa vyombo vya Habari nchini Tanzania iliyoandaliwa na Shirikia la Gesci kutoka Nchini Kenya kwa kushirikiana na Taasisi ya Milele Zanzibar Foundation kutoka Zanzibar ilifanyika Jumamosi ya tarehe 11 March 2023 katika Hoteli ya Double View iliyopo Kata ya Sinza Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo Jijini Dar es salaam kwa ajili ya kuitamburisha Ripoti ya ALiVE kwa wanahabari, pamoja na kuutamburisha Mradi wa ADAPT.
Samson John Sitta Mratibu wa Mradi wa ALiVE nchini Tanzania katika mahojiano baada ya Warsha, ameiambia Tanzania Kids Time kwamba pamoja na lengo la Warsha hiyo ya Siku moja kuwa ni kuitamburisha Ripoti ya Tathmini ya upimaji Stadi za maisha na maadili kwa vijana (13 – 17) Afrika mashariki (ALiVE), lakini pia ilikua ni kutoa taarifa ya utafiti kutoka katika Mradi mwingine wa ADAPT na kuwaeleza wanahabari namna gani ripoti hizo zitatumika kufanya uchechemuzi katika Sera za Nchi ili kuleta maboresho ya mitaala ya Elimu.
“Lengo la kukutana hapa ilikua ni kuwapitisha wanahabari katika Ripoti yetu ya upimaji wa Stadi za maisha kwa vijana wa umri wa miaka 13 – 17 Afrika mashariki, pamoja na hilo tulikua tunawasilisha taarifa nyingine ya mradi mwingine wa ADAPT ambao ni Mradi Dada wa ALiVE unaohakikisha baada ya utafiti na Ripoti kutoka ni kwa namna gani matokeo yake yanaweza kutumika katika kufanya uchechemuzi katika Sera” Alisema Samson John Sitta, hii hapa ni sauti ya Samson John Sitta.
Mwandishi wa Habari Hughes Dugilo kutoka Dar es salaam alikua miongoni mwa wanahabari walioshiriki katika Warsha ya iliyoandaliwa na Shirika la Gesci, alishukuru na kupongeza kwa jinsi miradi hiyo miwili inavyoshirikiana kutoa matokeo ya mahili za Stadi za maisha na maadili kwa vijana wa Afrika ya mashariki na kuhakikisha hatua zinachukuliwa kwa watunga Sera kisha Serikali kuchukua hatua ya kufanya mabadiliko, lakini pia alieleza namna alivyo na wajibu katika kuhabarisha Jamii kuhusu Stadi za maisha na maadili.
Mwandishi wa Habari Hughes Dugilo alisema, “kwanza nipongeze miradi ya ALiVE na ADAPT, leo tumeongeza ufahamu zaidi kuhusu Stadi za Maisha na Maadili, tukizungumzia Stadi za maisha tunagusa maeneo mengi, masuala ya kujitambua, kujitegemea na mimi kama Mwandishi wa Habari nina wajibu mkubwa sana baada ya Warsha hii, kwanza kutekeleza majukumu yangu katika kuihabarisha Jamii kwa ujumla kuhusu Stadi za maisha kwa vijana. Adhima ni kuona vijana wazitambua stadi za maisha, wazisimamie na waziishi ili baadae waje kuwa watu wa kulisaidia Taifa letu” Sauti ya Hughes Dugilo.
Mradi wa ALiVE ambao uko chini ya Taasisi Milele Zanzibar Foundation, ulifanya tathmini yake ya upimaji Stadi za maisha na maadili kwa vijana Afrika mashariki kwanzia Mwaka wa 2020 hadi 2022 upande wa Zanzibar na Tanzania Bara ili kuangalia Mahili za Stadi za Maisha na Maadili waliyonayo vijana katika Halmashauri za Wilaya 45 (Wilaya 11 kutokaTanzania visiwani na 34 za Tanzania Bara).
Mradi wa upimaji Stadi za Maisha na Maadili kwa vijana wa umri wa miaka 13-17 uliofanywa na Taasisi ya Milele Zanzibar Foundation kutoka Zanzibar ulijikita kutafiti Stadi za Maisha Tatu ambazo ni kujitambua, ushirikiano, utatuzi wa matatizo pamoja na kutafiti Tunu (Maadili) ya Heshima, ambapo upande wa Zanzibar jumla ya vijana wa kike na wakiume 2,447 wamehojiwa katika Kaya 1,942.
