Na, John Kabambala-Morogoro. Afrika na kusini mwa Jangwa la
Sahara, saratani ya shingo ya kizazi ndiyo inayoongoza kwa vifo vinavyotokana
na saratani kwa wanawake, Afrika Mashariki ina idadi kubwa ya matukio na vifo
vinavyotokana na saratani ya shingo ya kizazi na ndiyo saratani inayowapata
wanawake wengi zaidi Afrika mashariki, Nchini Tanzania, ndicho kisababishi
kikuu cha saratani kwa wanawake wenye umri wa miaka 15-44, na matukio ya kila mwaka na vifo vya takriban 9,772 na 6,695 mtawalia. Taarifa hiyo nikwamujibu wa ripoti ya- Barriers
to Human Papillomavirus (HPV) Vaccination of Adolescent Schoolgirls in Morogoro
Municipality, ilioandaliwa na The Muhimbili University
of Health and Allied Sciences October, 2021.
Saratani ya shingo ya
kizazi ni saratani ambayo hutokana na mabadiliko ya mfumo wa chembechembe au
cells zilizoko katika shingo ya kizazi, mabadiliko haya hupelekea chembe chembe
hizo kushamiri na kuzaliana kwa kasi kinyume na mpangilio wa maumbile, inasemekana
kuwa ni saratani inayoongoza kwa kusababisha vifo vya wanawake katika nchi
zinazoendelea. Ripoti ya mwaka 2012 ya shirika la afya duniani ‘WHO’ inasema
kati ya matukio 75,000 ya waathirika wa saratani ya Shingo ya kizazi barani
Afrika, 50,000 walifariki dunia.
NINI KINACHOSABISHA SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI?
Taasisi ya Saratani Ocean Road inaonesha, Ripoti za utafiti wa kisayansi zimeafiki kuwa
asilimia 99% ya saratani za shingo
ya kizazi hutokana na maambukizi ya virusi vya ‘Human Papillomavirus’ au HPV
vilivyoko katika jamii ya papilloma, baadhi ya virusi hivi vyenye aina zaidi ya
mia moja huambukizwa kwa njia ya kujamiana. Miongoni mwake ni Kufanya ngono zembe, Kuwa na wapenzi wengi, Kukoma
siku katika umri mkubwa, Utumiaji mafuta mengi katika chakula, Kutokufanya
mazoezi ya mara kwa mara, Unene kupita kiasi, Uvutaji sigara, Utumiaji wa pombe
kupita kiasi na Historia ya saratani ya matiti katika familia.
Visababishi vingine vya
hatari ni ndoa za utotoni, magonjwa ya zinaa ikiwa ni pamoja na maambukizi ya
VVU, upungufu wa vitamini na maambukizi ya HPV, chanjo hii inapotolewa kwa
wasichana wenye umri kati ya miaka 9 na 14, huwalinda dhidi ya saratani ya
shingo ya kizazi.
WATU GANI WAPO KWENYE HATARI ZAIDI?
Wasichana wanao anza
ngono katika umri mdogo na wenye umri mkubwa, pamoja na wanaotumia vidonge vya
kupanga uzazi kwa mda mrefu, Kuzorota kwa kinga ya mwili husabisha kuongzeka
kwa athari ya virusi wa HPV wanaoletekeza kansa ya shingo ya kizazi,Wanaopata
ujauzito katika umri mdogo chini ya miaka 17 wapo kwenye hatari Zaidi ya kupata
saratani hii.
CHANJO
HII ILIZINDULIWA LINI NCHINI TANZANIA:
Kwa mujibu wa WHO Tanzania, kwa mara ya kwanza
mwezi Aprili mwaka 2018, Tanzania
iliweka historia yakuwa miongoni mwa nchi zinazo tekeleza huduma ya utoaji na
usambazaji wa chanjo ya Human Papilloma Virus (HPV) dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi kwa wasichana, saratani
hii ni yapili kwa wanawake duniani kote, na katika ukanda wa Afrika Mashariki
ndio unaoongoza kwa kubeba mizigo ya saratani ya shingo ya kizazi na Tanzania
ilikuwa ni kati ya nchi tano zenye viwango vya juu zaidi barani Afrika.
Uzinduzi wa kitaifa
wa chanjo ya HPV ulifanywa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati huo ambae kwa sasa ni Rais wa Taifa
hilo, Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu, Wawakilishi wa Nchi wa WHO na UNICEF,
pamoja na wageni wengine kutoka mashirika mbali mbali.
Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, alipokuwa mgeni rasmi
alithibitisha dhamira ya serikali ya kuhakikisha lengo la chanjo ya wasichana 616,734 linafikiwa na kuwataka wazazi
na walezi kutokosa ‘fursa nzuri’ ya kupata chanjo hiyo watoto wao kupewa
chanjo.
KABLA YA KUZINDULIWA CHANJO YA HPV:
Kabla ya kuzinduliwa kwa chanjo
ya HPV, utetezi wa jamii na uhamasishaji ulifanyika katika ngazi zote, Elimu ya
HPV ilitolewa kupitia Televisheni na Redio katika ngazi ya Taifa wakati katika
Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kama halmashauri zingine, walimu wa afya
kutoka shule za Sekondari na Msingi walipatiwa mafunzo ya chanjo ya HPV ambao
nao wangeweza kuhamisha maarifa kwa wanafunzi na wafanyakazi wenzao na
kushirikiana kupanga ratiba za chanjo kwa wanafunzi wanaostahiki.
