BABA IPENDE FAMILIA ni kampeni yenye lengo la kuwahamasisha akina baba kuzipenda familia zao na kujitoa kuzisaidia na kushiriki katika malezi ya watoto ili kupunguza na kutokomeza kabisa ukatili unaofanywa kwa watoto na akina mama ndani ya familia. Ukatili huu umekuwa ukiendelea kwa miaka mingi na unawaathiri watoto na akina mama kwa kiasi kikubwa hatimaye wameshindwa kufikia malengo yao ya kimaisha na wangi wao wameshindwa kusoma na kubaki kuwa watoto wa mitaani.
Kampeni hii inaendeshwa na shirika lisilo la kiserikali linalotambulika kama Morogoro Organization for Women, Elders and Children Support (MOWECS) linalojishughulisha na kuwasaidia na kuwainua wanawake, wazee na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, lenye makazi yake katika mkoa wa Morogoro. Kampeni hii itakuwa mahususi kwa kata ya Mkundi, Lukobe na Chamwino kwa kuanzia, hatimaye Morogoro yote na mikoa mingine ya Tanzania.
Kampeni hii imezinduliwa tarehe 1.12.2019 na itaendeshwa kwa muda wa miezi mitatu kwa awamu ya kwanza hadi kufikia tarehe 1.3.2020, na kata tajwa zitakuwa zimefikiwa na kupata elimu juu ya ukatili wa watoto na wakinamama unaofanywa na wakinababa. Kampeni hii ni sehemu ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa ‘INUA MTOTO’ unaoendeshwa na shirika la MOWECS, lengo la mradi huu ni kuwasaidia watoto kupata unafuu wa maisha kwa kuwawezesha kupata mahitaji muhimu kama vile mahitaji ya kiafya, elimu, chakula, mavazi na malazi ambavyo ni muhimu sana kwa ukuaji na maendeleo yao kama Taifa la kesho. Sambamba na hilo kuwapa elimu wazazi na walezi wa watoto hao ili waweze kuwahudumia vizuri na kuwapatia mahitaji muhimu yanayotakiwa katika makuzi ya watoto pamoja na haki zao za msingi.
Tatizo la Ukatili kwa Watoto na wakinamama:
Tatizo la ukatili kwa watoto na wakinamama limekuwa tatizo sugu na endelevu nchini, wanawake na watoto katika familia wameonekana ni wahanga wakubwa. Kulingana na tafiti nyingi zilizofanywa inaonesha ongezeko la matukio ya ukatili baina ya watoto na wanawake, ambapo wanawake wameonekana kuwa waathirika wakubwa katika matukio haya na madhara makubwa sana yakiwapata watoto. Vyombo vya habari pamoja na mashirika ya kiserikali na binafsi yamefanya tafiti kuhusiana na ukatili kwa watoto na wakinamama hasa ukatili wa kinjinsia, ripoti zimeonesha ongezeko la ukatili ni kubwa hivyo serikali na jamii yapaswa kulikemea sana jambo hili.
Ripoti ya utafiti kuhusu hali ya watu na afya ya mwaka 2015/2016 uliofanywa na Taasisi ya Takwimu Tanzania imeonesha ongezeko la ukatili dhidi ya wanandoa na wapenzi kutoka asilimia 10 mwaka 2010 mpaka asilimia 14 mwaka 2015/2016, ikiwa asilimia 50 walifanyiwa ukatili na waume zao, asilimia 39 ni ukatili wa kimwili, asilimia 14 ukatili wa kingono na asilimia 36 ukatili wa kisaikolojia. Hata hivyo ukatili baina ya wanandoa umeonekana kusababisha athari kubwa kwa wanawake, ikiwemo asilimia 80 ya waliofanyiwa ukatili wamepata majeraha makubwa na wenginge kupata ulemavu wa kudumu kama vile kuvunjika mifupa, meno na vidole.
Ongezeko limekuwa kubwa ukilingana na tafiti iliyofanywa na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF) kuanzia Januari mpaka Oktoba 2018 ilibaini kuwa asilimia 21 ya vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake vilivyoripotiwa kwenye magazeti ya hapa nchini ni ukatili baina ya wanandoa na wapenzi, pia Gazeti la Mtanzania toleo namba 8930 la tarehe 3 Juni 2018 limeonesha kuongezeka kwa vitendo vya ukatili baina ya wanandoa na wapenzi kufikia 341 kati ya Juni 2016 na Mei 2018. Kulingana na ripoti hizi inaonekana ukatili dhidi ya wanawake imeongezeka kwa katika miaka ya karibuni.
Ripoti ya Dunia ya Maendeleo ya Binadamu ya mwaka 2018 juu ya ukatili dhidi ya watoto (2017) ndiyo iliibua hisia kali kwetu kama shirika na kuona jambo hili kama lisipochukuliwa hatua za haraka kuliondoa linaweza kuwa ni janga kubwa baadaye. Kwa mujibu wa ripoti hiyo inaonesha kuwa takribani mmoja kati ya wavulana saba amekutana na ukatili wa kingono kabla ya kutimiza miaka 18, na kati yao 71% wamekutana na ukatili wa kimwili, na kwa upande wa watoto wa kike, idadi ipo juu zaidi kwa mmoja kati ya watatu na asilimia 72. Na darubini ya kimaendeleo ilionyesha kuwa kufikia mwaka 2025 karibia asilimia 98 ya watoto wote watakuwa wakilelewa na mzazi mmoja yaani mama kwa sababu kadhaa ambazo zitafanya wakose huduma kwa mzazi mmoja ikiwemo na ukatili wa kingono, ugomvi wa familia, kushindwa kuwajibika na ndoa zisizotarajiwa.
Shirika la Mowecs linaangazia ukatili wa Mwanamke kama ndio chimbuko la ukatili unafuata baadaye ambao ni ukatili kwa mtoto. Malezi ya watoto katika jamii nyingi hufanywa na wazazi wawili baba na mama, ikiwa wazazi hao hawapo katika hali ya usawa ni wazi sana kwamba watoto huathirika na mitafaruku ya wazazi. Athari hizo zinaweza kuwa kukosa huduma za msingi, kuishi na mzazi mmoja, kutengwa hata maranyingine kufiwa na mzazi mmoja au wote kwa pamoja, na kwa sababu hiyo mtoto anakuwa anafanyiwa ukatili ingawa ilikuwa si moja kwa moja.
kweli baba ipende familia