Upande wa Tanzania Bara Mradi wa ALiVE umewafikia vijana 14,645 katika Kaya 11,802.
KWA NINI MRADI WA ADAPT KUTOKA SHIRIKA LA GESCI UNAHUSIKA.
Kwa mujibu wa Ramadhani Matimbwa Mratibu wa Mradi wa ADAPT Kutoka Shirika la GESCI la nchini Kenya, Mradi wa ADAPT ambao kirefu chake ni (Adapting of Assesment into Policy and Learning) mradi ambao umejikita kufuatilia hatua kwa hatua namna matokeo ya tafiti yanavyoweza kutumika vyema katika kufanya uchechemuzi kwa watunga Sera na kuleta mabadiliko chanya ya tafiti hizo.
“ADAPT Pia inajaribu kuchechemua tafiti za ALiVE namna tunavyojenga uwezo wetu sisi ni kwa kujadili hizi tafiti mbalimbali, tunawaita watu kwa pamoja tunawaeleza kile tunachokiamini ili kwa pamoja tukielewana mnaweza kujenga jambo Fulani lakini pia tunavyokutana na wahariri na wanahabari kwetu inatusaidia kufikisha taarifa hizi kwa Jamii na Serikali kwa sababu ADAPT lengio lake kubwa ni kufanya mabadiliko, sasa mabadiliko yale huwa yaanzia kwenye mijadala” Alisema Ramadhani Matimbwa, na hii hapa ni sauti yake.
MFANO WA YALIYOMO KATIKA RIPOTI YA ALiVE TANZANIA VISIWANI.
Kutoka katika ukurasa wa Tano wa Ripoti ya ALiVE Zanzibar kipengele cha Stadi ya Maisha ya “UTATUZI WA MATATIZO” Ripoti imebainisha 23% ya vijana wanapata wakati mgumu kutambua tatizo au asili yake kimtazamo na kwa hivyo hawawezi kutambua suluhisho lake.
Asilimia 48% ya vijana wanauwezo wa kutambua uwepo wa tatizo kutoka kwa mtu kimtazamo na kuchukua hatua ili kutambua uwezekano wa kupata suluhisho, 15% ya vijana wanauwezo wa kutambua uwepo wa tatizo kutoka kwa mtu kimtazamo, kutambua njia kuu za kutatua tatizo na kuweza kusuluhisha.
Lakini pia Ripoti imesema 14% ya vijana wanauwezo wa kutambua uwepo wa tatizo kutoka kwenye mitazamo mingi, kuwa na njia nyingi za suluhisho na kuchagua njia ipi inaweza kutumika kutatau tatizo.
SHIRIKA LA RELI LILIVYOFANIKISHA KUPATIKANA KWA MIRADI YA ALiVE NA ADAPT
Mtandao wa Elimu Afrika Mashariki unaofahamika kwa jina la RELI, (Regional Education Learning Initiative in East Africa) unafanya kazi katika Nchi Tatu za Afrika ya Mashariki ambazo ni Kenya, Uganda na Tanzania ambao hadi sasa una zaidi ya wanachama 70 ambao ni mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali kwa lengo la kuhakikisha ujifunzaji jumuishi kwa watoto wote katika Afrika Mashariki.
Mradi wa ALiVE unaotekelezwa na Taasisi ya Milele Zanzibar Foundation umetoka katika Kongani ya Stadi za Maisha na maadili ikiwa ni moja ya Kongani Nne zilizopo katika Mtandao wa RELI.
Mradi wa ADAPT unaotekelezwa na Shirika la Gesci kutoka nchini Kenya nao pia unatoka katika Kongani ya Stadi za Maisha na Maadili kwa lengo la kuleta mabadiliko kupitia ufuatiliaji wa matokeo ya tafiti mbalimbali na kuona kwa namna gani watunga sera wanaweza kuleta mabadiliko.
Ifahamu kwa undani RELI: RELI – Regional Education Learning Initiative in East Africa (reliafrica.org)