Na, John Kabambala.
Mwanamke mmoja jasiri, mwenye macho yenye ndoto na mikono
iliyoshiba ardhi, alijulikana kwa jina la Hadija
Alisido mama wa familia na mkulima
wa kawaida katika kijiji chake. Kilimo kilikuwa chanzo cha kipato chake na cha
familia yake, lakini matatizo yalikuwa hayakwisha kumwandama. Hali ya hewa ya
kutatanisha, udongo usiokuwa na rutuba, na mavuno duni yalikuwa vitisho vikubwa
kwa kipato chake.
Lakini kama ilivyotokea katika visa vingine vingi vya
mafanikio, Hadija alipata fursa ya kipekee ambayo ilibadilisha
kabisa mustakabali wake. Fursa hiyo ilikuwa mafunzo ya kilimo hifadhi kutoka
Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kupitia mradi wa Pamoja
Kigoma (KJP) unaotekelezwa mkoani humo kwa ufadhili wa mashirika ya umoja wa
mataifa. Mafunzo haya yalimpa Hadija
mbinu mpya za kilimo, zilizokuwa zikitumia ardhi kwa ufanisi, kulinda
mazingira, na kuongeza uzalishaji wa mazao.
Jinsi Hadija alivyosikiliza kila somo kwa makini na kujifunza
kila hatua ya kilimo hifadhi kwa vitendo, ndivyo ndoto yake ya kuleta
mabadiliko kijijini ilivyokua na kuwa kubwa.Kisa hiki kinaendelea kusimulia safari ya Hadija kutoka kwenye udongo usiokuwa na matumaini
hadi kwenye mavuno mengi, kutoka kwenye ukame wa kutisha, na kutoka kwe kijiji
kidogo kilichokuwa hakina matumaini hadi kuwa kielelezo cha mafanikio na
matumaini kwa wanawake wa vijijini nchini Tanzania.
Mwanzoni Hadija
alikuwa akilima eneo la ukubwa wa heka tano na kila heka moja kwa wastani alikuwa
akipata mavuno ya gunia kumi, ambapo kwa heka zote tano jumla alikuwa akipata
gunia hamsini zisizo pungua kwa msimu mmoja, kiwango hicho cha mavuno aliokuwa
akiyapata Hadija hayakuwa yanakidhi
mahitaji yake kwa mujibu wa malengo yake ya kila mwaka.
Miongoni mwa malengo yake makubwa ya kila mwaka yalikua ni
kuishi masha mazuri, kuwasomesha watoto wake kwenye shule zenye gharama kubwa
kwa ajili ya kupata elimu ya uhakika, kujenga nyumba nzuri yenye mahitaji yote
ya msingi laniki pia na kuongeza shughuli zake za kilimo. Vuta nikuvute malengo
hayo hayakuwa yanatimia siku hadi siku na mwaka hadi mwaka kwa masikitiko
makubwa.
TATIZO LA KILIMO KATIKA KIJIJI CHAKE.
Tatizo kubwa ilikuwa ni changamoto za Ukame na Upungufu
wa Maji, Ukame mara kwa mara uliathiri kwa kiasi kikubwa mavuno ya mazao.
Maji ya mvua yalikuwa yanapungua, na udongo uliathirika kutokana na upungufu wa
uhifadhi wa maji. Aidha familia
nyingi zilikuwa zinapambana na umaskini kutokana na mavuno duni ya mazao,
ambayo yalitokana na mazingira ya udongo na hali mbaya ya hewa. Kutegemea
Mazao ya Kilimo cha kawaida kisicho kuwa na maarifa ya kutosha, Wakulima
wengi walipata mazao machache kila msimu kama mahindi, viazi, mihogo na maharage
na hawakutumia mbinu bora za kilimo ambazo zingesaidia kuongeza uzalishaji. Hii
ilisababishwa na ukosefu wa elimu ya kilimo kinacho himili mabadiliko ya hali
ya hewa.
CHANZO CHA TATIZO
Chanzo kikuu cha matatizo haya kilikuwa ukosefu wa maarifa
na mbinu za kilimo bora katika kijiji hiki. Wanakijiji walikuwa wakifuata kilimo
cha mazoea kilimo ambacho wazee wao walikitumia tangu enzi na ezni ambapo hakikuwa
na ufanisi tena wa kutosha kuwa na uzalishaji wa mavuno mengi kwa kipindi hiki
na kujibu changamoto za mazingira na mahitaji ya wakulima.
MAFANIKIO YA HADIJA.
Suluhisho la mafanikio ya Hadija lilikuwa maarifa na mafunzo ya kilimo hifadhi kutoka FAO.
Mafunzo haya yalimpa ujuzi na mbinu mpya za kilimo ambazo zilikuwa na manufaa
makubwa katika kupambana na changamoto za kilimo zilizokuwa zinamkabili. Mbinu
za Kilimo Hifadhi: Hadija alijifunza kwa undani mbinu za kilimo hifadhi,
kama vile kupanda mazao kwenye mistari na matumizi ya mbolea za asili. Hizi
zilikuwa njia zinazosaidia kuhifadhi ardhi na kuongeza uzalishaji wa mazao.
