Jamii imetakiwa kuondoa migogoro na kutokomeza unyanyasaji na ukatili dhidi ya watoto ili kujenga kizazi bora kwa kuwafundisha maadili mema yanayompendeza Mungu na wanadamu.
Hayo yamebainishwa na Kiongozi wa Kaya na Familia wa Kanisa la Waadventista Wasabato Mafiga, Manispaa ya Morogoro Bwana Asheri Mgonya katika ibada ya kuhitimisha mafundisho ya siku saba ya Kaya na Familia. Yaliyolenga kuzikumbusha familia kuishi kwa Upendo na kuhakikisha hakuna unyanyasaji wa aina yoyote katika nyumba zao na kuepuka vurugu zisizotakiwa.
“mara nyingi unyanyasaji wa nyumbani unaanzia kwenye vitisho na maneno maneno, hatimye vurugu na ugomvi, uhusiano wenye unyanyasaji kimhemuko unaweza kuharibu ile hali ya kujiamini kwa mtu na kusababisha wasiwasi na msongo, kisha kumfanya yule mhanga kujiona hana msaada kabisa” alisema
Aidha alieleza kuwa, vurugu za nyumbani na unyanyasaji ni pamoja na jitihada zozote za mtu mmoja katika uhusiano wa karibu au katika ndoa kuwa na amri juu ya mwengine na kumdhibiti, awe ni mwenzi, mtoto au hata mzazi.
Mgonya alisema, Unyanyasaji unatokea ndani ya makundi yote ya umri, kabila, chimbuko, kiwango cha uchumi, hata katika shirikisho lolote la kidini ikiwa mara nyingi wanawake ndiyo wahanga wakubwa ingawaje wanaume nao wananyanyaswa.
John Zereman ni Kiongozi wa Kanisa hilo, alisema ni umuhimu kuwepo kwa mafundisho ya Kaya na Familia na kuwa endelevu ili kujifuza namna ya kuishi katika ndoa, kuchukuliana na kuondoa mogogoro ambayo huwaathiri watoto na Familia kwa ujumla.
“Familia zinapatakiwa kuishi kwa umoja na kufichua wale wanaofanya ukatili na kuwanyanyasa watoto au mtu yoyote ili sheria ichukue mkondo wake” alisema
Kwa upande wake Afisa maendeleo ya Jamii kutoka Taasisi ya My Health Foundation iliypo mkoani Morogoro alisema kuwa unyanyasaji unapokomaa katika familia huibua ukatili zdhidi ya watoto hivyo amewataka viongozi wa serikali za mtaa
“Balozi, wajumbe wa mitaa, Mwenye kiti wa kijiji na Viongozi wa dini wanatakiwa kuweka utaratibu wa kuzifuatilia familia zilizopo katika maeneo yao ili kujua changamoto zilizopo za kiunyanyasaji, ukatili, migogoro na masuala mengine” alisema
Hata hivyo Mjumbe wa Mtaa wa Tubuyu, Manispaa ya Morogoro Halima Mhando alisema kuwa utaratibu wao ni kusuruhisha migogoro inapotokea kataika familia pindi wanapopata taarifa kutoka kwenye jamii inayowazunguka.
“tunapopata taarifa za migogoro ya familia tunawaita wahusika na kuwasuruhisha, endapo serikali ya mtaa itashindwa, kesi hiyo inapelekwa ofisi ya Kata na baadae inaweza kufika Polisi au Mahakamani kwa mujibu wa Sheria”. Alisema Halima Mhando.
Na; SHUA NDEREKA Morogoro