
Na Hamad Rashid
Shirika la Sawa kutoka Mkoa wa Morogoro limeeleza mapendekezo ya Mradi wa Sauti zetu unaohechemua utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa Elimu jumuishi, ili Wadau na Serikali waweze kuchangia kuleta mabadiliko.
Afisa ubora wa Elimu kutoka Shirika la SAWA Mahmudi Ngamange, baada ya kuwasilisha utekelezaji wa Mradi wa Sauti zetu Wilaya ya Mvomero katika kikao cha pamoja na waandishi wa Habari kilichofanyika Mkoa wa Morogoro, aliiambia Tanzania Kids Time miongoni mwa mapendekezo ya mradi huo unaotekelezwa kwa kushirikiana na Shirika la HakiElimu na mashirika mengine matano yasiyo ya kiserikali.
“Ili kuondokana na changamoto zilizopo katika wanafunzi wenye mahitaji maalumu ndani na kuendeleza elimu jumuishi kwa watoto wote Tanzania, tunapendekeza Kuimarisha Usambazaji wa Sera, Uwekeza katika Kampeni za Uhamasishaji, Kuboresha Mafunzo ya Walimu, Kuongeza Fedha kwa Elimu Jumuishi, Wekeza katika Miundombinu Inayoweza Kupatikana, Kuimarisha Tathmini na Mchakato wa Utambulisho, Maboresho katika Njia za Ufadhili na Kufuatilia na kutathmini maendeleo” alisema Ngamange.

Aidha uzoefu kutoka kwa mtafiti wa mradi wa Sauti Zetu, Neema Elias bado eneo la elimu jumuishi linahitaji kutiliwa mkazo wa utekelezaji wa mkakati yake.
Neema Elias alisema “tulifanya utafiti kwa kufanya mahojiano na kikundi cha kuzingatia (focus group discussion), tukishikisha wazazi na watoto vilevile tuliwafuata na kuwauliza walimu moja kwa moja, kiukweli kuna watoto wengi wenye mahitaji maalumu ambao wanahitaji kuwekewa misingi mizuri ya kupata elimu, kwa mfano kuna mtoto mmoja mwenye ualbino tulimuhoji akasema huwa haoni vizuri nyakati za mchana kwa sababu miwani yake imepotea, kwahivyo anaendelea kupata elimu huku akikabiliwa na changamoto ya kuona kwa shida”

Mradi wa Sauti Zetu na mashirikiano ya kimataifa katika Elimu
Mradi wa Sauti Zetu una uhusiano mkubwa na lengo la pili la ushirikiano wa Kimataifa wa Kielimu (Global Partnership for Education – GPE), lengo hili linalenga kuongeza usawa katika upatikanaji wa elimu bora kwa waliotengwa zaidi.
Kwa kulifanyia kazi lengo hili, mpango huo unachangia dhamira ya Tanzania ya kutoa elimu ambayo haimuachi mtu yeyote nyuma.
Kwa mujibu wa Mahmudi Ngamange mradi wa Sauti Zetu unalenga kukuza uwazi, mwitikio na uwajibikaji kutoka serikalini na Taasisi zake kama Shule, Serikali za mitaa, wadau wa elimu na wabunge.
Mkuu wa shule ya Sekondari Wami, Noel Mkopi akihojiwa na waandishi wa Habari baada ya kikao alisema kwamba, pamoja na changamoto zilizopo, wanajitahidi kukabiliana na mazingira yaliyopo ya kufundisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
Noel Mkopi alisema “shuleni kwangu ninao wanafunzi wenye mahitaji maalumu ambao wana uoni hafifu na wale wanaosikia kwa shida, huwa tunajitahidi kuwaweka katika viti vya mbele ya Darasa wakati wa kujifunza, ili Mwalimu anapofundisha waweze kuona kwa urahisi, kitaaluma wanajitahidi japo sio sana ukilinganisha wale wasio na changamoto, lakini changamoto bado ni nyingi katika eneo la miundombinu hasa vifaa vya kuwasaidia ili waweze kusoma na kujifunza bila changamoto”
Mradi wa Sauti zetu ulianza kutekelezwa mwaka 2021 na utahitimishwa mwaka 2026, ukienda sambamba na utekelezaji wa mkakati wa Taifa wa Elimu Jumuishi wa mwaka 2021/ 2022 hadi 2025/2026.
Hata hivyo, Mradi wa sauti zetu unatoa wito kwa waandishi wa Habari kutoa Habari zinazohusu utekelezaji wa mradi huo ili kuleta uchechemuzi wa pamoja katika Sera na Sheria kuhusu mazingira yote ya Elimu jumuishi.