Na Hamad Rashid.
Awamu ya pili ya Mradi wa ALiVE (Action for Life Skills and Values), unaotekelezwa chini ya Mtandao wa Elimu wa Kikanda (RELI-Africa), kupitia Kongani ya Stadi za Maisha na Maadili (VaLi), Umeleta mafanikio makubwa hasa katika kutengeneza wazazi vinara wanaoielimisha jamii katika kuzilea na kuzikuza stadi za maisha na maadili katika Wilaya sita nchini,Tanzania bara na Zanzibar. Utekelezaji wa jitihada ya kukuza stadi za maisha na maadili kwa watoto na vijana umefanyika kwa kipindi cha Miezi mitatu (Oktoba, Novemba na Disemba) mwaka wa 2024.
Kwa mujibu wa Meneja wa kikanda Mradi wa ALiVE, Devotha Mlay kwa sasa ulimwengu ili mtu afanikiwe haitegemei taaluma pekee bali fikra tunduizi na maarifa ya stadi za karne za 21 jambo ambalo, ni muhimu zaidi kwa watoto na vijana kwa ajili ya maisha yao.
Mlay alisema “Ukiangalia zama zimebadilika sana,hapo zamani kidogo utakuta kwamba, kazi nyingi zilikuwa zinawatu wachache wachache na wala haikuhitaji sana kuwa na ubunifu na utaweza kuamini kwamba, kwa mfano, fundi selemara, anaweza kutengeneza Kiti kizuri sana lakini, kama hana uwezo wa kuzungumza na wateja wake vizuri, kuwakaribisha wateja wake vizuri, kusikiliza kile wanachokita na kuendana na mazingira ya wateja wake wanavyotaka, ufundi Selemara unaweza usimsaidie kufanikiwa sana katika kazi yake na hicho ndio tunachokiongelea. Hapo nyuma kidogo wazazi, wamejikita sana katika kuangalia masomo gani yanafundishwa na watoto wanapata ufaulu wa alama A, lakini kuna zaidi ya alama A, kwahivyo mzazi akafahamu stadi hizi ni za aina gani? Lakini je zinamsaidiaje kijana? Lakini pia akaweza kuwa sehemu moja ya watu ambao wanamsaidi, kijana huyu kuweza kupata stadi hizi, anapokuwa nyumbani”
Nchini Tanzania Shirika la Uwezo Tanzania ndio lililopewa jukumu la kusimamia utekelezaji wa programu ya mashirikisho ya wazazi katika maeno yote ya Tanzania Bara na Zanzibar, ikiwa Mradi huo unatekelezwa katika Nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.
“Katika kuwasaidia vijana waweze kumudu eneo la stadi za maisha na maadili, Uwezo Tanzania tumetengeneza mpango mkakati wetu, wa miaka miatano kwanzia 2024 hadi 2028 na katika mpango mkakati huu, tumeweka karibu 20% hadi 30%, za kuwekeza kwenye malezi na makuzi ya watoto”. Alieleza Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Uwezo Tanzania, Baraka Mgohamwende katika mahojiano na Tanzania Kids Time.
Kwa mujibu wa Afisa mwandamizi wa Mradi wa ALiVE, Samson John Sitta akizungumza akiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro aliposhiriki mafunzo ya wazazi vinara wa stadi za maisha na maadili, miongoni mwa malengo ya programu ya majaribio ya Mradi wa ALiVE yalikuwa kuratibu mashirikisho ya wazazi waweze kuzilea na kuziishi Stadi za maisha na maadili, na kuendesha Kampeni ya stadi za maisha na maadili katika Jamii na kutengeneza wazazi vinara 300 katika Wilaya 6 za Tanzania, mambo ambayo yamefanikiwa kwa zaidi ya asilimia 100.
Hatahivyo, Wilaya zilizoshiriki katika majaribio ya mradi wa ALIVE awamu ya pili ni, Morogoro na Mvomero zilizoko katika Mkoa wa Morogoro, Bagamoyo iliyoko Mkoa wa Pwani, Kaskazini A, Mjini Magharibi na Kusini chini ya utekelezaji wa mashirika ya, GLAMI, OCODE, SAWA, Sazani Trust na Milele Zanzibar Foundation.
Kila Wilaya ilitengeneza Vinara 50 walipataikana kutokana na vikao vya mashirikisho ya wazazi, ambapo kila kinara alikuwa na jukumu la kuifikia jamii yake kutoa elimu ya stadi za maisha, ambapo katika programu hiyo walimu, wanafunzi, vijana, viongozi wa Dini na Serikali walihusishwa.
“Mwanzoni wakati tunaanza hivi vikao wazazi walikuwa na uelewa mdogo sana, juu ya stadi za Maisha lakini baada ya kupata mafunzo wakapata muda wa kujadili, na kuwasilisha mwishoni wameonekana angalau kuanza kupata upeo, na wameonesha utayari wao wa kuweza kutoa stadi za Maisha, na maadili kwa vijana pamoja na watoto”, aliesema Deborah Ijiko Afisa ustawi kutoka Shirika la GLAMI baada ya kumaliza kikao na wazazi katika Shule ya Sekondari Ngerengere.
“Tunachokifanya kwanza ni kuwajengea uwezo wale vinara, ambao wapo katika shehia, kuona wao wanauelewa gani wa hizi stadi za Maisha ili na sisi tuweze kuwasaidia kwa namna gani, kuna changamoto moja kwamba, walimu na wazazi wanachanganya baina ya stadi za Maisha na stadi za kazi lakini tulipofikia ni pazuri sasa wanaelewa” aliongeza Safia Mkubwa Abdalla Mkurugenzi wa Shirika la Sazani Trust, Zanzibar.
Wazazi vinara wa stadi za maisha na maadili ni watu gani na hufanya nini?
