Na Hamad Rashid.
Shirika la Sawa Wanawake Tanzania lenye makao makuu yake Mkoani Morogoro, ni miongoni mwa mashirika wadau wanaotekeleza awamu ya pili ya Mradi wa ALiVE (Action for Life Skills and Values), unaojihusisha na kukuza stadi za maisha na maadili kwa watoto na vijana, limewaleta pamoja wazazi 394 katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Mvomero, kisha kuwawezesha kuzielewa na kuziishi stadi za maisha ili kuandaa watoto wao vyema waweze kujifunza mashuleni na kukabiliana na changamoto katika maisha.
Kulingana na asili ya Mradi huo, unaotekelezwa chini ya Mtandao wa Elimu wa Kikanda (RELI-Africa), kupitia Kongani ya Stadi za Maisha na Maadili (VaLi), katika Nchi za Tanzania Kenya na Uganda, katika utekelezaji wake Shirika la SAWA lilifanikiwa kutengeneza wazazi vinara 50 baada ya kufanya vikao saba katika vijiji vya Ndama, Mela, Makuture, Msasani, Vianzi, Matangani na Dakawa.
Hatahivyo, jumla ya wanawake 271 na wanaume 123, ambao kwa kiasi kikubwa wengi wao, ilikuwa mara yao ya kwanza kusikia kuhusu stadi za maisha na maadili, Afisa Ubora katika Elimu Shirika la SAWA Mahmudi Ngamange akizungumza na Tanzania Kids Time alisema, “Mradi huu wa Stadi za maisha na maadili, umeongeza kitu muhimu sana katika jitihata ambazo Shirika la SAWA limekuwa likitekeleza. Tumeshuhudia uelewa wa hali ya juu kuhusu stadi zamaisha, walioonesha wazazi, na hii itasidia mtoto kwenda shule akiwa na utambuzi wa stadi za maisha ili aweze kujifunza vizuri, kwa maana mtoto akikosa stadi za maisha ujifunzaji wake unakuwa mgumu”
‘Tumefurahishwa na mbinu iliyotumika katika Mradi, katika kuwashirikisha wazazi kuzilea stadi za maisha suala ambalo limejenga ushirikiano kati ya wazazi na watoto na kuanza kujitambua kwa watoto pindi wawapo nyumbani” aliongeza Afisa huyo anaesimamia Mradi wa ALiVE katika SAWA.
Mwanahawa Jeremia ni Mama lishe katika kijiji cha Vianzi Kata ya Vianzi, Wilaya ya Mvomero, yeye ni zao la Mzazi Kinara, Wilbroad Benard aliyepokea mafunzo ya stadi za maisha kutoka Shirika la SAWA kisha kuendeleza utoaji elimu katika jamii yake, katika mahojiano na Mwanahawa alieleza mabadiliko chanya ya yeye kufundishwa stadi za maisha.
“Nilipopewa elimu ya stadi za maisha, imenibadilisha, nimeanza kuweka ratiba ya kuwafundisha watoto wangu masomo ya ziada mwenyewe pindi wanaporudi Shule, vilevile nimembadilisha na mume wangu, nay eye sasahivi watoto wakitoka Shule anawafundisha masomo ya ziada (Tuition) na kuzungumza nao kuhusu Stadi za Maisha” alieleza Mwanahawa.
Mwanahawa aliongeza, “Suala hili limeanza kukuza taaluma ya watoto wangu shuleni kwa mfano, nina kijana aliyemaliza Darasa la sita atajiunga na Darasa la saba mwaka huu 2025 alikuwa anashika nafasi ya mwisho katika mtihani, lakini sasahivi amekuwa anajishughulisha vizuri katika masomo ya ziada, kwa hivyo, nashukuru sana ujio wa Mradi huu wa masuala ya stadi za maisha na maadili”
Katika kikao cha kuwasilisha mirejesho ya hatua za utekelezaji wa Mradi wa ALiVE na mashirika wadau, Mkutano uliofanyika mwishoni mwa mwezi Disemba 2024 Mjini Morogoro, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uchechemuzi katika Shirika la Uwezo Tanzania Greyson Mgoi alisema, “tunawaangalia sana wazazi katika jukumu letu la kufanya uchechemuzi wa kuziela stadi za maisha na maadili, kwa maana tafiti zinaonesha, watu wenye umri mkubwa wanauwezo mkubwa wa mahiri za stadi za maisha na maadili ukilinganisha na wale wenye umri mdogo, tuliamua kuwatumia wazazi, kwanza ili kuelewa utambuzi wao, kuwajengea na kisha kuwahimiza waweze kuzikuza stadi hizi ka jamii”.
