Na Hamad Rashid
Katika kuadhimisha siku ya walimu duniani, Kongani ya walimu (Teachers Development Support Cluster), ya Mtandao wa Elimu wa kikanda RELI AFRIKA – Tanzania, imefanya mdahalo uliolenga kusikia sauti na kujifunza kwa walimu waliofanikiwa baada ya kupatiwa mafunzo kazini na wadau mbalimbali wa RELI.
Maadhimisho hayo yaliyofanyika kwa njia ya Mtandano tarehe 11 Oktoba, saa Nne hadi saa Tano Asubuhi, yamehudhuriwa na mashirika mbalimbali, wadau wa RELI pamoja na walimu wa Shule za Msingi na Sekondari kutoka Tanzania Bara na Zanzibar huku Mdahalo wake, ukiongozwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uchechemuzi Shirika la Uwezo Tanzania Greyson Gervas Mgoi, waalimu wakieleza manufaa ya mafunzo ya Mradi wa Jifunze/TaRL (Teaching at the Right Level).
Sauti za walimu katika maadhimisho.
Mwalimu Grace Patrice kutoka Shule ya Sekondari Mloganzila Mkoa wa Pwani akichangia katika mjadala ulioongozwa na swali la kile mwalimu anachokipenda alisema, “Nashukuru sana nimejengewa uwezo na Shirika la PWC kupitia Mradi wa Jifunze/TaRL, mafunzo ambayo yameniwezesha kuwa na urahisi wa kufundisha kwa kutumia zana za kisasa, wanafunzi wananielewa zaidi kuliko mwanzo kabla sijapata mafunzo ya TaRL”
Mwalimu mwingine ni Sarah Komba anayefundisha katika Shule ya Msingi Kilunywa A, iliyopo Wilaya ya Kisarawe Mkoa wa Pwani naye alisema, “nimebadilika sana katika ufundishaji tofauti na mwanzo, kabla sijapata mafunzo ya TaRL, nafurahia zaidi elimu shirikishi niliyofundishwa ambayo imenisaidia kujenga mahusiano baina yangu na wanafunzi na sasa wananielewa kwa urahisi”
Aidha, Mwalimu Sarah baada ya kuanza kutumia mbinu za Jifunze/TaRL, zilimuwezesha kupanda viwango vya ufundishaji akatambuliwa mchango wake kwa kutunukiwa Tuzo ya Mwalimu bora na Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe.
Akijibu swali lililoulizwa na Mratibu wa mdahalo huo, Ndugu Greyson, kuhusu nafasi ya teknolojia katika ufundishaji, Mwalimu Waziri Mdoe kutoka Turini Sekondari iliyoko Mkoa wa Pwani alisema, Ulimwengu wa sasa unalazimu kuwa na zana za kidigitali katika kufundishia wanafunzi, na ni suala ambalo haliepukiki.
Walimu wengine walioshiriki maadhimisho hayo ni, George Ngomba kutoka Leena Pri and primary School ya Mkoani Morogoro na Maryam Khamis Mohamed kutoka Skuli ya Msingi Fuoni iliyoko kisiwani Unguja, Zanzibar.
Sambamba na maadhimisho hayo, Kongani ya Elimu imetaja mafanikio na mambo mengine yanayotarajiwa kufanywa ili kuendelea kuinua Elimu nchini, ikiwemo la kushirikiana na Kongani ya Stadi za Maisha ya RELI kuwajengenea walimu uwezo wa kufundisha, watoto kumudu stadi za kusoma, kufanya hesabu pamoja na stadi za Maisha na maadili.
Mtandao wa elimu wa kikanda unajumuisha zaidi ya mashirika ya Elimu yasiyo ya kiserikali 70 yaliyopo Afrika ya Mashariki.
Ujumbe wa maadhimisho kutoka kwa viongozi.
Akitoa Hotuba ya ufunguzi wa maadhimisho Bi, Faraja Kota Nyalandu aliwataka waalimu kutumia mafunzo waliyoyapata kufundisha na kuyasambaza kwa walimu wengine, na kwamba wanapaswa kuendelea kujifunza ili waendelee kuwasaidia watoto kumudu masomo yao.
Naye, Mkurugenzi wa Shirika la Maarifa ni Ufunguo Nicholaus Etilawe, akielezea uzoefu wake katika suala la matumizi ya viboko darasani, alisema Mwalimu anayetumia viboko mara nyingi huwa hajiamini, vilevile uwezo wake wa kufundisha huwa chini ilhali viboko kwa wanafunzi kuharibu saikolojia yao na kuwasababisha wasiwe na taaluma nzuri.
“Ni vyema Mwalimu utumia zaidi mbinu za kisasa kufundishia badala ya kutumia viboko” aliongeza Nicholaus Etilawe
Awali akiwalisisha utekelezaji na matokeo ya miradi mbalimbali ya Elimu iliyotekelezwa na Shirika la Milele Zanzibar Foundation (MZF), Meneja wa Miradi ya Elimu kutoka MZF Eshe Ramadhan Haji alieleza kwamba, miradi mingi imekuwa na matokeo Chanya kiasi ambacho baadhi ya wadau wa Elimu kuiendeleza katika maeneo yao ya kazi.
Viongozi wa Kongani ya Elimu ya RELI ni, Bi, Faraja Kota Nyalandu Mkurugenzi wa Shirika la Shule Direct na Bwana Greyson Gervas Mgoi Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uchechemuzi Shirika la Uwezo Tanzania.
Mashirika wadau wa RELI Afrika yaliyoshiriki maadhimishimo hay oni pamoja na Uwezo Tanzania, Milele Zanzibar Foundation, OCODE, SAWA Wanawake Tanzania, SHULE DIRECT, SAZAN Trust, PWC, Chuo cha ST JOHNS na RELI Tanzania.
Siku ya walimu duniani huadhimishwa Oktoka 5 kila mwaka, kutambua mchango wao katika Jamii, Taifa na Ulimwengu mzima, siku hii iliasisiwa mwaka 1966 na Shirika la kazi duniani (ILO) pamoja na Shirika la umoja wa mataifa la Elimu na Sayansi, (UNESCO).