Na Hamad Rashid
Shirika lisilo la kiserikali la SAWA lenye makao makuu yake Mkoa wa Morogoro, lilishiriki maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika Mwaka 2024, kwa kutoa msaada wa Bidhaa za vyakula na vifaa vya usafi katika Kituo cha Raya Islamic Orphanage kinacholea Watoto yatima na wanaotoka katika mazingira magumu, kilichopo katika Kijiji cha Lugono, Kata ya Mlali, Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.
Akitoa ujumbe kwa watoto na Jamii, Mkurugenzi wa Shirika la Sawa Bi, Heren Nkarang’ango alikemea upotoshaji wa maadali unaofanywa kwa njia ya mitandao ya kijamii, pamoja na utoaji wa zawadi wenye nia mbaya kwa watoto.
“Sasahivi kuna mgeni ameingia ambaye ni Runinga, Simu na Mitandao ya Kijamii kuna Aplikesheni za ajabu zinazotoa maudhui yasiofaa kwa watoto, watoto msikubali kudanganyika, vilevile msikubali kupokea zawadi kwa mtu usiemfahamu au unayeona ana nia mbaya na wewe, na endapo ikitokea hivyo toeni taarifa kwa wazazi wenu, walimu na viongozi wa Jamii” alisema Bi, Nkarang’ango.
Mkurugenzi wa Kituo cha Raya Islamic Orphanage Bi, Raya Subaha Maganga anaelea watoto 90 katika kituo hiko, alishukuru kwa ajili ya Msaada huo vyakula kutoka Shirika la SAWA.
Raya alisema “Napenda kuwashukuru sana SAWA kwa kuona umuhimu kuja hapa kuadhimisha siku hii muhimu na watoto wetu hapa, mimi na wao tunazungumza Lugha moja, mimi natetea Watoto na wao wanatetea watoto”
Msaada uliotolewa na Shirika la SAWA ni pamoja na Unga wa mahindi Kilogramu 250, Mchele Kilogramu 100, Sukari Kilgramu 50, Mafuta ya kupikia Lita 40, Mfuko mmoja mkubwa wa Sabuni ya Unga ya kufulia, na maduku 10 ya Dawa za kusafishia Chooni vyenye thamani ya Shilingi Laki nane na Kumi za Kitanzania.
Ujumbe wa kaulimbiu ya Siku ya Mtoto wa Afrika mwaka 2024 Nchini Tanzania unasema Elimu jumuishi kwa Watoto, izingatie maarifa, maadili na Stadi za Kazi, huku ujumbe wa Afrika ukisema, Elimu kwa Watoto wote Barani Afrika wakati ni sasa.