Katika kikao hicho pia, Afisa Ustawi wa Jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Joseph Medard alisema, “tumeweza kushuhudia mabadiliko chanya ya watoto pamoja na wazazi namna walivyoweza kuhusishwa katika kufahamu njia sahihi za kuziishi satadi za maisha na maadili, suala hili tumeona limeleta mabadiliko chanya ya kifikra juu ya namna ya kukabiliana na utatuzi wa matatizo na hata ushirikiano kwa watoto wenyewe lakini pia wazazi na watoto”.
Namna Takwimu zinavyoonesha umuhimu wa stadi za maisha.
Kwa mujibu wa report ya maendeleo ya elimu ya Tanzania ya mwaka 2022 katika kipengele cha “Soko la Ajira” waajiriwa 6 kati ya kumi (sawa asilimia 61) ni wahitimu wa shule ya Msingi na muajiriwa mmoja kati ya kumi (sawa na asilimia 1.3 tu) ni wale waliohitimu Elimu ya Chuo kikuu, ambao walioekana kukosa stadi hizo muhimu na kupeleka kutopata ajira.
Vilevile, ripoti ya utafiti wa jumuiya ya vyuo vikuu vya Afrika Mashariki ya mwaka 2015, inaonesha, wahitimu wengi wa vyuo vikuu wanastadi za ujuzi mbalimbali lakini, hawana satdi zinazowawesha kutumia juzi hizo katika maeneo ya kazi.
Tafiti hii inaonyesha kwamba waajiri walisema wahitimu wa chuo wanakosa stadi kama vile Mawasiliano, Kujitambua, utatuzi wa Matatizo na Fikra Tunduizi hivyo, walishindwa kuwaajiri katika nafasi mbalimbali.
Meneja wa mradi wa ALiVE Zanzibar na mshauri wa kiufundi upande wa Tanzania Bara, Ramadhani Matimbwa akizungumzia umuhimu wa mzazi katika malezi ya mtoto alisema, “Sisi kama watengenezaji wa mradi huu wa ALiVE (Action for lifeskills and values), tunashauri sana wazazi wachukue nafasi yao, mzazi jihusishe, mzazi shughulika na mwanao, mzazi mshike mkono mwanao, kwa hivyo wazazi wawatoe watoto wawaunganishe kwa pamoja waweze kucheza, lakini michezo ambayo inawafanya waweze kutumia akiili kidogo, kucheza na vitu ambavyo vinaweza kuwafanya kubuni mbinu mbalimbali”.
Kuhusu stadi za maisha.
Kulingana na wataalamu wa stadi za maisha, Stadi za maisha ni mahiri wezeshi zinazomsaidia mtu kuweza kukabiliana na hali mbalimbali ya maisha yake kila siku kulingana na mazingira anayokuwepo popote pale, au inaweza kuwa ni maarifa, ujuzi, mitazamo au mbinu ambazo anaweza kutumia mtu ili kukabiliana au kutatua changamoto mbalimbali katika mazingira yanayomzunguka.
Mfano wa stadi za maisha ni kama, ubunifu, utatuzi wa matatizo, mawasiliano, kujiamini, ushirikiano, kujitambua na fikra tunduizi (kufikiri kwa kina).
“Tunafurahi kuwa sehemu ya watekelezaji wa mradi huu wa ALiVE, sisi kama SAWA vilevile tuliwekeza nguvu Zaidi katika kuwaelimisha wazazi am,bao kiukweli ndio msingi muhimu wa mtoto kuwa na stadi za maisha na maadili, na tumetekeleza mradi huu kwasababu SAWA ni wanachama wa mtandao wa elimu wa kikanda Afrika mashariki (RELI – Africa), kwa hivyo tunatekeleza mradi huu kwa usimamizi wa Shirika la Uwezo Tanzania” alieleza Mratibu wa Shirika la SAWA, Evarist Momburi alipohojiwa Ofisini.
Shukuru Wales ni mzazi kinara katika kijiji cha Vianzi, Kata ya Vianzi, Wilaya ya Mvomero, alikotoa mafunzo kwa waumini 34 kanisani, kuhusu stadi za maisha na maadili.
“Niliwaelezea maana ya stadi za maisha, walifurahi Zaidi kusikia mafunzo hayo, kiasi kwamba walio wengi waliniambia niendelee kutembelea maeneo mengi, pia walisema mafunzo haya yametugusa sana, maana tumekuwa na maisha magumu kwa sababu ya kukosa stadi za maisha na maadili, hata watoto wetu wanaangamia kwa sababu ya kukosa stadi za maisha na maadili, sasa tumebadilika na tunaamini watoto wetu watabadilika kwa kuapata elimu ya stadi za maisha na maadili” alisema kinara Shukuru Wales.
Vilevile, baada ya utekelezaji wa Mradi huu wa Stadi za Maisha Halmashauri ya Mvomero, Stadi za Maisha zinazungumzwa kila mahali kwenye mikusayiko ya watu kama vile makazini, mashambani, kwenye familia, kwenye vikoba, maeneo ya ibada, na popote ambapo vinara wa stadi za maisha wanakutana na watu.