Tangu kuzinduliwa kwa chanjo ya
HPV mnamo 2018, katika Manispaa ya
Morogoro, chanjo ya dozi ya kwanza na ya pili ya HPV ni 84% na 48% ilifikiwa Desemba 2019,
Utoaji huu mdogo hasa wa kipimo cha pili cha chanjo ya HPV una athari kwa afya
ya uzazi ya wanawake vijana ya siku za usoni, na kwa hivyo inahitaji uchambuzi
wa kina wa vikwazo vya utumiaji wa chanjo hii mpya iliyoletwa.
Ripoti hiyo mpya iliotolewa
mwezi April, inaonesha watoto milioni 67
hawakuchanjwa kati ya mwaka 2019 na 202, Idadi ya waliochanjwa ilipungua
katika mataifa 112, ikiwemo
Tanzania na Watoto waliozaliwa kabla au
baada ya janga la Corona, sasa wameingia kwenye kipindi ambacho wamevuka awamu
ya umri wa kuchanjwa , hali inayousisitizia umuhimu wa kuchukua hatua za ziada
kuwahudumia waliikosa na kuzuwia maambukizi ya magonjwa hatari.
Takwimu za UNICEF
zinaashiria kuwa kati ya watoto milioni 67 waliokosa chanjo zilizoratibiwa kati
ya 2019 na 2021, milioni 48 hawakupokea chanjo yoyote, Watoto walio katika hali
mbaya ni wale wa mataifa masikini zaidi ambayo huenda pia yanazongwa na vita
namaendeleo duni.
CHANJO HII INASAIDIA
NINI?
UNICEF inasema:
Chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi (HPV) inasaidia kulinda dhidi ya
kansa kadhaa, haswa saratani ya shingo ya kizazi, ambayo inakadiriwa kuwa
chanzo cha nne cha vifo vya saratani kati ya wanawake ulimwenguni kote, katika
nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika, chanjo ya HPV ilipungua kati ya 2019 na 2021 nchi hizo ikiwe Tanzania licha
ya maendeleo yasiyopingika kwa miongo mingi, ya uzingatiaji wa utoaji chanjo, imeendelea
kukabiliwa na changamoto kadhaa utekelezaji wa jambo hilo.
Ripoti hiyo inasema, Utoaji wa chanjo umerudi nyuma,
au umedumaa, katika maeneo mengi sana, Tunazidi kuwakosa watoto walio na chanjo
za kuokoa maisha, haswa watoto waliotengwa kijamii na maskini zaidi, na hali
imekuwa mbaya zaidi wakati wa janga hili, Kushindwa kwa mifumo ya afya kufikia
kila mtoto na chanjo kunaonyesha uwekezaji mdogo wa nyumbani katika huduma ya
afya ya msingi, rasilimali watu duni kwa afya, na mapungufu ya uongozi katika
ngazi na maeneo mbalimbali ya serikali.
Kupungua kwa chanjo katika kipindi chote cha janga
hili kunapaswa kuchukua hatua sasa dhidi ya utoaji chanjo na lazima iwe
kipaumbele katika miaka ijayo, Ni lazima tuchukue hatua za pamoja ili kuwapata
watoto waliokosa chanjo wakati wa janga hili, kujenga upya mifumo na
kukabiliana na mapungufu makubwa katika mifumo ya afya, kushindwa kuchukua
hatua kutaharibu maisha ya watoto wa leo na vijana na watu wazima wa kesho, na
kutarudisha nyuma maendeleo zaidi ya SDGs.
DALILI ZA SARATANI HII NI ZIPI?
Kutokwa na majimaji au
uchafu wenye harufu kali ukeni, Kutokwa na damu ukeni mbali na siku za mwezi au
baada ya tendo la ndoa, Maumivu makali ya sehemu ya chini ya tumbo ( pelvic
area), Kuhisi maumivu makali wakati wa kujamiiana, Kupungua kwa uzito wa mwili
bila kukusudia, Mkojo wenye matone ya damu.
KIPI UFANYE KUZUIA SARATANI YA SHINGO YA
KIZAZI?
Usivute sigara wala
kutumia tumbaku ya aina yoyote pia Hakikisha nyumbani kwako hamna moshi, Kuwa
na mpenzi mmoja, Usichangie mapenzi na watu wengi, Kula chakula chenye afya
hasa vyakula asilia, Kunyonyesha kunapunguza hatari kwa mama kuugua saratani, Hakikisha
watoto wako wanapata chanjo dhidi ya hepatatis B na HPV, Epuka kuchomwa sana na
miale ya jua, au tumia mafuta yanayo kukinga dhidi ya miale hiyo, Epuka
matumizi ya Dawa za uzazi wa mpango zenye madhara, Jishughulishe kuupa mwili
mazoezi, Punguza unywaji wa pombe na Jitahidi kufanyiwa ukaguzi wa mapema
kutambua uwepo wa saratani.
Saratani ya shingo ya
kizazi inazuilika au kutibika kabisa endapo itagundulika ikiwa kwenye hatua za
awali, hivyo ni muhimu kufanya uchunguzi wa afya yako kwa kadiri
utakavyoshauriwa na wataalam wa afya Wanawake wote walio na umri kuanzia miaka
30 na kuendelea wanatakiwa kufanya uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi, Kumbuka: Wakati wa uchunguzi wa saratani ya shingo
ya kizazi ni sasa usisubiri hadi uone dalili, fika kituo cha huduma za afya kwa
ushauri/mwongozo Zaidi.