Na Hamad Rashid
Shirika la Milele Zanzibar Foundation limezindua mafunzo ya DI – (Destination Imagination) Boot Camp kwa lengo la kuwaandaa walimu wa Shule za Sekondari kutumia falsafa ya kidunia ya Destination Imagination, kufundishia masomo ya STEAM ambayo ni Sayansi, Teknolojia, Sanaa, Hisabati pamoja na Stadi za karne ya 21 ili kuwasaidia wanafunzi kukuza uwezo wa ubunifu na uvumbuzi katika kutatua matatizo yanayo wakabili.
Mafunzo hayo ya siku tano, yalifunguliwa katika Ukumbi wa Skuli ya Sekondari Tumekuja Iliyopo Mkoa wa Mjini Magharibi ,Unguja na Mgeni Rasmi Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ndugu Khamis Abdallah Said ambaye pia alifikisha ujumbe Serikali kwa walimu na wanafunzi.
“Teknolojia imekuja kuwa karibu nasi, walimu na wanafunzi mliokuja hapa lengo letu uondoke na kitu mwalimu unahitaji kuwa mbunifu, na ninyi watoto someni na katika hili sisi Wizara ya Elimu, Wizara ya Afya, Maji, Umeme na kadhalika tunahusika katika hili, kwa maana kuwaandalia mazingira ya kuja kuwa viongozi katika maeneo hayo ili muongoze Uchumi wetu, kama tunataka uchumi wetu ukue, kama tunataka Nchi yetu iendelee tunaanza na walimu, Elimu ndio jambo la mwanzo, waalimu ni jukumu letu kuwatengeneza Injinia wa baadae, wahandisi, na wataalamu mbalimbali wa baadae” alisema Katibu Mkuu Khamis Abdallah Said
Meneja wa Miradi ya Elimu katika Shirika la Milele, Eshe Haji Ramadhan alizungumza kabla ya Mgeni rasmi katika siku ya kwanza ya mafunzo hayo ya siku tano alieleza kuwa “Pilot program hiyo ya DI- BootCamp, inatekelezwa katika Skuli 15 Unguja na Pemba (Skuli 9 za Unguja na Skuli 6 kutoka Pemba) jumla ya wanafunzi 75 unguja na pemba wamejumuishwa katika program hiyo, inayowahusisha wanafunzi 5 katika kila Skuli, walimu 30 wa masomo ya Sanaa na Sayanzi, walimu wakuu 15 ili kupata usimamizi imara ndani ya skuli hizo na inatarajiwa kutoa athari kwa walimu na wanafunzi wengi zaidi baada ya kutumia ujuzi huo kuwasaidia wengine”
Mkufunzi Mkuu wa Falsafa ya Destination Imagination, Bi, Raya Ahmada katika ufunguzi wa mafunzo hayo alieleza kimahususi miongoni mwa mbinu za kufanikisha Programu hiyo kwa walimu na wanafunzi wa Shule za Sekondari.
“katika eneo la Stadi za Stad za Karne ya 21 ambapo tumechagua Stadi Tano ambazo ni, ushiriikiano, ubunifu, kujitambua, utatuzi wa matatizo na heshima lakini pia katika kile tunachokiita STEAM, tutatilia mkazo masomo ya Sayansi na Teknolojia kwa wanafunzi wa kike ili kuondoa dhana ya masomo ya Sayansi kwamba anayepaswa kuyasoma ni mwanaume pekee” Alisema Raya.
Boot Camp hiyo ya walimu na wanafunzi inatarajiwa kuleta mabadiliko chanya, kama alivyoeleza Mwl. Abbas Mdungi Mohamed wa Shule ya Sekondari Mikindani – Dole, “tunatarajia baada ya mafunzo haya yatatubadilisha hasa katika kuwaandaa vyema wanafunzi, na hatutakubali tushindwe kuwajenga kinadharia na vitendo vijana wet”
MAELEZO MAFUPI KUHUSU DESTINATION IMAGINATION.
“Falsafa ya Destination Imagination” ni dhana inayohusiana na mtindo wa Elimu na maendeleo ya maarifa yanayolenga kuchochea ubunifu, ujasiriamali, na ufumbuzi wa matatizo kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari. Programu hii huwawashirikisha wanafunzi katika timu ambazo zinajitahidi kutatua changamoto na kuonyesha ubunifu wao kwa njia mbalimbali.
Mchakato huwawezesha, wanafunzi kujifunza ujuzi muhimu kama vile, kufanya kazi za vikundi, kutatua matatizo, na kujenga ujasiri katika kujieleza.
Zaidi ya hayo, Falsafa hii inasisitiza umuhimu wa kutoa fursa kwa wanafunzi kutumia akili zao na kuendeleza ufumbuzi wao wa kipekee kwa changamoto za kielimu na kijamii.