Wawezeshaji wa mafunzo kutoka Shirika la Uwezo Tz, Milele Zanzibar
Foundation na RELI wakiwa katika picha ya pamoja na waandishi wa Habari.
Na Hamad Rashid
Mapema mnamo
Mwezi wa kumi na mbili tarehe nne mwaka huu wa 2023, Shirika lisilo la
kiserikali la Uwezo Tanzania liliratibu
mafunzo ya kuwajengea uwezo wanahabari juu ya uwajibikaji wao wa kuelimisha stadi
za maisha na maadili katika Jamii, mafunzo yaliyofanyika Jijini Dar Es Salaam
yakiwakutanisha waandishi wa Habari na wahariri kutoka,Tanzania Bara na Zanzibar
kwa kuwapa mafunzo na kusikia kutoka kwao ni upi mchango wao katika kufanikisha
uelewa wa stadi za maisha na maadili kwa mustakabakli wa Taifa, ikiwa ni awamu
ya pili ya Mradi wa ALiVE unaotekelezwa nchi tatu za Afrika Mashariki, (Tanzania,
Kenya na Uganda).
Meneja mawasiliano
na uchechemuzi wa Mradi wa “Tathmini ya Stadi za Maisha na Maadili” (ALiVE) Afrika
ya Mashariki, Devotha Mlay baada ya kuwezesha mafunzo kwa wanahabari alieleza
umahususi wa mafunzo hayo.
“Tunafanya
mafunzo haya ili kushirikiana kwa pamoja kuongeza uelewa wa Stadi za Maisha na
Maadili kwa wazazi na wanajamii kupitia vyombo vya Habari, hii inatokana na
matokeo ya Mradi wa ALiVE awamu ya kwanza kubaini uelewa mdogo wa Jamii kuhusu stadi
za maisha, lakini pia Mradi wa ALiVE awamu ya pili unataka vyombo vya Habari vihusike
kuzungumza mada hizi mara kwa mara pasi na kusubiri matukio tu” alisema Devotha
Mlay.
Devotha Mlay (aliyesimama katikati), Meneja mawasiliano na uchechemuzi
wa Mradi ALiVE Afrika Mashariki, akitoa mafunzo kwa wanahabari.
Greyson Mgoi
Meneja wa Mawasiliano na Mratibu wa Mradi wa ALiVE kutoka Shirika la Uwezo
Tanzania pamoja na Jafari Mzamva Afisa Msaidizi Mradi wa ALiVE kutoka Shirika
la Ocode, walikua sehemu ya wawezeshaji wa mafunzo hayo ya wanahabari juu ya kufanya
uchechemuzi na kutumia taaluma zao kutengeneza Jamii yenye uelewa na kuziishi Stadi
za Maisha na maadili.
“Tunawapatia
mafunzo haya wanahabari ili kuwajengea uwezo wa kuyafahamu vyema maswala ya
stadi za Maisha na maadili ili waweze kutumia taaluma zao kuzifikia jamii na
wadau mbalimbali na kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa stadi hizi kwa vijana na Watoto
katika jamii zetu”Alisema Mgoi.
Greyson Mgoi (aliyesimama kushoto), Meneja mawasiliano na mratibu wa Mradi wa ALiVE, shirika la Uwezo Tanzania
akitoa mafunzo kwa wanahabari
Mwandishi wa
Habari kutoka Zanzibar Mohamed Hassan Kabwanga, akiwasilisha kazi ya kundi lililojadili
kueleza wajibu wa wazazi kuhusu Stadi za Maisha, alisema “ni muhimu wazazi kuzitambua
Stadi za Maisha na maadili kisha kuwapa maarifa hayo Watoto kwa ajili ya
kuwajengea stadi zitakazowasaidia katika maisha”
Bwana Mohamed
aliongeza kuwa “mzazi awe kichocheo cha Mtoto kujifunza na kuzitekeleza Stadi
za Maisha”
Mwandishi wa Habari Mohamed
Hassan Kabwanga akiwa katika mafunzo.
Mwandishi wa
Habari mwingine ni Hamad Rashid kutoka Morogoro naye, alieleza walichojadili
katika kundi lililojikita kutazama Taasisi ya Elimu nchini Tanzania, iliyochini
ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
“Taasisi ya
Elimu iweke msisitizo wa kuanzishwa Jumuiya au Klabu za Stadi za Maisha na Maadili
shuleni, ili kutoa nafasi ya watoto kuhamasishana wao kwa wao namna ya kuziishi
Stadi za Maisha na Maadili kwa manufaa yao na kuleta mabadiliko katika Jamii” alisema
Hamad.
Vilevile, ni
muhimu wahusika wanaowafundisha Stadi za Maisha na Maadili watoto na vijana,
wajengewe kwanza uwezo wa kutambua stadi hizo na wathibitike kisha waweze
kuzifundisha kwa watoto, katika maeneo yote ya shule, taasisi za dini na kwenye
makutaniko mbalimbali ya Jamii yanayoshirikisha watoto na vijana, aliongeza
Hamad.
Ofisa kutoka
Shirilika la Milele Zanzibar Foundation Samson John Sitta ambaye ni, Ofisa Mkuu
wa Mradi wa Tathmini ya Stadi za Maisha na Maadili (ALiVE) upande wa Tanzania bara,
alikua sehemu ya wawezeshaji wa mafunzo hayo kwa wanahabari.
Akihojiwa na
Tanzania Kids Time alisema, “mafunzo haya ni muendelezo wa kuongeza kwa
wanahabari juu ya Stadi za Maisha ili wazielewe vyema kisha watumie Taaluma zao
kuifikishia Jamii, vilevile mafunzo haya yalikusudia kuwafahamisha wanahabari
matokeo ya Mradi wa ALiVE awamu ya kwanza na hatua zilizofikiwa hadi sasa”
Katika
hatua nyingine alisema “sisi tunafanya hivi ili kuimarisha mashirikiano na
vyombo vya Habari ili kufanikisha uchechemuzi wa Jamii kuzikumbatia Stadi za
Maisha na Maadili kwa mustakabali wa Taifa”
Samson John Sitta
(aliyesimama katikati), Msimamizi wa Mradi wa ALiVE Tanzania bara, akitoa mafunzo
kwa waandishi wa Habari.
Hata
hivyo waandishi wa Habari na wahariri walioshiriki mafunzo hayo walipata nafasi
ya kuorodhesha na kuzijadili Stadi za Maisha na Maadili zikiwemo: –
Mawasiliano, Ushirikiano, Utatuzi wa matatizo, Kujitambua, Ubunifu na maadili mojawapo ikiwemo Heshima.
MAANA YA STADI ZA MAISHA: –
Stadi
za Maisha zinaweza kutafsiriwa kuwa, ni uwezo mpana ambao unachakatwa na kila
mtu kwa viwango tofauti, vinavyotuwezesha kuishi kwa ujasiri na kujitegemea
katika maisha peke yetu pamoja na kuchochea mabadiliko chanya kwa watu wengine
katika Jamii.