Na, John Kabambala.
“Lishe bora ni haki ya kibinadamu”
Utapiamlo ni hali ya upungufu wa lishe au lishe iliyozidi. Tunapozungumzia
upungufu hapa tunazungumzia udumavu ambao ni utapiamlo wa muda mrefu (chronic
malnutrition), ukondefu ambao ni utapiamlo wa dharura (Acute Malnutriton) na
uzito pungufu (Underweight) ambao huonekana kwa watoto wenye udumavu na
ukondefu. Vile vile utapiamlo unaweza kuwa wa upungufu wa virutubishi muhimu
vya vitamini na madini ambavyo pamoja na kwamba mahitaji yake ni kidogo lakini
umuhimu wake ni mkubwa sana kwa afya na Ustawi wa binadamu.
Upungufu wa vitamin na madini unajulikana pia kama utapiamlo
uliojificha au (hidden hunger) kwa kuwa madhara yake hayaonekani mapema. Aina
nyingine ya utapiamlo ni ule wa lishe iliyozidi ambayo inapelekea magonjwa sugu
yasiyoambukizwa yatokanayo na chakula, kama kisukari, magonjwa ya moyo,
shinikizo la damu na hata baadhi ya saratani.
SABABU ZA UTAPIAMLO ZIMEGAWANYIKA KATIKA MAKUNDI MATATU:
Sababu za karibu (immediate causes), Ulaji duni na Magonjwa,
Sababu zilizojificha (undelying causes) hizi ni zile sababu zinazopelekea uwepo
wa sababu za karibu ambazo ni, Upungufu wa uhakika wa chakula katika kaya,
Upungufu katika matunzo ya makundi maalumu ya watu, na Upungufu katika huduma
za msingi za afya katika jamii.
Sababu za Msingi (Basic causes) hizi ni zile sababu
zinazopelekea kuwepo kwa sababu wezeshi na sababu za karibu: Elimu duni
Rasilimali, Udhibiti wa rasilimali watu, uchumi na rasilimali za mashirika, Mfumo
wa siasa na itikadi, Mfumo wa uchumi, mila na desturi.
Sekta mtambuka zinahusika na kuzuia utapiamlo ni sekta za
kilimo na uhakika wa chakula, Afya na Ukimwi, Maji, mazingira na usafi, Elimu,
Maendeleo ya mtoto, usalama katika Jamii, Mazingira na mabadiliko ya tabia
nchi, Mipango, Maendeleo ya Jamii na Jamii kwa ujumla.
NIKWA NAMNA GANI
UTAPIAMLO KWA WATOTO UTAZUILIWA?
Kwa mujibu wa nyaraka kutoka kwenye mashirika mbalimbali
yakiwemo ya kimataifa kamavile UN
NUTRITION, WHO,UNICEF, SCI na mengine yanaonesha kwamba, ni muhimu kusimamia hali ya lishe
ya wanawake katika umri wa kuzaa ili watakapokuwa wajawazito wawezeshe kukuwa
vyema kwa kiumbe kinachokuja. Siku 1000 ni za Msingi sana katika kuzuia
utapiamlo kwa watoto. Siku 1000 zinajumuisha siku 270 za ujauzito, siku 730 za
mtoto katika miaka miwili ya mwanzo. Udumavu unaotokea na kutorekebishwa katika
siku 1000 za kwanza hautaweza kurekebishwa tena.
Afua zinazolenga kupunguza/kuzuia udumavu na utapiamlo ni
zile zinazolenga siku 1000 ambazo ni kuanzia mama anapokuwa mjamzito hadi mtoto
anapofikia umri wa miaka miwili, Kuboresha lishe ya Jamii yaani watoto wadogo
na wachanga, vijana, wanawake na wanaume, Mama kuhudhuria kliniki mara
anapojihisi mjamzito, Mjamzito kupata dawa za kuongeza damu madini chuma na
aside ya foliki na Mjamzito kupata dawa za kutibu malaria na minyoo.
Mwenza na Mjamzito kupata ushauri wa lishe, kupumzika wakati
wa ujauzito na maandalizi ya Uzazi, Matibabu ya magonjwa wakati wa ujauzi na Mama
mzazi kupata dawa za kuongeza damu na nyongeza ya vitamin A katika siku 42
baada ya Uzazi, Mama mzazi anashauriwa kupata Huduma za Uzazi wa mpango ili awe
na muda wa kulea mtoto na familia, Mama mzazi anashauriwa lishe yake mwenyewe
wakati wa ujauzito na anaponyonyesha, Mama anashauriwa kunyonyesha mtoto maziwa
ya mama tuu mara anapozaliwa kwa muda wa miezi sita ya mwanzo na Mtoto
aanzishiwe vyakula vya nyongeza mara anapofikia umri wa miezi sita huku
akiendelea kunyonyeshwa maziwa ya mama hadi atakapofikia umri wa miaka miwili
au zaidi.