Kulingana na asili ya awamu ya pili ya ALiVE vinara ni, wazazi waliopewa mafunzo ya kuzitambua, kuzikuza, kuziishi na kuweza kujitolea kuzifundisha stadi hizo, katika jamii yao katika njia mbalimbali kulingana na mazingira yao ikiwemo vikao vya kijamii na kufanya vipindi vya elimu katika Redio na Runinga.
Vinara baada ya utekelezaji wa uelimishai jamii stadi za maisha.
Mwanahamisi Thabiti ni mzazi kinara wa satadi za maisha na maadili, kutoka Kata ya Mkuyuni, Wilaya ya Morogoro, katika mahojiano na Tanzania Kids Time alielezea kufanikiwa katika kuiunganisha jamii kuwa na mahusiano mazuri yanayowahusisha watoto.
“Hapo zamani mahusiano na mashirikiano baina ya mtoto na mzazi yalikuwa magumu, tulikuwa hatuwasikilizi watoto, kwenye Jamii mtoto akikwambia jambo unaweza ukamfokea bila kumfundisha, lakini sasahivi tunawaona majirani namna tunavyoishi nao, hata mtoto akirejea nyumbani mzazi anamkaribisha, anamuuliza vizuri na kama anachangamoto anaongea nae, hadi wanapata muafaka uliokuwa sahihi, kwakwel tumefanikiwa” alihitimisha Mwanahamisi Thabiti.
Mwalimu Abasi Omari Lipongola kutoka Shule ya Sekondari Mkuyuni iliyopo Wilaya ya Morogoro naye alieleza, “kwenye dhana ya mawasiliano na ushirikiano, kwakweli kuna matokeo chanya makubwa, watoto wamebadilika kifikra na kuna mawasiliano mazuri baina ya sisi walimu na wao, lakini pia baina ya watoto na wazazi wao na hiyo imewafanya wazazi waweze kufuatilia kwa ukaribu zaidi, maendeelo ya masomo ya watoto wao, lakini pia tumepata mrejesho kutoka kwa wazazi katika namna ambavyo watoto wanavyo husiana na wazazi wanapokuwa nyumbani”
Mzazi kinara mwingine ni Suleiman Khamis Sheha kutoka Shehia ya Tumbatu Gomani iliyoko Wilaya ya Kaskazini A, Zanzibar, alishuhudia kuwa “hapo mwanzo kulikuwa na baadhi ya vijana wamejitokeza kuvaa nguo juu ya magoti huku kwetu tunaita mafuti, baadhi yao tayari wameanza kubadilika kwa kiasi Fulani, na katika sehemu za maskani zao wanapokaa, baadhi ya vijana wameanza kujishughulisha na kazi nyingine za binafsi kwa mfano, wanajihusisha na kuchimba mashimo ya vyoo au Karo za majumbani, lakini wengine wanajihusisha na kazi za Uvuvi na baadhi ya mambo mengine”
Mafanikio ya Mradi wa ALiVE Tanzania.
Miongoni mwa mafanikio ya Mradi wa ALiVE tangu ulipoanza katika awamu yake ya kwanza Mwaka 2020, ni kutengeneza uchechemuzi uliosaidia Serikali ya Tanzania kuingiza stadi za maisha katika maboresho ya Mtaala mpya wa Elimu. Baadhi ya stadi za maisha zilizojumuishwa ni pamoja na Kujitambua, Utatuzi wa matatizo, na Ushirikiano.
Aidha upande wa Zanzibar Serikali imeanza mchakato wa kuandaa muundo wa kazi wa stadi za maisha (Zanzibar Life Skills Framework), lakini pia kufanikiwa kuanzishwa kitengo cha Stadi za maisha na maadili katika Taasisi ya Elimu Zanzibar iliyoko chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali.
Akizungumzia matokeo ya programu ya mashirikisho ya wazazi kuhusu stadi za maisha Mkurugenzi wa mawasiliano na uchechemuzi Shirika la Uwezo Tanzania, Greyson Mgoi alieleza kuwa ni mazuri na yamekuwa na mustakabali chanya kwa Taifa la leo na kesho.
“Kupitia jitihada hii tumefanikiwa kwenda katika Wilaya ya sita ambapo, Wilaya tatu zipo Tanzania bara na tatu za Zanzibar tumekuwa tukihamasisha wazazi na walimu kusaidia watoto kukuza stadi za maisha na maadili na matokeo ni mazuri, tunaona wazazi wamepokea vizuri sana uhamasishaji huu, tumeona wazazi wamekuwa mstari wa mbele sana, hivyo tunaimani kwamba wazazi kwa kushirikiana na walimu watasaidia kukuza stadi hizi za maisha, kwa watoto wao na miaka kadhaa baadae tutaweza kuwa na vijana wenye viwango vya juu kabisa vya stadi za maisha na maadili” alisema Greyson.
Stadi za maisha na sifa zake.
Stadi za maisha ni mahiri wezeshi zinazomsaidia mtu kuweza kukabiliana na hali mbalimbali ya maisha yake kila siku kulingana na mazingira anayokuwepo popote pale, mfano kuwa na stadi ya utatuzi wa matatizo mawasiliano, kujiamini, ushirikiano na kujitambua.
Kulingana na wataalamu wa stadi za maisha, moja ya sifa za stadi za maisha, mtu huzaliwa nazo, suala ambalo mzazi ana nafasi kubwa ya kumsadia mtoto kukuza stadi za maisha. Sifa nyingine, Stadi sio sawa na Maarifa.
Baadhi ya wazazi wakipata mafunzo ya stadi za maisha na maadili katika Shehia ya Mkokotoni, Wilaya ya Kaskazini A, Unguja – Zanzibar wanaonekana katika picha hapo chini.