Uhifadhi wa Maji: Mafunzo yalimpa Hadija maarifa ya kuhifadhi maji, na
hivyo kudhibiti upatikanaji wa maji wakati wa ukame. Hii ilisaidia kulinda
mazao na kuwa na uhakika wa chakula hata wakati wa hali mbaya ya hewa. Kilimo
cha Mzunguko wa Mazao: Hadija
alipata ujuzi wa namna kulima kilimo cha mzunguko wa mazao ambacho kiliboresha
uzalishaji wa ardhi yake na kumuepusha na kuvu.
Kupitia mbinu za kilimo hifadhi, Hadija alifanikiwa kuongeza mavuno ya mazao yake mwaka huu alilima
eneo la ukubwa wa heka mbili na kuvuna mazao kiasi cha gunia miamoja na
ishirini za mahindi (120) kwa maana
kila heka moja alipata gunia sitini sitini (60).Mavuno haya yalikuwa ya kustajabisha maana hakuwahi kutokea
katika maisha yake yote ya kilimo kupata mazao kiasi hicho.
Hata hivyo kilimo
hifadhi kilisaidia kupunguza athari za ukame kwa kutumia mbinu za uhifadhi wa
maji, na kuboresha hali ya udongo. Hadija
hakuishia hapo tu, alilima mihogo na mavuno yake kwa mwaka huu amepata tani
sita ambazo alipouza mihogo hiyo alipata kiasi cha Tshs, 7,820,000/= kiasi ambacho alikuwa akikisikia tu kwa watu
wengine kikitajwa lakini sasa amekipata mwenyewe kwa kuuza mihogo alio ilima
kwenye shamba lake mwenyewe kwa kufuata elimu ya kilimo hifadhi iliotolewa na
FAO.
Ndoto yake ya kujenga nyumba na kusomesha watoto wake kwenye
shule zenye uhakika wa elimu imetiamia, ameweza kuwalipia watoto wake ada
katika shule hizo na kuboresha maisha yake ya nyumbani, kupitia yeye jamii yake
imeona sasa kumbe kilimo hifadhi ni mkombozi na niuhakika wa kupata mavuno
mengi yakutosha.
USHAURI WA NEEMA
KWA WANAWAKE WA KIJIJINI NA JAMII KWA UJUMLA
Hadija anatambua
kuwa maarifa na mafunzo ya kilimo hifadhi yalimwezesha kuleta mabadiliko katika
maisha yake na kijiji chake anaona nivema sasa kutoa ushauri wake kwa wanawake
wa kijijini na jamii kwa ujumla:
“Jifunzeni
na Kuweka Muda wa Kujifunza: Hadija
anaamini kuwa maarifa ni nguvu. Anawahimiza wanawake wa kijijini kujifunza
mbinu mpya za kilimo na kujitolea kwa mafunzo. Kuweka muda wa kujifunza
kunaweza kuleta mabadiliko makubwa katika uzalishaji wa mazao.
Shirikianeni na Jifunzeni Kutoka Kwa Wenzenu: Hadija anasisitiza umuhimu wa
kushirikiana na kujifunza kutoka kwa wenzao. Kuanzisha vikundi vya wakulima wa
kijijini kunaweza kuwa njia nzuri ya kusambaza maarifa na mbinu bora za kilimo.
Tumia Ardhi kwa Ufanisi: Hadija anaonyesha umuhimu wa kuhifadhi ardhi na kuilinda. Kwa
kutumia mbinu za kilimo hifadhi, ardhi inaweza kuwa na uzalishaji wa muda mrefu
na kuwa na rutuba zaidi.
Jifunzeni Kuendesha Miradi ya Maji: Hadija anahimiza jamii, utunzaji wa rasilimali muhimu
ya maji, na kudhibiti upatikanaji wa maji kunaweza kuwa na athari kubwa katika
kilimo na maisha ya kijijini.
Kuwa Mfano kwa Wenzako: Hadija anawaambia wanawake wa kijijini kuwa wanaweza kuwa mifano
kwa wenzao. Kwa kufuata mafanikio yao na kushirikisha maarifa yao, wanaweza
kuleta mabadiliko makubwa katika jamii zao. Kusaidiana na Kusimamia
Rasilimali: Jamii inapaswa kusaidiana na kusimamia rasilimali kwa
uwajibikaji. Kwa kushirikiana, wanaweza kuboresha hali ya maisha ya kijijini
kwa ujumla kwani wanawake wa vijijini ni mashujaa wa chakula.”
Kupitia siku ya wanawake wa vijijini FAO imemzawadia vifaa
muhimu vya kilimo mbele ya muwakilishi mkaazi wa Umoja wa Mataifa Zlantan
Milisic katika halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma. Nasasa Hadija anasema “natoa shukrani na pendo lisilo kifani kwa shirika la chakula na
kilimo la umoja wa Mataifa (FAO) kwa maarifa na elimu ya kilimo hifadhi familia
yangu inaneemeka kwa mavuno haya, msimu ujao nimejipanga zaidi kuliko uliopita”
Kwa ushauri wa Hadija,
wanawake wa kijijini wanaweza kuwa nguvu kubwa katika kuleta mabadiliko katika
kilimo na jamii zao. Kupitia kujifunza, kushirikiana, na kushirikisha maarifa,
wanaweza kuwa chachu ya maendeleo na kuondoa umaskini katika vijiji vyao. Kisa
cha kweli cha Hadija ni kielelezo
cha mafanikio na matumaini makubwa, na ushauri wake unaweza kuwa mwongozo wa
kuleta mabadiliko katika vijiji vya Tanzania na kote duniani.