Mama kumpeleka mtoto kliniki kwa ajili ya Huduma za chanjo
ili kuzuia magonjwa yanayozuilika kwa chanjo, Ushauri unatolewa wa njia za
kupata chakula kutoka makundi mbalimbali kwa kulima mbogamboga na kufuga
wanyama wadogo, Ushauri wa usafi wa mazingira, vibuyu chirizi na matumizi
ya vyoo bora na kanuni za usafi zinatakiwa kuzingatiwa ili kuzuia magonjwa
yanayoweza kupelekea utapiamlo kwa kuwa wakati wa ugonjwa watoto hukosa hamu ya
kula hivyo kupelekea kupungua uzito na wanapopungua uzito hali zao za kinga
hupungua hivyo kupelekea watoto kupata magonjwa ya mara kwa mara na mwisho
hufikia hali ya utapiamlo.
Mikakati ya kupunguza utapiamlo inatakiwa kufanyika katika
sekta mtambuka za kilimo na uhakika wa chakula, afya na UKIMWI, maji na usafi wa mazingira (WASH), Elimu, usalama katika Jamii (Social protection), mazingira
na mabadiliko ya tabia nchi na katika Ngazi ya Jamii kwa ujumla, Afua nyingine
za kupunguza utapiamlo ni pamoja na urutubishaji wa vyakula kama vile nafaka
kama unga wa ngano na mahindi zinaongezwa madini ya zinki na madini chuma,
vilevile asidi ya folik na vitamini B 12.
Mafuta ya kula huongezwa vitamin A na chumvi huongewa madini joto.
Watoto hupatiwa nyongeza ya vitamin A na dawa za kutibu
minyoo kila mwezi wa sita na wa kumi na mbili; Huduma hii hutolewa sambamba na
kupima hali ya lishe na kisha kupatiwa matibabu kwa wenye utapiamlo mkali.
HALI YA LISHE ILIKUWAJE MIAKA 13 ILIOPITA
MKOA MOROGORO?
Kwa mujibu wa Nyaraka muhimu kuhusu masuala ya Lishe kutoka
Ofisi ya Lishe Mkoa wa Morogoro zinaonesha kwamba, hali ya udumavu katika mkoa wa
Morogoro umepungua kutoka asilimia 44.4 (TDHS, 2010), asilimia 36.9 (NNS, 2014)
na kufikia asilimia 33.4 (TDHS, 2015-2016). Malengo ya kitaifa yalikuwa ni
kufikia asilimia 28 ifikapo mwaka 2021, Hali ya ukondefu (utapiamlo wa dharura)
ilikuwa asilimia 5 (TDHS, 2010) na kuongezeka mpaka asilimia 6 (TDHS,
2015-2016) malengo yalikuwa kufikia asilimia chini ya 5 mwaka 2021.
Upungufu wa damu kwa wanawake katika umri wa kuzaa ilikuwa
asilimia 45 (TDHS, 2010) na iliongezeka hadi kufikia asilimia 47.5 (TDHS,
2015-2016), kiwango hiki kilitakiwa kufikia asilimia 33 ifikapo mwaka 2021. Upungufu
wa damu kwa watoto chini ya miaka mitano kiliongezeka kutoka asilimia 59 (TDHS,
2010) hadi kufikia asilimia 65.7 kwa (TDHS, 2015-2016).
SASA HALI YA LISHE
IKOJE?
Utekelezaji wa afua za lishe Tanzania unafuata mpango
mkakati mtambuka wa lishe wa Taifa wa mwaka 2016-2021unaolenga watoto, vijana
wanawake na wanaume wa Tanzania wawe na lishe bora itakayopelekea maisha na
afya bora ambayo yataongeza uzalishaji na kuongeza uchumi wa mtu mmoja mmoja na
wa taifa hivyo kufikia Maendeleo endelevu. Maeneo saba ya kipaumbele ya Mkakati
mtambuka wa lishe wa Taifa (2016-2021) huo yalikua ni, kuinua lishe ya wanawake
katika umri wa kuzaa, watoto wachanga na wadogo na vijana, Kuinua mikakati ya
kuzuia na kutibu upungufu wa vitamin na madini, Kuinua mikakati ya
matibabu jumuishi ya utapiamlo wa dharura (ukondefu), Kuzuia na kutibu magonjwa
sugu yasiyoambukiza yatokanayo na chakula.
Kuinua mikakati jumuishi ya lishe katika sekta mtabuka
ambazo ni kilimo na uhakika wa chakula, afya na UKIMWI, maji na usafi wa mazingira (WASH), Elimu, usalama katika Jamii (Social protection), mazingira
na mabadiliko ya tabia nchi, Kuimarisha mikakati ya lishe na utawala katika
sekta mtambuka na Kuanzisha Uratibu wa takwimu za masuala ya lishe katika sekta
mtambuka.