Mahakama kuu Kanda ya
Morogoro imewafikiwa wananchi zaidi ya Elfu Therathini kuwapatia Elimu na
ushauri wa kisheria sambamba na kujibu changamoto zao mbalimbali za kisheria
ndani ya siku saba za maadhimisho ya wiki ya Sheria.
Mafanikio hayo ya
Mahakama yalielezwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu Kanda ya Morogoro, Paul
Joel Ngwembe Februari 02, 2022, katika maadhimisho ya Siku ya Sheria yaliyofanyika
katika viwanja vya Kituo cha haki jumuishi Kihonda, wakati akieleza kazi
zilizofanywa na Mahakama katika kipindi cha Wiki ya Sheria akitaja maeneo
waliyofika na kutoa Elimu, na kwamba wananchi watambue juhudi za hizo ni kwa
ajili yao, kwasababu katika maisha ya Binadamu Sheria haikwepeki.
Jaji Ngwembe pia alizungumzia
maendeleo ya Teknolojia namna ilivyo na kasi, ikileta manufaa makubwa pamoja na
athari ikiwemo Ugonjwa wa Uviko 19, akisema kuwa wamejipanga kuipeleka mahakama
mtandaoni ili kupunguza baadhi ya changamoto zinzoazoweza kujitokeza ikiwemo
Rushwa.
“Mahakama inaamini maisha yote ya
Binadamu yanaongozwa na Sheria, hivyo binadamu hawezi kuikwepa Sheria katika
maisha yake yote” alisema Jaji Mfawidhi Paul Ngwembe.
“katika maadhimisho haya Wiki ya Sheria Kituo
chetu cha haki jumuishi, tulikua na maeneo tofauti tofauti ya utoaji Elimu,
tulikua na Kituo pale viwanja vya Chamwino, pale Kituo cha mabasi Msamvu,
Kiwanja cha Ndege pale Fire, Soko kuu la Chief Kingalu, tumetembelea Shule za
Msingi Saba, Sekondari Nne, Chuo cha ualimu Kigurunyembe na magereza yote
mawili ambapo ni Gereza la Mahabusu na Gereza la mtego wa Simba’’ aliongeza
Jaji Ngwembe
Serikali ya Mkoa wa
Morogoro ilitoa ahadi ya kuendelea kuwezesha miundombinu ya mawasiliano katika
Mkoa wa Morogoro ili kufanikiwa kwa Mahakama ya kidijitali, alitoa ahadi hiyo Mkuu
wa Wilaya ya Morogoro ALBERTH MSANDO aliyemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
“Nichukue fursa hii kuahidi kwamba
tutahakikisha tunashirikiana na Mahakama kufikia malengo yake, tunapozungumzia Mahakama
ya kidijitali haiwezi kufanikiwa kama hatutaweka Miundombinu ya mawasiliano
katika maeneo yote, Serikali imeendelea kuwa na mpango wa kuhakikisha kwamba
katika vijiji vyote kunakua na mawasiliano ya Internet (mtandao) kutoka kwenye
vyombo vyetu vya mawasiliano” alisema
Mkuu wa Wilaya Wakili Msomi, Alberth Msando.
MARIAMU KAPAMA ni
Mwenyekiti msaidizi wa Chama cha wanasheria wa kujitegemea TLS Mkoa wa
Morogoro, alisoma Hotuba yao ambapo Pamoja na mambo mengine alieleza athari za
UVIKO 19 ilivyoathiri utendaji kazi na kuleta madhara kwa baadhi ya wapendwa
wao, akiishauri Mahakama kuitumia Teknolojia vema katika kukabiliana na janga
hilo.
Hotuba ya Ofisi ya
Mwanasheria mkuu wa Serikali, ilisomwa na Wakili Mfawidhi Mkoa wa Morogoro
XAVIER NDALAHWA, Akiahidi Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaendelea
kuboresha mfumo wa TEHAMA ili kuunga mkono jitihada za Mahakama.
“Niseme tu kwamba, tumeshuhudia
matumizi ya Mtandao, kusajili na kusikiliza mashauri yakifanikisha katika
utoaji wa Haki hasa katika kipindi cha Uviko 19, ambapo mashauri yalisikilizwa
bila msongamano Mahakamani, mfumo wa mahakama umelea faida kubwa ikiwa ni
pamoja na kuokoa muda na gharama” alisema Xavier Ndalahwa.
Maudhui mengine na jumbe
za Siku ya Sheria nchini yamepambizwa na burudani mbalimbali kutoka kwa
wanamuziki na wanasanaa, CHEDY ELLY SENZIGE ni mtunzi kutoka Morogoro alisoma
Shairi maalumu la Siku ya Sheria.
‘’zama za mapinduzi ya nne ya viwanda, safari
ya maboresho kuelekea mahakama mtandaoni’’ ndio kaulimbiu ya Siku ya Sheria
itakayodumu kwa Mwaka wote wa 2022.
Na Hamad Rashid- Morogoro.